HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 2 October 2019

AFISA TARAFA ITISO: TUTATUMIA MAKUNDI YA NGOMA ZA ASILI KUHAMASISHA NA KUELEZA UMUHIMU WA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

Afisa Tarafa Remidius Emmanuel akizungumza na baadhi ya vikundi vya Sungusungu pamoja na wananchi wa kata ya Itiso wakati wa tamasha dogo la utamaduni lililoandaliwa na viongozi wa kabila la Wagogo wa Tarafa ya Itiso na kufanyika  katika Kijiji cha Mapanga (Makulu).
 Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Tarafa ya Itiso A/Insp. Mohamed Ally akitoa neno kwa wananchi pamoja na baadhi ya vikundi vya Sungusungu wakati wa tamasha dogo la utamaduni lililoandaliwa na viongozi wa kabila la Wagogo wa Tarafa ya Itiso na kufanyika  katika Kijiji cha Mapanga (Makulu)
 Kiongozi wa Kabila la Wagogo Tarafa ya Itiso, Chief Mahemu Izidoli Maope akizungumza wakati wa tamasha dogo la utamaduni lililoandaliwa na viongozi wa kabila la Wagogo wa Tarafa ya Itiso na kufanyika  katika Kijiji cha Mapanga (Makulu)
Afisa Tarafa  Itiso Remidius Emmanuel akiwa kwenye picha ya pamoja na uongozi wa kabila la Wagogo  wa Tarafa ya Itiso mara baada kumalizika kwa tamasha dogo la utamaduni lililoandaliwa na viongozi wa kabila la Wagogo wa Tarafa ya Itiso na kufanyika  katika Kijiji cha Mapanga (Makulu).

AFISA Tarafa  Itiso  Remidius Emmanuel amesema kuwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotegemewa kufanyika November mwaka huu, ngoma za asili zitatumika kuhamasisha umuhimu wa wananchi kushiriki.

Hayo ameeleza  katika tamasha dogo la utamaduni lililoandaliwa na viongozi wa kabila la Wagogo (Tarafa ya Itiso) wakiongozwa na  Chief  Mahemu Izidoli Maope  kiongozi wa kabila hilo ngazi ya Tarafa lililofanyika  katika Kijiji cha Mapanga (Makulu)  na kuhusisha  makundi ya ngoma za Utamaduni (Kata ya Itiso), Makundi ya Sungusungu na baadhi ya viongozi wa Serikali za Vijiji, Kata, Tarafa pamoja na wananchi wa Kijiji hicho.

Amesema kuwa licha ya juhudi na hamasa zinazoendelea kwa  kuwahimiza wananchi   kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika 24.11. mwaka huu,  bado upo umuhimu mkubwa wa kufikisha elimu na kupitia sanaa ya ngoma  za asili.

Amesema kuwa makundi ya sanaa hususani ngoma za asili katika Tarafa  ya Itiso yana mchango mkubwa katika kuhamasisha shughuli za maendeleo.

"Wote mnafahamu kwamba tunaendelea na hatua mbalimbali za maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, na moja kati ya sifa za mpiga kura ni lazima awe amejiandikisha kupiga kura katika kitongoji au mtaa husika, kwa hiyo ni jukumu letu kuendelea kuhamasisha  wananchi wenye sifa kujiandikisha pale tu zoezi litakapoanza rasmi, nimeona upo umuhimu wa kutumia makundi haya ya ngoma za asili kuongeza hamasa juu ya zoezi hili, Tazama kwa muda mfupi ngoma yao nimesikia wakieleza mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano,wamehimiza uzalendo na uchapa kazi" ameeleza.

Hata hivyo amesema; pamoja na mambo mengine kwa sasa Tarafa ya Itiso inaendelea na zoezi la kutambua makundi yote ya sanaa katika tarafa  hiyo yakiwemo makundi ya ngoma za asili, na kwamba hiyo ni hatua muhimu kuelekea tamasha kubwa la utambuzi wa makundi ya sanaa katika Tarafa ya Itiso.

"Ninaamini kabisa kwamba huku vijijini vipo vipaji vingi sana ila vimejificha, ni vigumu sana kuonekana, lakini sisi viongozi ni jukumu letu kuibua vipaji hivyo ili dunia itambue uwepo wenu na nyinyi muingie katika ushindani na kuongeza kipato kupitia vipaji vyenu. Katika hili nimedhamiria kabisa  nitaomba ushirikiano kwa kila mmoja wetu" amesema.

Akitoa rai kwa makundi ya sungusungu yaliyoshiriki katika tukio hilo, AfisaTarafa huyo amepongeza kazi kubwa inayofanywa na  makundi hayo, ingawa amekemea baadhi yao kutumia kofia ya sungusungu kuwanyanyasa wananchi na amewataka wale wote  wenye tabia za namna hiyo kuacha mara moja na badala yake wafanye kazi zao kwa  weledi na uzalendo.

 Mkuu wa Kituo cha Polisi kata ya Haneti A Inspekta. Mohamed Ally   amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi na kusema jeshi la polisi litaendelea kuwachukulia hatua wale wote watakao endelea kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani, na amewataka wananchi wa Tarafa hiyo kuendelea kutoa ushirikiano pale wanapobaini uwepo wa wahalifu katika maeneo yao.

Kwa upande wake Chifu Mahemu Izidoli Maope ambaye ni kiongozi wa Kimila wa Kabila la Wagogo Tarafa ya Itiso,mbali na kumshukuru kiongozi huyo kwa ushiriki wake katika tukio hilo, amesema msingi wa matukio hayo ni kuendelea kukumbushana tamaduni zetu ambazo ndio asili ya utanzania wetu na wakati wote kuendelea kuhamasisha shughuli mbalimbali za ki-maendeleo.

"Katika  Wilaya ya Chamwino Tarafa ya Itiso ni miongoni mwa Tarafa yenye vikundi vingi vya ngoma za asili, ikiwa makundi haya yatatumika vema yatasaidia sana kukemea maovu jamii zetu na kuhimiza maendeleo katika nyanja mbalimbali" ameeleza Chifu Mahemu.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad