Wanafunzi wa darasa la saba 29,264 wanatarajia kufanya mtihani wa
kuhitimu elimu ya shule ya msingi kwenye Halmashauri saba za wilaya
kwenye Mkoa wa Manyara.
Katibu Tawala wa mkoa wa Manyara, Missaile Mussa alisema mitihani hiyo
inafanyika kwa muda wa siku mbili za jumatano na alhamisi.
Mussa alisema kati ya wanafunzi hao 29,264 wanaotarajiwa kufanya
mitihani wasichana ni 15, 502 na wavulana ni 13,762
Alisema wanafunzi hao wanatarajiwa kufanya mtihani huo kwenye shule
606 zilizopo kwenye halmashauri saba za wilaya ya Babati mji,
halmashauri ya wilaya ya Babati, Kiteto, Simanjiro, halmashauri ya
wilaya ya Mbulu, Hanang' na Mbulu mji.
"Tumejipanga vizuri kuhakikisha unafanyika ipasavyo, hatuna mashaka,
usalama utakuwepo wakati wote wanafunzi wamejiandaa na mtihani na
wasimamizi tuliwapa semina ya namna ya kusimamia," alisema Mussa.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto, Tamim Kambona
alisema wanafunzi 3,808 wanatarajia kufanya mtihani huo kwenye shule
za msingi 87.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga
alisema wanafunzi 3,900 watafanya mtihani kwenye shule za msingi 88
zenye mikondo 177.
Mkurugenzi wa mji wa Babati, Fortunatus Fwema alisema wanafunzi 2,171
watafanya mtihani kwenye shule za msingi 39.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Yefred
Myenzi alisema wanafunzi 3,243 watafanya mtihani huo kwenye shule za
msingi 81.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Babati, Hamis Malinga
alisema wanafunzi 7,213 wakiwemo wavulana 3,225 na wasichana 3,988
wanatarajia kufanya mtihani kwenye shule 141.
No comments:
Post a Comment