UONGOZI WA WAFANYAKAZI DAWASA WATEMBELEA MIRADI YA JAMII NA MAJITAKA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, 7 September 2019

UONGOZI WA WAFANYAKAZI DAWASA WATEMBELEA MIRADI YA JAMII NA MAJITAKA

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASA) Neli Msuya akizungumza na uongozi wa wafanyakazi wa DAWASA FIBUCA na TUICO kabla ya kuanza ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya majisafi na majitaka.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii wa Mamlaka ya majisafi na majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Neli Msuya akielezea mradi wa kuchakata majitaka wa Toangoma baada ya kutembelewa na Uongozi wa vyama vya wafanyakazi wa DAWASA vya FIBUCA na TUICO wakati wa ziara ya kutembelea miradi mbalimbali. Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Neli Msuya akielezea mradi wa majitaka Vingunguti uliowezesha kujenga vyoo 117 kwa wananchi wanaoishi maeneo ya karibu na mabwawa ya kuchakata majitaka na kupunguza magonjwa ya mlipuko.
Uongozi wa Vyama vya wafanyakazi wa mamlaka ya Majisafi an Majitaka Dar es Salaam wa FIBUCA na TUICO wakitembelea miradi mbalimbali ya maji safi na majitaka.
Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
Uongozi wa Vyama vya wafanyakazi wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) FIBUCA na TUICO wametembelea miradi mbalimbali ya Mamlaka hiyo inayopatikana ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na kufurahishwa na hatua zinazofanywa na Menejimenti inayoongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu Mhandisi Cyprian Luhemeja.

Ziara hiyo imehusisha miradi ya maji ya jamii na miradi ya kuchakata maji taka ya Vingunguti na Toangoma.

Akizungumza baada ya kutembelea miradi hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi FIBUCA Eli Achahofu amesema kuwa wamefurahi sana kutembela miradi ya Dawasa ambapo itakapokuja kukamilika itamtua mama ndoo kichwani.

Amesema,” miradi yote ni mizuri hususani huu wa Vijibweni ambao utakapokuja kukamilika kero ya maji kwa wakazi wa Kigamboni itakuwa historia,”

Achahofu ameeleza kuwa, wamepata elimu kubwa sana katika ziara hiyo, na Mamlaka imepiga hatua kubwa sana katika mradi wa kuchakata maji taka na hilo limesaidia hata kupunguza magonjwa ya mlipuko ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

“Kuna vyoo 117 vimejengwa na Dawasa kwa wananchi wanaoishi Vingunguti karibu na mabwawa ya kumwaga majitaka, walielimishwa wakaelewa na kwa sasa wanaishi vizuri, vyoo vyao ni vizuri na hilo limepunguza hata magonjwa ya mlipuko ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam,”

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii DAWASA Neli Msuya amesema miradi ya jamii yote iliyokuwa chini ya Halmashauri pamoja Jumuiya za watumiaji maji kuanzia sasa zitakuwa chini ya Mamlaka hiyo ikiwano na visima vya watu binafsi.

Amesema, hatua hiyo itasaidia kufikisha maji kwa wananchi waliopo nje ya mtandao wa Dawasa ambapo visima hivyo vimekuwa na msaada mkubwa sana ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

“Miradi ya watumiaji maji na ile halmashauri imekuja chini yetu Dawasa, kuanzia sasa tutaiendesha na kuboresha huduma na zaidi vipo visima vya watu binafsi ambavyo na vimesaidia wananchi kwa kipindi kirefu kupata huduma ya maji,”amesema Msuya.

“Mradi wa majitaka ambapo upo Vingunguti ambapo ni mradi mkubwa wa kuwajengea vyoo wananchi wapo waliokubali na wengine walikataa lakini mfumo uliopo ni kuwa vyoo hivyo mtu anapokitumia maji hayakai pale bali yanaenda moja kwa moja mpaka kwenye mabwawa yetu ya majitaka na hilo limesaidia sana kuondokana na magonjwa ya mlipuko,”amesema

Naye Mkazi wa Vingunguti Nuru Selemani ameishukuru Dawasa kwa kuweza kuwajengea vyoo vizuri na hatua hiyo imeweza kupunguza magonjwa ya mlipuko na pia vinadumu kwa muda mrefu.
Ameeleza kuwa kabla ya kujengewa vyoo hivyo , walikua wanatiririsha majitaka wakati wa mvua tena kwa kujificha nyakati za usiku ila mpango ulioletwa na Dawasa wa kuwajengea vyoo umesaidia sana na hata sasa watoto wao hawaumwi mara kwa mara.

Nuru amewashauri wananchi wengine wa maeneo hayo ambao hawajajengewa vyoo waweze kukubali ili waondokane na adha ya majitaka.

Uongozi huo wa Wafanyakazi uliweza kutembelea miradi ya jamii ya watumia maji Domu, Mradi wa watumia maji Moringe na Mradi wa Vijibweni na kwa upande wa majitaka walitembelea mabwawa ya Vingunguti na Mradi wa kuchakata majitaka Toangoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad