Spika Ndugai kuongoza matembezi yahisani Dodoma - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 11 September 2019

Spika Ndugai kuongoza matembezi yahisani Dodoma

·Ni Kwa ajili ya utanuzi wa kituo cha afya cha St Lukes

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai anatarajiwa kuongoza mamia ya wakazi wa Dodoma katika matembezi ya hisani ili kuchangisha fedha za kutanua na kuboresha Kituo cha cha afya cha St. Lukes (Mpwapwa).

Matembezi hayo yatafanyika Jijini Dodoma Jumamosi hii Septemba 14, 2019 kuanzia Uwanja wa Jamhuri saa kumi na mbili na nusu asubuhi na kuishia Nyerere Square ambapo Spika ataendesha zoezi la kuchangia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Tom Mazanda alisema huu ni uzinduzi wa chagizo ambalo litakuwa endelevu kabla ya kufanyika harambee kubwa Jijini Dar es Salaam mwezi ujao ambapo mgeni rasmi ni Rais Mstaafu Mh Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.

“Tshirt za uhiriki tayari zimeanza kuuzwa Jijini Dodoma kwa Tsh 25,000 ambapo washiriki watatakiwa kuzivaa wakati wa matembezi siku ya Jumamosi,” alisema na kutoa wito kwa wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha zoezi hili muhimu kwa wakazi wote wa Dodoma kwani kituo hicho cha afya kinatumiwa na watu kutoka sehemu mbalimbali nchini kutokana na kuwa na daktari mahiri.

Alisema mradi huo utahusisha ujenzi wa wodi ya wanawake na watoto, upanuzi wa maabara, kununua vifaa vya afya na kuongeza watendaji huku akibainisha kuwa shughuli ya matembezi na chagizo inaratibiwa na Kampuni ya Energia ya Jijini Dar es Salaam.

Kwa wanaochangia kupitia benki, mwenyekiti huyo alisema namba za akaunti ni CRDB-MPWAPWA BRANCH ST. LUKES UJENZI A/C-0150507423904 na NMB MPWAPWA BRANCH ST LUKES UJENZI A/C- 50410011146 na kwa wale ambao wangependa kuchangia kwa njia ya simu namba za kutuma mchango ni 0754-363405, 0786-149840 na 0713-014681.

"Tunatoa wito kwa taasisi mbalimbali, mashirika, viongozi na wananchi kwa ujumla washiriki vikamilifu ili  zoezi hili liwe na mafanikio," alisema.

Naye Askofu wa Dayosisi ya Mpwapwa, Dr Jacob Chimeledya alitoa wito kwa wakazi wote wa Dodoma wakiwemo wabunge kushiriki vikamilifu ili waweze kutimiza malengo ya matembezi hayo.

“Mradi huu utakuwa na faida kubwa kwa wana Dodoma kwa ujumla bna sio wakazi wa Mpwapwa tu. Mahitaji yamekuwa makubwa kwa maana hiyo rasilimali zilizopo hazitoshi kuhudumia mamia ya watu wanaohitaji huduma katika kituo chetu ndio maana tumeamua kufanya mradi huu wa utanuzi,” alifafanua.

Alisema kituo kilisajiliwa rasmi mwaka 1993 kama zahanati kutoka kwa Wamishionari wa CMS walioanzisha huduma za afya katika eneo hilo toka mwaka 1876. Kituo cha Afya cha St Lukes kwa sasa kinahudumia wastani wa wagonjwa kati ya 50 na 60 kwa siku, wanawake wanaojifungua kwa mwaka ni kati ya 550 na 600.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Kituo hicho, Dk Edwin Kiula, wanawake wanaotibiwa magonjwa mengine ya akina mama ni zaidi ya 400 na watoto wanaolazwa ni wastani wa 300 kwa mwaka, wakati wagonjwa wanje (OPD) kwa ujumla ni 11,000 hadi 13,000 kwa mwaka kliniki ya wajawazito na watoto ina wastani wa mahudhurio 18,000 hadi 20,000 kwa mwaka.

Magonjwa yanayotibiwa sana katika kituo hicho ni maradhi ya via vya uzazi (PID), numonia kwa watoto, kuhara na malaria, aliongeza Dr Kiula.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad