HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 4, 2019

MALINZI AIOMBA MAHAKAMA KUMUACHIA HURU KWANI HANA HATIA

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

ALIYEKUWA Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi ameendelea kujitetea na kuiomba  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumuachia huru kwa sababu hana hatia katika mashitaka 16 yanayomkabili ikiwemo ya utakatishaji fedha.

Malinzi amedai hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde wakati akijitetea. Akiongozwa na Wakili Richard Rweyongeza, Malinzi amedai wakati wa uongozi wake ndani ya TFF na taasisi zingine katika maisha yake hakuwahi kushiriki kutakatisha fedha.

Amedai, katika mashitaka ya utakatishaji yanaonesha kwamba alitakatisha Sh 43,100,000 kutokana na mashitaka ya kughushi ambayo  mahakama hiyo haijamuona kuwa na kesi ya kujibu.
Pia amedai  jumla ya fedha zilizoandikwa kwenye mashitaka ya kughushi si Sh 43,100,000 badala yake ni Sh 37,100,000 hivyo idadi iliyowekwa kwenye mashitaka hajui imetokea wapi.

Malinzi amedai fedha anazodaiwa kuzitakatisha alizipata kwa utaratibu halali wa TFF kwani zipo nyaraka mbalimbali zilizowasilishwa mahakamani hapo ikiwemo risiti na nyaraka za benki zinazothibitisha kwamba alipokea fedha kihalali.

Ameeleza kuwa, mpaka Desemba 31,2016  yeye ndio anayeidai TFF na kwamba katika mashitaka ya 15 hadi ya 26 ni ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na sio ya kughushi na mashitaka ya kughushi aliyonayo hayajaonesha kama alipata kitu chochote kutokana na makosa hayo.

Malinzi amedai  alifanya mabadiliko ya mtia saini kutoka Edger Masoud kwenda kwa Nsiande Mwanga kihalali kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa Katiba na kanuni za TFF na  si mamlaka ya kamati tendaji kujadili mtia saini badala yake ni Rais ndio anateua mtia saini na kupeleka katika bodi ya maamuzi kwa ajili ya kujadili na kisha hupelekwa benki.

"Nilisaini maamuzi ya kubadili mtia saini kwa mujibu wa katiba ya TFF kuonesha kuwakilisha shirikisho. Sikunufaika na kitu chochote kutokana na kubadilisha mtia saini badala yake mabadiliko haya yalinufaisha wengi," amedai Malinzi.

Pia amedai muhtasari wa Juni 5,2016 uliowasilishwa mahakamani hapo si sahihi na kwamba orodha sahihi ya wajumbe waliohudhuria kikao cha TFF inapatikana kwenye kitabu cha muhtasari na kwamba katika kikao hicho, mashahidi waliokuwepo hawakuhudhuria.

Amedai Mwanga hakuhusika kwa namna yoyote kuandaa maamuzi ya bodi na wala hakushiriki katika kufanya maamuzi kwani alikuwa mwajiriwa kama wengine.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mtendaji wa TFF, Selestine Mwesigwa, Mhasibu wa TFF Nsiande Mwanga na  Karani Flora Rauya.

Kesi hiyo ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 20 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa Dola za Marekani 173,335.

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa sababu mmashitaka ya utakatishaji  fedha kuwa miongoni mwa mashitaka  ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana huku Rauya akiwa  nje kwa dhamana.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad