HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 28, 2019

RAIS DKT. SHEIN AZUNGUMZA NA UONGOZI WA WIZARA YA BIASHARA NA VIWANDA ZANZIBAR


 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar ,wakati wa mkutano wa Utekelezaji wa Bajeti na Mpango Kazi wa Wizara hiyo juazia mwezi  wa Julai 2018 hadi Juni 2019, uliofanyika ukumbi wa Ikulu Zanzibar , kushoto kwa Rais Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi na kulia kwa Rais Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.(Picha na Ikulu)
 WAZIRI wa Biashara na Viwanda Zanzibar Mhe. Balozi Amina Salum Ali akiwasirisha mutasari wa Utekelezaji wa Bajeti na Mpango Kazi wa Wizara yake kwa mwezi wa Julai 2018 hadi Juni 2019, kulia Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Abdulhamid Yahya Mzee na kushoto Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh, uliofanyika ukumbi wa Ikulu Zanzibar ukiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, hayupo pichani.
 MKURUGENZI wa Taasisi ya Viwango Zanzibar  (ZBS)  Ndg .Khatib Mwadin  akijibu swali wakati wa mkutano wa Utekelezaji wa Bajeti ya Mpango Kazi kwa mwezi Julai 2018 hadi Juni 2019, uliofanyika ukumbi wa Ikulu Zanzibar, ukiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, (hayupo pichani  kulia Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Zanzibar (ZSTC) Dk. Said Seif Mzee
 NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar Bi. Khadija Khamis Rajab wa kwanza kushoto akisoma taarifa ya Utekelezaji Bajeti na Mpango Kazi ya Wizara yake kwa mwezi wa Julai 2018 hadi Juni 2018, wakati wa mkutano huo uliofanyika Ukumbi wa Ikulu Zanzibar ukiongozwa na Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein.
 BAADHI ya Watendaji wa Idara za Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar wakifuatilia taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti na Mpango Kazi kwa Wizara yao kwa mwezi wa Julai 2018 hadi Juni 2019, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.
 MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) Ndg Maalim Kassim Suleiman, akizungumza wakati wa mkutano wa Utekelezaji wa Bajeti na Mpango Kazi wa Wizara ya Biashara na Viwanda kwa mwezi wa Julai 2018 hadi Juni 2019, uliofanyika ukumbi wa Ikulu Zanzibar, ukiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, hayupo pichani.
 MSHAURI wa Rais Pemba Mhe.Dk. Maua Abeid Daftari  akizingumza wakati wa mkutano wa Utekelezaji  wa Bajeti na Mpango Kazi  wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar uliofanyika ukumbi wa Ikulu Zanzibar, ukiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein. Hayupo pichani.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akizungumza wakati wa mkutano wa Utekelezaji wa Bajeti na Mpango Kazi wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar kwa mwezi Julai 2018 hadi Juni 2019, uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.(Picha na Ikulu) 


Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha sauti za Wajasiriamali zinasikika na zinafanyiwa kazi ili kufikia malengo waliyoyakusudia.

Rais Dk. Shein aliyasema, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda wakati ilipowasilisha Mpango Kazi wa Julai 2018 hadi Juni 2019 sambamba na Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa mwaka 2019/2020.

Alieleza kuwa matajiri walio wengi duniani walianza na ujasiriamali hivyo ni vyema wajasiriamali wakapewa kipaumbele katika shughuli zao wanazozifanya ili waweze kupata mafanikio na kufikia malengo yao waliyoyakusudia ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha kikamilifu katika maonesho ya kibiashara ya ndani na nje ya nchi.

Alieleza kuwa mbali ya matajiri hao duniani, hata hapa Zanzibar matajiri walio wengi wameanza na ujasiriamali hivyo, si jambo la busara kuwabeza  na badala yake ni vyema wakapema kipaumbele na mashirikiano ya kutosha. 

Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwasaidia wajasiriamali ili na wao waweze kuwa wafanyabiashara wakubwa na kufikia malengo waliojiwekea jambo ambalo limeiibua Serikali katika kuhakikisha inawatekelezea matakwa yao na kuwashirikisha kikamilifu

Pamoja na hayo Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda kwa kuwasilisha vyema Mpango Kazi wao na kueleza kuwa utendaji wao pamoja na wafanyakazi wa Wizara hiyo ndio uliopelekea kupata mafanikio 

Hivyo, Rais Dk. Shein aliutaka uongozi huo kuongeza kasi na kufanya kazi kwa bidii ili mafanikio zaidi yaendelee kupatikana katika kuimarisha sekta hiyo ambayo ina umhimu katika kuimarisha uchumi na kukzua sekta za kijamii.

Rais Dk. Shein alipongeza mafanikio makubwa yaliopatikana katika Wizara hiyo chini ya uongozi wa Waziri wake Balozi Amina Salum Ali ambaye amefanya juhudi kubwa ya kuiimarisha Wizara hiyo katika uongozi wake kwa mashirikiano ya pamoja na watendaji wake.

Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kuendelea kumsaidia Waziri wao huyo kila mmoja kwa wakati wake na nafasi yake kwa lengo la kuimarisha sekta ya biashara na viwanda kwani azma ya Serikali ni kuhakikisha Zanzibar inakuwa kwenye ramani ya viwanda.

Alieleza matumaini ya kuimarika kwa zao la mwani ambapo tayari kuna aina nne za mwani hapa Zanzibar na kueleza kuwa hatua hiyo itapelekea kupata mafanikio mazuri ya zao hilo ikiwa ni pamoja na mchakato wa kujenga kiwanda cha mwani huko Chamanangwe Pemba.

Alieleza kuwa Zanzibar ina historia kubwa ya kulima mazao mbali mbali yakiwemo ya viungo vya chakula kwa muda mrefu, hivyo ni vyema mazao hayo yakaimarishwa ikiwa ni pamoja na kuwashajiisha wakulima kuyalima vikiwemo viungo kama pilipili hoho.

Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kulima kwa wingi kwa viungo vya chakula kwa sababu vimekuwa vikipendwa sana nje ya nchi hivyo ni vyema kilimo hicho kikaimarishwa.

Aidha, alieleza kufarajika kwake na uongozi wa Wizara hiyo kwa kutumiwa alama ya ubora ya Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) katika bidhaa mbali mbali zinazozalishwa ndani na nje ya nchi huku akieleza azma ya Zanzibar kuwa nchi ya viwanda.

Makamo wa Pili wa Rais  wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd alitoa pongezi kwa uongozi huo na kuzipongeza juhudi za Waziri Balozi Amani Salum Ali za kuhakikisha  maendeleo yanapatikana katika sekta ya viwanda na biashara ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa  Mamlaka inayosimamia Viwanda vidogo vidogo na Vya Kati (SMIDA).  

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza kazi nzuri ya uwasilishaji iliyofanywa na Wizara hiyo huku akisisitiza haja kwa uongozi huo kuendeleza mashirikiano na uadilifu.

Mshauri wa Rais wa Zanzibar Pemba Dk. Maua Abeid Daftari kwa upande wake alitoa pongezi kwa Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) kwa kuendeleza zao la mchaichai kisiwani Pemba kwani wananchi wengi wamehamasika na kuomba wasaidiwe kuwekewa vinu karibu na sehemu wanazoishi. 

Mapema Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salaum Ali akiwasilisha muhtasari wa utekelezaji Mpango Kazi wa Wizara hiyo alisema katika kipindi cha mwaka 2018/2019 jumla ya tani 218,911 za chakula muhimu ukiwemo mchele, sukari na unga wa ngano zilikuwepo kwa ajili ya matumizi ya soko la ndani na kuifanya Zanzibar kuendelea kuwa na chakula cha kutosha cha aina hizo katika kipindi chote.

Alieleza kuwa sensa ya viwanda iliyofanyika mwaka 2016 ilionesha idadi ya viwanda imeongezeka  ambapo sukari imeongezeka kutoka tani 677 iliyozalishwa mwaka 2017 hadi tani 3,339 kwa mwaka 2018 sawa na ongezeko la asimilia 79.7 na uzalishaji wa unga wa ngano nao uliongezeka kutoka tani 25,196 mwaka 2017 hadi tani 26,963 mwaka 2018.

Balozi Amina alieleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2018/2019, Shirika la Biashara la Taifa limenunua karafuu tani 211.34 kwa jumla ya TZS Bilioni 2.9 ambapo pia uzalishaji wa mafuta ya mimea ulifikia kilo 40,955.3 kwa jumla ya TZS bilioni 1.5.

Alieleza kuwa Serikali inaendelea kununua karafuu kulingana na Sera ya Serikali ya kununua kwa bei ya asilimia 80 ya bei ya kuuzia nje hata hivyo, msimu mdogo wa karafuu kwa mwaka 2018/2019 ulipelekea kupungua kwa tani za ununuzi wa karafuu.

Kwa bajeti ya mwaka 2019/2020, alisema Wizara inakusudia kuimarisha maabara za ZBS zilizopo Amani pamoja na kuimarisha miundombinu, vifaa vya ukaguzi wa magari, kuliendeleza eneo la Nyamanzi sambamba na kuongeza vifaa kwa ajili ya matamasha.

Alieleza kuwa Wizara hiyo kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Indonesia inatarajia kufanya mafunzo ya ukulima wa mwani ulio na tija na kuanza maandalizi ya kuanzisha kiwanda cha kusarifu mwani huko Chamanangwe kisiwani Pemba.

Balozi Amina, alieleza mpango wa Wizara wa kusimamia program maalum ya wajasiriamali inayopata msaada kutoka mfuko maalum wa Nchi za Falme za Kiarabu pamoja na mchango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Alisisitiza kuwa ili kurahisisha ufanyaji biashara hapa Zanzibar, Wizara itaandaa mfumo maalum wa Tehama ambao utatoa taarifa na huduma muhimu za usajili, uwekezaji na leseni au vibali vinavyotakiwa kwa wawekezaji na wafanyabiashara.  

Pia, uongozi huo ulieleza juhudi inazozichukua kwa wafugaji wa nyuki kwa kuwapa mafunzo maalum  wafugaji  hao sambamba na kusimamia vyema ufugaji huo kwa lengo la kupata asali yenye ubora na viwango vinavyohitajika kitaifa na kimataifa. 

Uongozi huo pia, ulimpongezi Rais Dk. Shein kwa utaratibu mzuri alioweka wa mikutano hiyo inayojadili Mpango Kazi wa Mawizara huku wakitumia fursa hiyo kueleza sifa inazozipata Zanzibar kutoka kwa wageni wanaokuja kuitembelea kutokana na amani, utulivu, upendo pamoja na maendeleo yaliopo. 

Uongozi huo pia, ulizitaja bidhaa zilizizothibitishwa ubora na kupatiwa alama ya ubora ya (ZBS) kwa mwaka 2018/2019 ni maji ya kunywa ya (Zan Aqua), mchele (Tulip) unaozalishwa nchini Pakistan, mchele wa (Ikram), unga wa sembe (Mwangaza), Mikate ya slesi, maji ya kunywa (Pure life) na (Uhai), mafuta ya nazi na mifuko.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad