HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, July 12, 2019

Wakandarasi tumieni vijana wanaomaliza JKT, kujenga miradi ya umeme

Na Zuena Msuya, Kigoma
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewashauri wakandarasi nchini kuwatumia vijana wanaomaliza mafunzo katika jeshi la kujenga taifa wenye  taaluma na ujuzi mbalimbali ikiwemo sekta ya Nishati ya Umeme.

Mgalu alisema idadi kubwa ya vijana wanaohitimu mafunzo ya JKT wanakuwa na nidhamu, pamoja na uzalendo  katika kutekeleza majukumu yao  kwa maslahi ya Taifa.

Naibu Waziri alitoa ushauri huo alipokuwa akikagua maendeleo ya usambazaji wa Umeme vijijini katika kikosi Jeshi la Kujenga Taifa cha 825KJ Katika Kambi ya Mtabila, wilayani Kasulu mkoani Kigoma na kuzungumza na uongozi wa kituo hicho pamoja na Makuruta, Julai 11,2019. 
Aidha walishauri vijana wanaopata mafunzo ya jeshi kujifunza taaluma ya umeme wanapokuwa vyuoni ili kuwepo na mafundi mchundo wengi pale watakapohitajika kutumiwa na wakandarasi katika kujenga miradi ya umeme.

Aliongeza kuwa endapo kutakuwa na vijana wengi wzalendo katika taaluma hiyo, itasaidia kuondoa changamoto ya vishoka mitaani na watu wasiowaaminifu katika kutekeleza miradi ya umeme na mafundi mchundo katika kuwatanda nyaya kwenye nyumba za wananchi.
"Vijana wanaopitia mafunzo ya jeshi wengi huwa waadilifu na wazalendo kwa miradi inayotekelezwa katika nchi yao, hivyo nawashauri wakandarasi wote nchini kuwatumia vijana hao katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hasa ile yenye gharama kubwa na inayotumia fedha nyingi, kwa maslahi yao na nchi kwa ujumla", alisisitiza Mgalu.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa kikosi cha 825 KJ katika Kambi ya Mtabila, Meja  Peter Lyanga alimueleza Naibu Waziri Mgalu kuwa katika hiyo vijana wengi wanahitimu wakiwa na taaluma mbalimbali wakiwa na nidhamu ya hali ya juu hivyo amewatoa hofu wakandarasi juu wa vijana hao.
Aidha aliomba kuharakishwa kwa utekelezaji wa mradi wa umeme katika eneo hilo ili kambi hiyo iweze kupata huduma hiyo,ambayo itawasaidia vijana kuongeza ujuzi zaidi katika mafunzo yao yanayoendana na teknolojia ya kisasa zaidi. 

Katika hatua nyingine Mgalu aliwasha Umeme katika vijiji vya Wilaya za Kasulu na Buhigwe mkoani Kigoma na kuwataka wananchi kutumia Umeme huo kujiletea maendeleo. 
Katika Wilaya ya Kasulu, Mgalu aliwasha Umeme katika Zahanati ya Ruhita, Shule ya Sekondari ya Kasange pamoja na kijiji cha Ruhita.

Vilevile alizungumza na wakazi wa vijiji vya Shunga, Ruhita na Kasange ambapo pamoja na mambo mengine alimtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa usambazaji Umeme katika  vijiji hivyo kuongeza kasi zaidi kwani wananchi wamekuwawakiusubiri kwa muda mrefu.
Katika ziara hiyo pia, Mgalu alikagua kazi ya usambazaji wa umeme kijiji cha Nyankoronko wilayani  Buhigwe na kuwasha umeme katika jengo la halmashauri ya Wilaya hiyo na kuzungumza na wananchi wa wilaya hiyo.

Kwa upande wao, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Samson Anange  na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Michael Ngayalina waliwataka wananchi wa wilaya hizo  kutunza miundombinu ya umeme iliyopo katika maeneo yao wakati wakiendelea kusubiri hadi pale watakapowafikiwa na mradi huo katika nyumba zao.

Pia amewataka kutoa ushirikiano wa nguvu kazi hasa kwa vijana pale ambapo wakandarasi watakuwa wakiwahitaji vijana hao kwa kuwa watapata ajira za muda mfupi na kukidhi mahitaji yao. 
Sambasamba na hilo waliwasisitiza wakazi wa wilaya hizo kuwa wasikubali kulipa gharama za kuunganishiwa umeme kwa zaidi ya shilingi 27,000 wala kuuziwa vifaa vya umeme kama vile nguzo pamoja na LUKU.
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na makuruta wa kikosi cha 825KJ katika kambi ya Mtabila wilayani Kasulu mkoani Kigoma, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini katika wilaya hiyo.
 Makuruta wa kikosi cha 825KJ kambi ya Mtabila wilayani Kasulu mkoani Kigoma wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, hayupo pichani, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini katika wilaya hiyo.
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( katikati) akizungumza na mkazi wa kijiji cha Ruhita,wilayani Kasulu, mkoani Kigoma, kabla ya kukata utepe kuwasha umeme katika nyumba yake ikiwa ni ishara ya kuwasha umeme katika kijiji hicho. 
 Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu,( katikati) akimkabidhi kifaa cha umeme tayari( UMETA) mama mwenye ulemavu,Merania Katekwa, mkazi wa Kijiji cha Nyankoronko wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, ambaye hana uwezo wa kulipia gharama za kuunganisha umeme licha ya  nyumba yake kukidhi viwango  na kupitiwa na mradi wa usambazaji umeme vijijini.
Akina mama wa kijiji cha Shunga, Kasulu mkoani Kigoma, wakifurahi na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, alipowaeleza kuwa umeme katika kijiji hicho utafika hivi karibu na tayari mkandarasi anaendelea na kazi ya kusimika nguzo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad