HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 17, 2019

Wakandarasi msikumbatie kazi- Subira Mgalu

Zuena Msuya, Tabora,
Naibu wa Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka wakandarasi ambao wanadhani hawatakamilisha ama kuchelewesha kazi ya usambazaji wa umeme  vijijini  kutokana na changamoto mbalimbali , ni vyema kazi hizo wakapatia wakandarasi wenye uwezo ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati.

Akizungumzia kazi ya kusambaza umeme vijijini katika maeneo aliyotembelea mkoani Tabora, Julai 16, 2019, Mgalu alisema kuwa kuna baadhi ya wakandarasi wamekuwa  hawaendani na kasi inayotakiwa katika kutekeleza mradi huo,na kwamba wamekuwa na sababu nyingi za kujitetea licha ya awali kuonyesha kuwa na uwezo wa kufanya kazi hizo.

Aliweka bayana kuwa kasi ndogo ya utekelezaji mradi huo ikilinganishwa na kipindi kilichowekwa kuukamilisha, inaonyesha wazi kabisa kuwa wakandarasi hao hawatamaliza kazi hiyo kwa wakati uliopangwa na hivyo kurudisha nyuma juhudi za serikali katika kutimizma yake ya kuwapatia umeme wananchi wote .

“Kuna wakandarasi ambao walianza vizuri lakini sasa wanasuasua kutokana na changamoto mbalimbali, usikumbatie kazi igawe kwa wenye uwezo, usisubiri jumba bovu likuangukie,Serikali wala Wizara ya Nishati hatutakubali kurudishwa nyuma, ukishindwa ama kuchelewesha sheria itachukuwa mkondo wake kwa kuwa fedha nyingi zimetengwa kwa ajili ya kuwapatia wananchi umeme,”alisisitiza Mgalu.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Mgalu aliwasha umeme katika baadhi ya nyumba za kijiji cha Itundaukulu pamoja na Zahati ya kijiji hicho, pia katika shule ya msingi ya Simbo pamoja na kuwasha umeme katika baadhi ya nyumba katika Kijiji cha Simbo wilayani Uyui, Tabora.

Aidha alikemea tabia ya baadhi ya wakandarasi wanaondoka katika eneo la mradi mara baada ya kijiji husika kuwashwa umeme, badala ya kubaki na kuendelea na kazi ya kuwaunganishia wananchi wengine waliokwisha lipitia huduma hiyo, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa sana na wananchi.

Aliwagiza viongozi wa Serikali za mitaa na vijiji kuwa walinzi wa wakandarasi hao, na wahakikishe kazi ya uunganishwaji wa wananchi inaendelea, na endapo mkandarasi atalazimika kuondoka  eneo la mradi, basi kuwepo na  sababu maalum na watoe taarifa kwa uongozi wa Vijiji.

“Nasikitishwa sana na baadhi ya wakandarasi, wakiona umeme umeshawashwa katika kijiji na wao wanaondoka eneo hilo, nawaeleza ukweli wakadarasi timizeni wajibu wenu kulinga na makubalino ya mikataba na kutekeleza maagizo mbalimbali mnayopewa, tabia hii hatutaivumilia, fanyeni kazi kwa mujibu wa mikataba muwatendee haki watanzania na taifa kwa ujumla,”  alisisitiza Mgalu.

Aidha amefafanua kuwa bei ya kuwaunganishia wananchi umeme vijijini ni shilingi 27,000 tu,  bei hii itandelea kutumika hata pale Mradi wa REA utapokamilika na kazi hiyo wakapewa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuendelea na kazi hiyo, hivyo wanachi wote waendee kuunganishwa lengo ni kuwafikia wananchi wote.

“Hapo awali ilikuwa ,mara baada ya mradi wa REA kukamilika katika eneo husika kazi ya uunganishaji wananchi inakabidhiwa kwa Tanesco, na bei ya kulipia gharama hiyo ilikuwa ni zaidi ya 170,000/=, sasa serikali imesema hapana bei ibaki ileile shilingi 27,000 kwa wananchi wote wa vijijini,” alisema Mgalu

Vilevile aliwatoa hofu wananchi kuwa, mara baada ya mradi wa REA kukamilika, serikali imeanzisha mradi mwingine wa ujazilizi ambao utakuwa ukiendelea na kazi ya kusambaza umeme kwa wananchi ambao hawakuweza kufukiwa na REA, na mradi huyo utahusisha mikoa mbalimbali.
 Mateso Juma( kulia) mwenye ulemavu wa ngozi , mkazi wa kijiji cha Kijiji cha Ifucha katika Halmashauri ya Tabora mjini, akiwa ameshikilia kifaa cha umeme tayari( UMETA) baada ya kukabidhiwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( kulia). Serikali iliagiza kuwa licha ya UMETA kugaiwa bure kwa wateja 250 wa mwanzo watakaounganishiwa umeme,kipaumbele kiwe kwa wazee wasiojiweza, wajane, na walemavu.
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wakazi wa kijiji cha Itundaukulu wilayani Uyui, mkoani Tabora (hawapo pichani) Naibu Waziri yupo mkoani Tabora kwa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini REA.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu(kutoka kulia)akipokea barafu(ice cream) na soda baridi kutoka kwa mama mjasiriamali (kushoto) anayefanya biashara hiyo baada ya kufungiwa umeme wa REA katika kijiji cha Simbo  wilayani Uyui, mkoani Tabora.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad