Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amewataka Wakurugenzi wa
Halmashauri kupitia kwa wahandisi wa ujenzi kuwatambua na kuwajengea
uwezo mafundi wote wanaotoka kwenye jamii wanaofanya kazi za serikali
kwa kutumia mfumo wa ujenzi usiotumia wakandarasi (Force Account)
hususani waliofanya kazi nzuri kwenye ujenzi wa hospitali za wilaya ya
Mkoa wa Simiyu.
Mtaka ameyasema hayo mara baada ya kufanya ziara katika hospitali za
wilaya ya Itilima, Bariadi na Busega zinazoendelea kujengwa lengo ni
kujua hatua ziizofikiwa katika ujenzi, ambapo amesema mafundi hao
wakitambuliwa na kujengewa uwezo utendaji wao utaimarishwa na kazi
watakazofanya zitafanywa katika ubora.
“Ni lazima kama Mkoa tuwe na mfumo wa kuwatambua mafundi wote
waliofanya kazi ya kujenga hospitali zetu zote tatu na tuanze
kuwajengea uwezo,ili miradi yetu ya Serikali tunayoendelea kuifanya
tusiwe na watu wapya sana na kama tukipata wapya watakuwa wanafanya
kazi chini ya uangalizi wa watu wenye uwezo mzuri zaidi” Mtaka
Mbali na hayo amezipongeza wilaya hizo kwa mfumo walioutumia wa
kununua vifaa kiwandani moja kwa moja kwani umesaidia kuokoa fedha
nyingi ambazo zimefanikisha ujenzi kufikia katika hatua nzuri, huku
akizisisitiza wilaya hizo kuwashirikisha Wakala wa Ufundi na Umeme
(TEMESA) kwenye ununuzi wa vifaa vya umeme ili kupunguza gharama
zisizo za lazima.
Kwa upande wao Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya SACF James John
(Bariadi) Elizabeth Gumbo (Itilima) wamesema kuwa miongoni mwa
changamoto zilizopelekea kutokamilisha kwa miradi hiyo ambayo
ilitakiwa kukamilika Juni 30 , 2019 ni fedha kutotosheleza na
kusisitiza kuwa ikiwa watapokea fedha mapema watakamilisha majengo
yote.
“Tulipokea bilioni 1.5 tumebakiwa na shilingi milioni 75 kwa ajili ya
kulipa mafundi tulioingia nao mkataba, ili tuweze kukamilisha hatua
zilizosalia katika ujenzi wa majengo saba ya awali tunahitaji shilingi
milioni 370” alisema James John mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya
Bariadi.
“Tulipokea shilingi bilioni 1.5 tumebakiwa na shilingi milioni ambazoo
zimetengwa kwa ajili ya malipo ya mafundi, tukiongezewa shilingi
milioni 360 tutamaliza majengo kwa hatua zilizobaki” alisema Elizabeth
Gumbo mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Itilima.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Busega Tano Mwera amebainisha kuwa kwa
hatua walioyofikia fedha zinatosha kukamilisha mradi na kwamba
changamoto iliyopelekea wasiweze kukamilisha kwa wakati ni
ucheleweshwaji wa mfumo na kwamba ikifanyiwa kazi mradi utakamilika
kwa wakati.
Naye Katibu Tawala wa mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesisitiza
Halmashauri za Wilaya ya Bariadi, Busega na Itilima kumalizia ujenzi
wa Hospitali za wilaya kwa wakati ambapo pia alitoa rai ya kuhakikisha
barabara zinatengenezwa, miti na bustani za maua zinapandwa katika
maeneo hayo ambayo hospitali hizo zinajengwa.
Katika ujenzi wa hospitali za wilaya ya Bariadi, Itilima na Busega
ambao ni wa awamu ya kwanza kuna jumla ya majengo takribani ishirini
na moja yanapaswa kujengwa (21) ikiwa ni majengo saba kwa kila
Hospitali (kwa awamu ya kwanza) ambayo yapo katika hatua mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto) akizungumza na Viongozi wa Wilaya ya Busega, Itilima na Bariadi katika majumuisho ya Ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa katika Hospitali za Wilaya hizo, iliyofanyika Julai 04, 2019.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi(kushoto) akimuongoza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na wajumbe wengine wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Itilima, Julai 04, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(mwenye koti jeusi) na viongozi wengine wakitoa katika moja ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Bariadi wakati wa ziara maalum ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo iliyofanyika Julai 04, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(mwenye shati la kitenge mbele) na viongozi wengine wakitoa katika moja ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Busega wakati wa ziara maalum ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo iliyofanyika julai 04, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(mwenye shati la kitenge mbele) na viongozi wengine wakitoa katika moja ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Busega wakati wa ziara maalum ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo iliyofanyika Julai 04, 2019.
Baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakikagua Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bariadi Julai 3, 2019.
Baadhi ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Busega yakiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi
Baadhi ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Bariadi yakiwa
katika hatua mbalimbali za ujenzi
No comments:
Post a Comment