MILIONI 42 BAKWATA KUJENGA MSIKITI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 11 July 2019

MILIONI 42 BAKWATA KUJENGA MSIKITI

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
BARAZA Kuu la Waislamu (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza limezindua ujenzi wa msikiti wa baraza hilo utakaogharimu sh. milioni 42 kwa kuweka jiwe la msingi.

Akizungumza kabla ya kuweka jiwe hilo jana Sharif Said Jafari Swadiqu Bin Sayeid Muhammad kutoka Malindi nchini Kenya, alisema uongozi wa BAKWATA Mwanza umefikiria jambo jema kujenga msikiti kwenye soko ili kuwafanya waumini wa dini ya kiislamu wanaofanya biashara katika eneo hilo wasimsahau Mungu.

Alisema chini ya uongozi wa Sheikh Mkuu Mufti wa Tanzania, Abubakar Zuberi uislamu umeanza kuwa na mabadiliko makubwa kwa muda mfupi kutokana na kauli mbiu ya Jitambue, Badilika, Acha mazoea.

“Heshima ya uislamu ni msikiti ( kuwa na nyumba ya ibada) na uislamu unazingatia kuwa na msikiti na ni fikra njema msikiti kujengwa sokoni. Pia jamii ya kiislamu kupitia mambo matatu ya Mufti Abubakar Zuberi, yanamfanya mtu ajitambue, abadilike na kuacha mazoea mambo ambayo yameufanya uislamu Tanzania kubadilika,”alisema Sharif Said Jafari Bin Sayeid.

Mjukuu huyo wa kizazi cha 42 cha Mtume Muhhamad S.A.W. alidai msikiti huo utakaoitwa Masjid Abubakar Zuberi una umuhimu mkubwa kwenye uislamu kwa sababu wapo baadhi wanajenga mioyo ya watu na si misikiti pekee.

Sharif Said Jafari bin Sayeid akizungumzia akina mama kiislamu alisema ni wanaharakati wakubwa wa kuendeleza uislamu hivyo wajitambue, wainuke kwa sababu wanayo nafasi na fursa kubwa wenye jamii.

Awali Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza alhaji Sheikh Hassan Kabeke alisema dhamira yao ilikuwa kujenga jengo la msikiti wa ghorofa tatu kwa sababu BAKWATA kati ya misikiti 324 haina hata mmoja ambo ni maalumu na unmilikiwa na mkoa.

“Tulikuwa na dhamira ya kujenga msikiti wa ghorofa tatu lakini baada ya serikali kuamua kutumia eneo la BAKWATA kwa ajili ya soko kwa miaka miwili tumebadili nia hiyo na kujenga msikiti wa muda utakaotumika kwa kipindi hicho wakati tukijipanga kujenga wa kudumu utakaokuwa na hadhi ya Mufti Zuberi,”alisema.

Alieleza kwa kuwa heshima ya uislamu ni msikiti hivyo wenye dhamira ya kuendeleza uislamu waunge mkono mradi huo wa ujenzi msikiti kwa fedha, vifaa vya ujenzi (mawe, kokoto, mchanga, nondo, saruji na misumari).

“Gharama za ujenzi wa msikiti huu wa muda ni sh. milioni 42, waumini watautumia kwa ibada wakati tukijipanga kujenga ule wa kudumu.Utatumika kwa miaka miwili kisha utajengwa mkubwa kwa hadhi ya Mufti,”alisema Sheikh Kabeke.

Aidha, Sheikh Kabeke alisema Mkoa wa Mwanza umepata heshima ya kuandaa Maulid ya Kitaifa mwakani na yatadhimishwa kwa kufanya mashindano ya kuhifadhi Quran, adhana, mpira kwa wanafunzi wa madrasa, mapishi ya akina mama,makongamano ya kiuchumi na maadili.
 Sharif Said Jafari Swadiqu Bin Sayeid Muhammad (wa tatu kutoka kulia) akiomba dua kabla ya kuweka jiwe la Msingi kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti wa BAKWATA Mkoa wa Mwanza jana.
 Sharif Said Jafari Swadiqu Bin Sayeid Muhammad (wa tatu kutoka kushoto) akifungua pazia kuashiria kuweka jiwe la Msingi la UJENZI wa Msikiti wa BAKWATA Mkoani Mwanza jana.
 Baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu wakimsikiliza Sharif Said Jafari Swadiqu Bin Sayeid Muhammad (aliyesimama) wakati akizungumza kabla ya kuweka jiwe la Msingi la UJENZI wa msikiti wa BAKWATA mkoa wa Mwanza utakaoitwa Masjid Abubakar Zuberi.Walioaa wa tatu kutoka kushoto ni Sheikh Hassani Kabeke, sheikh wa Mkoa wa Mwanza.
 Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Sheikh Hassani Kabeke akizungumza na waandishi wa habari mar baada ya kuzinduliwa kwa UJENZI wa msikiti wa BAKWATA mkoani humu jana. Picha zote na Baltazar Mashaka

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad