HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, June 17, 2019

WANAFUNZI WA KIKE WANATAKIWA KUZINGATIA MASOMO

NA DENIS MLOWE, IRINGA

WANAFUNZI wa vyuo vikuu mkoani Iringa wametakiwa kuzingatia zaidi masomo kuliko kujihusisha na maisha ya starehe ambayo yamekuwa yakiwagharimu wengi wao kutotimiza ndoto walizojiwekea pindi wafikapo vyuoni.

Akizungumza katika kongamano kubwa la wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu vilivyoko mkoani hapa makada wa Chama cha Mapinduzi, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Jeska Mbogo amewataka wanafunzi hao kuzingatia zaidi masomo kuliko kupoteza muda kwenda katika kumbi za disco na kuwa na mahusiano na wanaume na kusisitiza kuelekeza akili katika masomo kwa mambo ya kidunia watayakuta .

Mbogo alisema kuwa imekuwa kasumba ya wanafunzi wengi wa kike kuanzisha mahusiano ambayo hayana faida yoyote katika maisha yao ambapo baadhi yao wanashindwa kutimiza ndoto zao kutokana na kujiingiza katika mapenzi katika umri mdogo ama kwa kudanganywa na makundi rika au kudanganywa kwamba wakijihusha na mapenzi na walimu watafanya vyema katika mitihani yao.

Alisema kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakijiingiza kwenye mambo ya anasa na starehe badala ya masomo huku wakisahau kuwa wazazi wao wanatumia nguvu nyingi katika kuwasomesha kwa gharama kubwa katika kulipia ada ya masomo na kuja kushawishika na wanaume wasiokuwa na malengo nao.

Aliongeza kuwa katika maisha ya kila siku endapo unataka kufanikiwa mwanamke unatakiwa kujitambua nini lengo la kufika chuoni, kujithamini utu wako, kujielewa na kujiamini kutakuletea mafanikio ambayo unayataka katika kutimiza ndoto za maisha yako hapo mbeleni.

Mbogo aliwataka wanafunzi hao kujikubali jinsi walivyo kwani ndivyo Mungu ndivyo alivyowaumba na kuachana na tabia ya kujibadilisha maumbile kwa kutumia dawa za kachina ili kubadili muonekano wa maumbo yao ili kuonekana wazuri wakati ni bora kujikubali ulivyo kuliko kutaka kuisha maisha ya kuwaonyesha watu bila kutambua madhara ya mbele yatakuwaje.

Katika kongamano hilo, Mbogo alikabidhi kadi zaidi ya 100 kwa wanafunzi hao kujiunga na Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) wa CCM mkoa wa Iringa ambapo wanafunzi hao waliomba kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali katika vyuo wanavyotoka kuweza kujikomboa kiuchumi na kuwaahidi kuwapatia mafunzo hayo.

Alitoa wito kwa wazazi kutenga muda wa kuwa karibu na Watoto wao na kuzungumza nao kwani wazazi wengi wamekuwa wako bize kutafuta hela na kusahau kukaa na kuzungumza na Watoto wao jambo ambalo linazidi kuendeleza mmomonyoko wa maadili kwa Watoto wao.

Naye Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Iringa, Rose Tweve aliwataka wanafunzi wa kike kujiamini katika Maisha yao kwani hakuna kitu kinachoweza kumkomboa mwanadamu kama kujiamini kwani watu wote waliofanikiwa duniani walijiamini na kuthubutu na ndio maana wamefanikiwa.

Rose aliwataka vijana hao kutokuwa watu wakulaumu au kulalamika bali wawe ni watu wa kufanya kazi kwa vitendo kulisaidia Taifa lao kwani ni fahari sana kusema wewe nimelifanyia nini Taifa lako kuliko kusema kusema Taifa lako limekufanyia nini .
 Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Jeska Mbogo akisalimiana na mmoja ya wanawake wa UWT mkoa wa iringa wakati alipofanya ziara ya kikazi mkoani Iringa.
 Katibu wa Umoja wa Wanawake Mkoa wa Iringa, Chiku Masanja akiwatambulisha baadhi ya wajumbe wa kamati ya uwt mkoa wa Iringa kwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Jeska Mbogo .
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Jeska Mbogo akizungumza na wajumbe na viongozi wa UWT mkoa wa Iringa.
 Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Jeska Mbogo , akikabidhi kadi kwa mmoja wa wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu mkoani Iringa kujiunga na UWT.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad