HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 6, 2019

WANAFUNZI WA JESHI LA UWOKOVU WAFURAHIA ‘OUTING’ YA TVP BAGAMOYO


Wanafunzi wa darasa la saba wa shule ya msingi ya Jeshi la Uwokovu wamefurahia safari yao ya kwenda kutembelea sehemu za mji wa kihistoria wa Kaole uliopo mjini Bagamoyo, mkoa wa Pwani, ikiwa sehemu yao ya kujifunza kwa vitendo walichokisoma darasani kwa kipindi cha miaka 7 kabla ya kumaliza elimu yao ya shule ya msingi miezi michache ijayo.

Wakiambatana na wafanyakazi wa True Vision Production (TVP) waliofadhili safari hiyo ya sehemu ya kujifunza kwa vitendo (study tour), wanafunzi hao wamesema wamepata faraja sana kupata ufadhili wa safari hiyo.

Kilichowafurahisha  zaidi ni wafanyakazi wa TVP kujumuika nao, kuwahudumia wale wenye ulemavu wa viungo na kula nao pamoja chakula cha mchana.
Wakiongea kwa niaba ya wanafunzi wenzao, Noah Michael (15) amesema wamejifunza biashara ya utumwa ilivyoanza Pwani ya Afrika ya Mashariki, kikubwa zaidi akiwaomba TVP kuendelea kujitolea kwa wanafunzi wenye uhitaji.

“Tumejifunza mambo mengi, tumefurahia pia chakula kitamu, kikubwa zaidi TVP tumekuwa nao katika matembezi yetu, wametuletea chakula mezani na kuwa sehemu ya walezi wetu,” amesema Michael.
Naye Joyce Mahona (14) , mwenye ndoto ya kuwa daktari, amesema amejifunza jinsi watumwa walivyokuwa wanauzwa, ameona msikiti wa kwanza kabisa kujengwa katika karne ya 13, kisima cha kale na kuona makaburi wa watu wa kale.

Alanus Lugome amesema mbali ya kuona vitu vingi vya kale, kikubwa zaidi kilichomshangaza ni kuuona mti wa ubuyu wenye miaka zaidi ya 500.
Katika kudhihirisha ule usemi usemao ‘Disability is not Inability (ulemavu sio sababu ya kushindwa au kutojua kitu), wanafunzi hao walimshangaza mtembeza watu maeneo ya kale (Tour Guider), Leo Tagalile kwa maswali mazuri waliyouliza wanafunzi juu ya mji huo wa kihistoria.

Miongoni mwa maswali waliyoyauliza ni pamoja na kutaka kujua akina nani waliokuwa wenyeji wa eneo hilo kabla ya ujio wa wakoloni, kwa nini paliitwa Kaole na je mbuyu huo bado unatoa matunda licha ya kuwa na umri wa miaka 500?.

Pia wanafunzi hao, mbali na kuiona bandari ya kwanza katika Pwani ya Afrika ya Mashariki, pia walitembelea jengo la The Caravan Serai, lililojengwa mwaka 1870 kwa ajili ya kupokea watumwa waliotoka sehemu mbalimbali kama vile Kilwa Masoko kabla ya kuuzwa.
“Mmefanya kitengo kikubwa sana kwa sababu wanafunzi wenye ulemavu wa viungo, huwa hawaamini kama jamii nyingine inawakubali na kuwathamini,”
“Siku zote wanajisikia faraja sana watu wengine wanapojumuika nao sababu wengine hata jamii zao zinawatenga,”

“Wao wamezoea kuwa karibu na jamaa zao na walimu wao tu, wakitokea watu wengine tofauti kama TVP na kuwa nao siku nzima, wao wanafarijika sana,” amesema Anne Kibanga Mwamgunda, mwalimu wa taaluma wa shule hiyo, inayojumuisha “TT
“Mbali ya kuwasaidia katika mitihani, pia itawapa kumbukumbu muhimu katika maisha yao,” amesema mwalimu Emmanuel Ibrahim.

Amesema mara ya mwisho wanafunzi wake kutembelea Kaole ni miaka miwili iliyopita kwa ufadhili wa aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP, marehemu Reginald Mengi.
Mmoja wa wafanyakazi wa TVP, David Sevuri amesema wamejisikia faraja kuwasaidia wanafunzi hao kwenda katika mji huo wa Pwani ya Bagamoyo kama sehemu ya kujifunza kwa macho, baada ya nadharia ya darasani.

“Tuliwahi kuwatumia wanafunzi watatu kutoka shuleni kwenu kutengeneza tangazo la televisheni la Haki Elimu, hivyo tukaona sababu nyingine ya kuwa karibu na nyinyi,”amesema Sevuri.
TVP, inayojihusisha na utengenezaji wa Makala maalumu za video (documentary) na matangazo ya radio, ilitoa pia magunia ya unga, mchele na mafuta kama sehemu ya msaada wa chakula kwa watoto hao.
 Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya True Vision Production wakiwasaidi watoto wenye ulemavu wakati wa ziara yao
 David Sevuri akiwakabidhi wanafunzi wa shule ya msingi Jeshi la Uwokovu sehemu ya vyakula wakati wa ziara yao ya Kaole
 Mbali na kuona sehemu za kale, vyakula pia vilikuwa sehemu ya ziara hiyo
 Mmoja wa wanafunzi akichukua kumbukumbuku muhimu kama anavyoonekana
Ulikuwa ni wajibu wa TVP crew kuwahudumia kama Isaac Lukando anavyoonekana pichani

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad