HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 27, 2019

SERIKALI YAWAASA WANANCHI KUTOTUMIA DAWA ZA KULEVYA ILI KULINDA NGUVUKAZI YA TAIFA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewaasa wananchi wake kutojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya ili kulinda nguvukazi ya Taifa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya kupiga vita Dawa za Kulevya duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Tangamano, jijini Tanga.

Mhe. Mkuchika amesema matumizi ya dawa za kulevya yanaleta athari kwa jamii nzima, kwani hushusha kiwango cha uzalishaji na hatimaye kukwamisha maendeleo ya Taifa.
 “Matumizi ya dawa za kulevya yanaathiri kwa kiasi kikubwa nguvukazi ya Taifa letu, ambayo ndio tegemeo katika uzalishaji na ukuzaji wa uchumi wa Taifa letu” Mhe. Mkuchika amesisitiza.

Mhe. Mkuchika amezitaja dawa za kulevya zinazotumika kwa wingi kuwa ni bangi, mirungi, heroin, cocaine na baadhi ya dawa za hospitali zenye asili ya kulevya kama vallium, ketamine, pethidine, indocile, morphine na tramadol.
Mhe. Mkuchika amewataka wananchi kuepuka matumizi ya dawa za kulevya ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kuijenga nchi kuwa ya viwanda na kufikia lengo la uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Jitihada za Serikali kuwa nchi ya viwanda zinahitaji fedha katika utekelezaji wake, hivyo badala ya kutumia fedha nyingi kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya, tutumie fedha hizi kujenga miundombinu itakayotukuzia uchumi na kutuletea maendeleo katika Taifa letu” Mhe. Mkuchika amesema.
Aidha, Mhe. Mkuchika ametoa rai kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kutoa taarifa za uwepo wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya katika maeneo wanayoishi ikiwa ni pamoja na kuwaomba viongozi wa dini kuungana na serikali kukemea matumizi ya dawa za kulevya kwani wanayo nafasi kubwa katika jamii kuwajenga vijana kiroho, kimwili na kisaikolojia ili wawe na tabia njema.

Naye, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) amesema tatizo la dawa za kulevya ni janga kubwa duniani kote na kwa bahati mbaya watumiaji wa dawa hizo kwa asilimia kubwa ni vijana ambao ndio tegemeo la uzalishaji na viongozi watarajiwa.

Maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya hufanyika kila mwaka Juni, 26 kwa lengo la kutoa fursa kwa umma kupata elimu kuhusu athari za matumizi na biashara ya dawa za kulevya kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu.
  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akizungumza na wananchi wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Tangamano, jijini Tanga.
 Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) (hayupo pichani) wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Tangamano, jijini Tanga.
 Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) akizungumza na wananchi wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Tangamano, jijini Tanga.
 Mmojawapo wa waathirika wa dawa za kulevya, Bw. Said Bandawa akitoa ushuhuda wa namna Serikali ilivyomsaidia kuondokana na matumizi ya dawa za kulevya wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya kupiga vita Dawa za Kulevya duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Tangamano, jijini Tanga.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akiteta jambo na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya kupiga vita Dawa za Kulevya duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Tangamano, jijini Tanga.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad