JUMLA ya shilingi Milioni 400 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa kituo
cha Afya Mapera kata ya Mapera Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ambrose Mtarazaki amesema hayo jana
wakati akifungua kikao cha Baraza la robo ya tatu cha Baraza la
madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Umati
Mjini Mbinga.
Alisema, ujenzi wa kituo hicho utakapokamilika utasaidia sana
kuwaondolea wananchi wa kata ya Mapera na Bonde zima la Hagati
kusafiri umbali mrefu hadi Hospitali ya wilaya iliyopo Mbinga Mjini au
Hospitali ya Misheni Litembo kufuata matibabu.
Mtarazaki ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kutoa fedha hizo
ambazo zitakwenda kukamilisha kazi hiyo na kuimarisha huduma za Afya
kwa wananchi hasa ikizingatia kuwa, lengo la kujenga kituo cha Afya
Mapera ni la muda mrefu hata hivyo walishindwa kutokana na ukosefu wa
fedha.
Amewaomba wananchi wa Mapera na kata jirani kuhakikisha wanashiriki
vema katika ujenzi wa miundombinu kwa kupeleka mchanga ,tofali na
mahitaji mengine ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati badala ya
kuiachia Serikali jambo linalo weza kuchelewesha kazi hiyo.
Aidha Mtarazaki, ametaka fedha hizo zitumike kwa malengo
yaliyokusudiwa na kuwaonya watendaji wa Serikali kanzia ngazi ya
kijiji hadi wilaya kutothubutu kwa namna yoyote kujaribu kutumia
fedha hizo kinyume na malengo.
Katika hatua nyingine Mtarazaki alisema, katika kipindi cha robo ya
tatu ya Mwaka wa Fedha 2019/2020 Halmashauri ya wilaya imeweza
kutekeleza na kufuatilia miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo
mbalimbali hatua iliyochochea sana upatikanaji wa huduma bora za
kijamii kwa Wananchi.
lisema, katika kipindi hicho Halmashauri ya wilaya imetoa shilingi
Milioni 261 kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa na Upimaji na usimamizi wa
matumizi Bora ya Ardhi katika vijiji mbalimbali.
Mtarazaki alisema, pia Halmashauri ya wilaya imetoa jumla ya shilingi
milioni 198 kama mkopo kwa makundi maalum ya wanawake,vijana na watu
wenye ulemavu pamoja na shilingi milioni285 zilizotengwa kwa ajli ya
ununuzi wa magari mawili ili kurahisisha utendaji wa watumishi na
utoaji huduma Bora kwa wananchi.
Alisema, sambamba na hilo Halmashauri imefanikiwa kupata hati safi
kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG),na
amewataka watumishi wa Halmashauri ya kuendelea kufanya kazi kwa
weledi na madiwani kuhakikisha wanasimamia kikamilifu vyanzo
vyote vya mapato ili fedha zinazokusanywa ziende kufanya kazi ya
kumaliza changamoto na upatikanaji wa huduma za kijamii.
Pi aliwaeleza madiwani kuwa,hadi kufikia mwezi April mwaka huu
Halmashauri imeshakusanya asilimia 85 ya mapato yake ya ndani.
Hata hivyo alisema, licha ya mafanikio hayo bado kuna tatizo kubwa
kwa baadhi ya watendaji wachache kushindwa kutumia mashine za POS kwa
ajili ya kukusanya mapato ya Halmashauri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Juma
Mnwele akifafanua jambo kwa wajumbe wa Baraza la madiwani wa
halmashauri hiyo kilichofanyika jana katika Ukumbi wa Umati
Mbinga,katikati Mwenyekiti wa halmashauri Ambrose Mtarazaki.
No comments:
Post a Comment