HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 28, 2019

NAIBU WAZIRI KANYASU AAGIZA TAWA IUNDE TUME KUCHUNGUZA KIFUTA MACHOZI WILAYANI BUNDA



Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sarakwa wilayani Bunda mkoani Mara kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa mapema kwenye ofisi za kijiji wakati wanyamapori wakali na waharibifu wanapoharibu mazao. 
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Sarakwa wakimsikiliza Naibu Waziri waMaliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu wakati wa mkutanao wa hadhara uliofanyika katika eneo la Shule ya ,msingi ya Sarakwa mara baada ya kusikiliza malalamiko yao kuhusu malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi. 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akisalimiana na baadhi ya watumishi wa wilaya ya Bunda mkoani Mara mara baada ya kuwasili katika ofisi ya Mkuu wa wilaya kwa ajili ya kikazi ya siku moja. 
Mbunge wa jimbo la Bunda vijijini, Boniface Getere akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sarakwa kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu kuzungumzia kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa mapema kwenye ofisi za kijiji wakati wanyamapori wakali na waharibifu wanapoharibu mazao yao. 
Mwenyekiti wa kijiji cha Sarakwa, Samson Kapeta akizungumza na wananchi wake kabla ya kumkaribisha na Mbunge wa jimbo la Bunda vijijini, Boniface Getere kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho. 

…………………… 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) iunde timu ya kuchunguza uhalali wa malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi kilichotolewa kwa wananchi walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu wa mazao katika maeneo mbalimbali nchini. 

Mhe. Kanyasu ametoa agizo hilo mara baada ya kupokea malalamiko na madai kutoka kwa baadhi ya wananchi wa vijiji 4 vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, wilayani Bunda mkoani Mara ambao mazao yao yaliliwa na kuharibiwa na wanyamapori wakali wamekuwa hawalipwi huku wasiostahili ndo wamekuwa wanalipwa . 

Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Sarakwa, Mariwanda ,Unyali na Kihomboi vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Bunda mkoani Mara, Mhe. Kanyasu amesema kuwa mara baada ya uchunguzi kukamilika wale watakaobainika kupokea fidia hiyo wale wasiostahili watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kuzirudisha fedha hizo.

‘’Nataka niwambie, wale waliopokea kifuta jasho na kifuta machozi kutoka serikalini wakati hawastahili lazima hizo fedha wazitapike” Amesisitiza Mhe. Kanyasu 

Aidha, Mhe. Kanyasu amesema licha ya fidia hiyo kuendelea kulalamikiwa kuwa kidogo ikilinganishwa na hali halisi ya maisha ya sasa, wananchi ambao mazao yao yameharibiwa wanatakiwa kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria iliyopo na sio vinginevyo. 

Katika hatua nyingine Mhe. Kanyasu amewataka wananchi wanaoharibiwa mazao yao na wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo tembo watoe taarifa ndani ya muda wa siku tatu katika ofisi za vijiji katika maeneo yao ili hatua za malipo ziweze kufanyika kwa muda. 


Pia, Kanyasu amewaeleza wananchi hao kuwa Serikali imeanza kupitia upya utaratibu wa kifuta jasho na kifuta machozi ili kiweze kuendana na gharama za maisha ya sasa. 

Kwa upande wake Bw. Abel Hadawi, mmoja wa wananchi ambaye mazao yake zaidi ya ekari 20 yaliharibiwa mwaka jana, amemweleza Naibu Waziri huyo kuwa amaekuwa akijaza fomu kwa ajili ya kulipwa fidia lakini kila malipo yanapokuja jina lake limekuwa halimo. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) kanda ya Ziwa, Emmanuel Nkya amewaeleza wananchi hao kuwa wanachotakiwa kufanya ni kujaza fomu nne ili kuwe na nakala kuanzia ofisi ya kijiji hadi makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii. 

Naye Mbunge wa Bunda vijijini, Boniface Getere amemwomba Naibu Waziri Kanyasu kuyashughulikia malalamiko ya wananchi wote wanaostahili kulipwa kifuta jasho na kifuta machozi kwa kuwa wengi wao wameathiriwa na kubaki omba omba kufuatia mazao yao kuharibiwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad