HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 16, 2019

JWTZ WATUMIA NDEGE YA ATCL KUSAFIRISHA WAPIGANAJI KUISHIRIKI ULINZI WA AMANI DARFUR

Na Luteni Selemani Semunyu
Maafisa na Askari wa jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanaoshiriki Ulinzi wa Amani katika  Jimbo la Darfur nchini Sudan kwa Mara ya kwanza  kwa kipindi cha Miaka 10 ya Ulinzi wa Amani Jimboni humo wametumia Ndege ya Shirika la Ndege ya  Serikali ya ATCL ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Mhe Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu katika  kulifanya Shirika hilo linapiga hatua zaidi kwa maslahi ya Shirika na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita wa JWTZ Meja Jenerali Alfred Kapinga amesema Jeshi ni Taasisi inayoongozwa na Uzalendo,uadilifu, uhodari  hivyo ni faraja kubwa kwa Jeshi  na wapiganaji kuunga mkono jitihada za Serikali katika Kuboresha Uchumi  ikiwa ni  sehemu ya mchango wao katika kuonesha  uzalendo kwa vitendo kwa  kutumia vitu vya nyumbani kwa maslahi mapana ya Taifa.

“ Tumekuwa tukitumia Ndege zetu za Jeshi lakini tumekuwa tukitumia Ndege za mataifa mengine kwa Mikataba kutoka Umoja wa Mataifa lakini sasa ni faraja kwani tumefanikiwa kuwashawishi Umoja wa Mataifa kutumia Ndege zetu” Alisema Meja Jenerali Kapinga.

Aidha,Meja Jenerali kapinga alisema   mbali na kutumia Ndege hiyo lakini aliwaasa Maafisa na Askari hao kuhakikisha wanapeperusha vema Bendera ya Nchi na kuendelea kuitangaza kwa  sifa nzuri za Utendaji Kimataifa.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Ndege la la Tanzania (ATCL),  Mhandisi Ladislaus Matindi  Alisema ni Fursa Nzuri kwa ATCL na wanalishukuru Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kupitia kwa mkuu wa majeshi ya Ulinzi  kwa Mchango mkubwa   kufanikisha kupata tenda hiyo.

“ Namshukuru Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi  Jenerali Venance Mabeyo na watendaji wake kwa Uzalendo wake na kuhakikisha anafanikisha ATCL kupata fursa kwa mara ya kwanza na hii itakuwa mwanzo mzuri na tutahakikisha tunaitumia vizuri  fursa hii kujitangaza zaidi Kimataifa kwa maslahi  ya Nchi “ Alisema Mhandisi Matindi.

Vilevile  Mhandisi Matindi aliongeza kuwa Ndege ya Dream Liner ina uwezo wa kusafiri kwa saa 12 bila kusimama, hivyo kwa  kutumia saa tatu kusafiri kutoka hapa mpaka nchini Sudan  ni sehemu ndogo ya Uwezo wake na ni nafasi ya kuwajaribisha watendaji wa Ndege wa ATCL katika kuhudumia safari Ndefu.

Naye Kamanda wa Kikosi cha TANZBATT- 13,  Luteni Kanali Khalfan Kayage  anayekwenda na  Kikosi hicho  alisema kuwa  inawapa nguvu kupeperusha Bendera yetu kupitia Ndege na ameahidi kufanya kazi kwa Bidii kuendeleza jina na sifa nzuri ya Tanzania Kimataifa.
 Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita wa JWTZ Meja Jenerali Alfred Kapinga  ( Kushoto ) akiagana na Kamanda Kikosi  Kundi la 13  Luteni kanali Khalfan Kayage (Kulia ) kinachoenda kushiriki Ulinzi wa Amani Jimboni Darfur Nchini Sudan leo mei 16 wakati wakiondoka kwa Ndege ya ATCL (Haipo pichani )  katika Uwanja wa Ndege wa Jeshi Jijini Dar es Salaam katikati ni Mkurugenzi wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi. Picha na Luteni Selemani Semunyu
 Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita wa JWTZ Meja Jenerali Alfred Kapinga Akiagana na  Maafisa na Askari wa  JWTZ   Kundi la 13 linalokwenda kushiriki Ulinzi wa Amani Jimboni Darfur Nchini Sudan wakati wakiondoka kwa Ndege ya ATCL (haipo Pichani) leo Mei 16  katika Uwanja wa Ndege wa Jeshi Jijini Dar es Salaam Picha na Luteni Selemani Semunyu
Baadhi ya Maafisa na Askari wa JWTZ  Kundi la 13 wakijiandaa  kuondoka kwa Ndege ya ATCL leo Mei 16 2019 katika Uwanja wa Ndege wa Jeshi Jijini Dar es Salaam kwenda kushiriki Ulinzi wa Amani Jimboni Darfur Nchini Sudan  . Picha  na Luteni Selemani Semunyu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad