HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 2, 2019

Dkt Gwajima ataka Timu za Uendeshaji Huduma za Afya za Mikoa kutumia muda wao vizuri kufuatilia na kusimamia huduma za afya

Na Mathew Kwembe, Njombe
Serikali imezitaka timu za uendeshaji huduma za afya za mikoa kuelekeza nguvu zaidi na muda zaidi katika kusimamia  shughuli zote za utoaji wa huduma bora za afya katika mikoa yao badala ya kutumia nguvu na muda mwingi kukaa ofisini au kuwa safarini.

Agizo hilo limetolewa leo mjini Njombe na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya, Dkt Dorothy Gwajima wakati akizungumza na timu ya uendeshaji huduma za afya ya mkoa wa Njombe.

Amesema jukumu kubwa la timu za usimamizi huduma za afya mikoa ni kuhakikisha kuwa timu za usimamizi huduma za afya halmashauri zinaimarisha usimamizi wa timu za uendeshaji huduma za vituo husika ili, zihakikishe huduma zinatolewa kwa ubora stahiki.

Aidha, kupitia ufuatiliaji wa kina, timu za usimamizi wa afya mkoa na halmashauri  zinapaswa kupata mwenendo wa huduma kutoka vituo vyote na maeneo yote ya huduma za afya jamii kisha,  kufanya uchambuzi wa takwimu na taarifa hizo na kuzijadili ili, kutoa ushauri, mapendekezo, maelekezo ya kuwesha kuwa na mipango stahiki inayojibu hoja husika kwa wakati.

Dkt. Gwajima amezikumbusha timu zote za usimamizi huduma za afya za mikoa na halmashauri kuwa, huduma za afya zinazotolewa katika vituo na katika ngazi ya jamii zina uhusiano wa moja kwa moja na umakini wa utendaji wa timu za afya za mikoa na halmashauri hivyo, watambue kuwa, wanalo jukumu kubwa la kuelekeza nguvu na muda wa kutosha katika kufuatilia utoaji wa huduma husika badala ya kutumia muda mwingi kukaa ofisini na kusafiri hata safari ambazo wanaweza kuwakilishwa.

Hivyo, amesema kipimo cha ubora, umahiri na tija ya utendaji wa timu za afya mkoa na timu za afya za halmashauri ni ubora wa huduma zinazotolewa ngazi ya vituo vya afya na siyo vinginevyo.

Dkt Gwajima amesema, takwimu zinaonesha baadhi ya timu za usimamizi huduma za afya mikoa na halmashauri hazitumii muda wa kutosha kufanya ufuatiliaji wa kina wa utoaji huduma za afya katika vituo na jamii na badala yake muda mwingi unatumika kukaa ofisini, safarini au kuendekeza malumbano yatokanayo na kukataa kupokea mabadiliko katika uwajibikaji (resistance to change) kitu ambacho, amesema hakikubaliki kwani kinapoteza muda.

 Amesisitiza kuwa, lazima muda mwingi utumike kwa timu hizi kuwa karibu zaidi na ufuatiliaji wa mwenendo wa utoaji huduma za afya kwa wateja ili, kubaini changamoto zinazojitokeza, kuziwasilisha, kuzichambua na kuzijadili kama timu kisha, kuzitumia kutoa ushauri, maelekezo, mapendekezo na kupanga mipango inayogusa huduma kwa uhalisia wa takwimu.

Dkt. Gwajima amesema, kila mjumbe wa timu ya usimamizi wa huduma za afya anatakiwa kuwa na taarifa fupi ya utekelezaji wa ufuatiliaji wa mwenendo wa huduma siyo tu kila mwezi na kila robo bali kila siku kwani, vipo viashiria muhimu vya kufutilia na kuvifanyia uchambuzi kila siku na kinyume na hapo, haikubaliki maana hakutakuwa na maelezo ya nini hasa kimefanyika siku husika.

Kuhusu eneo la upatikanaji wa huduma Dkt. Gwajima amesema, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli imeendelea kuinua ubora wa huduma za afya kwa kujikita katika kuboresha maeneo mengi na baadhi yake ni ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya na kuongeza bajeti ya dawa.

Hivyo, jukumu la timu za usimamizi huduma za afya ni kufanya ufuatiliaji na usimamizi wa kina ili, juhudi hizi zizidi kuzaa matunda makubwa zaidi na kuondoa kero zinazoepukika hususan, matukio ya kukosekana kwa dawa yatokanayo na kutozingatia taratibu za manunuzi ya umma na tabia za baadhi ya watoa huduma kutumia dawa hizo bila kuzingatia Mwongozo wa Matibabu.

Amesema, tabia zinazokwamisha juhudi za Serikali zinachangiwa na baadhi ya timu za usimamizi huduma za afya mikoa na halmashauri kutoweka nguvu na muda wa kutosha katika kufuatilia mwenendo wa utoaji huduma katika vituo husika.

Dkt Gwajima amesema, timu za usimamizi huduma za afya zina jukumu la msingi la kuhakikisha huduma za tiba zinakuwa bora katika vituo na kuvutia watumiaji wengi wenye uhitaji.

Aidha, kwa kuwa miongoni mwa watumiaji ni wanachama wa mifuko mbalimbali ya bima za afya ni dhahiri kuwa, watachangia huduma na hivyo, kuwezesha vituo vya huduma kupunguza utegemezi kwa Serikali na hii ndiyo itaongeza tija zaidi.

Amesema, kupunguza utegemezi wa vituo kwa serikali inawezekana kwa kuwa, bado fedha nyingi za marejesho ya mfuko wa taifa wa bima ya afya zinaenda kwa watoa huduma wanaomiliki vituo binafsi ambao ni wachache ukilinganisha na idadi ya vituo vya Serikali hivyo, kuna haja ya kuzingatia hili.

Dkt. Gwajima amesema, uzembe katika kujaza kumbukumbu za huduma iliyotolewa ikiwemo, kumbukumbu za madai ya fedha unachangia kuwepo kwa makato yanayoepukika.

Aidha, baadhi ya watoa huduma kutojali uwepo wa dawa na vipimo kunachangia wateja wengi kwenda kununua dawa nje ya kituo ikiwemo, baadhi ya watoa huduma  kuanza biashara bubu za kuuza dawa kwa wateja hivyo, tabia hizi zidhibitiwe mara moja na timu za usimamizi huduma za afya mikoa na halmashauri.

Dkt. Gwajima amesema, mapungufu mbalimbali mara nyingi hayaripotiwi na timu za usimamizi huduma za afya na sababu kubwa ni wajumbe wengi wa timu hizi kutotoa muda na nguvu za kutosha kufanya ufuatiliaji wa huduma.

Aidha, amempongeza mfamasia wa kituo cha afya cha njombe mjini bwana Ben Ngogo kwa kuwezesha uwepo wa rekodi nzuri za kumbukumbu za dawa pamoja na kuwa anakabiliwa na ufinyu wa stoo ya dawa. Pia, Dkt. Gwajima amempongeza Muuguzi wa Wodi ya Kujifungua katika kituo hicho bibi Diana Simime kwa umakini wake katika kusimamia usafi pamoja na changamoto ya ufinyu wa chumba na uchakavu wa miundombinu. Amemtaka Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Dkt.Thomas Ndailo kuongeza kasi ya kutimiza malengo ya kujenga kituo cha afya kwenye eneo lenye nafasi.

Dkt. Gwajima amesema, ana imani kuwa, watoa huduma walioko vituoni watafanya vizuri zaidi iwapo, timu za usimamizi huduma za afya mikoa na halmashauri zitaelekeza nguvu na muda wa kutosha katika kufuatilia utekelezaji unaofanyika katika vituo hivi, kuchambua takwimu na taarifa, kujadili, na kushauri na kuelekeza na siyo vinginevyo.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Bumi Mwamasage ameahidi kusimamia kwa nguvu zote yote yaliyo elekezwa na kuhakikisha kuna uwajibikaji mkubwa zaidi wa timu zote za usimamizi huduma za afya katika halmashauri zote.

Dkt. Gwajima anaendelea na ziara ya ufuatiliaji wa ufanisi wa timu za afya mikoa na halmashauri katika mikoa ya Ruvuma na Iringa baada ya kukamilisha kwenye mikoa ya Dodoma, Morogoro na Njombe kauli mbiu ikiwa ni ‘ubora na uhai wa mifumo ya utoaji huduma za tiba na kinga kipimo cha ufanisi wa timu za usimamizi huduma za afya mikoa na halmashauri’.
 Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya, Dkt Dorothy Gwajima  akizungumza na timu ya uendeshaji huduma za afya ya mkoa wa Njombe.

 Baadhi ya wajumbe wa timu ya uendeshaji huduma za afya ya mkoa wa Njombe  wakimsikiliza  Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia sekta ya Afya Dkt Dorothy Gwajima leo mjini Njombe

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad