HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 15, 2019

Bilioni 20 Zakusanywa Ada ya Vitambulisho vya Wajasiriamali

Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
TAKRIBANI Sh bilioni 20.3 zimefikishwa kwenye mfumo wa malipo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kugawa vitambulisho vya wajasiliamali vipatavyo 1,022,178.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo alipokuwa akizungumza na wakuu wa mikoa kabla ya kupitia tathimini ya ugawaji wa vitambulisho hivyo kwa wajasiriamali.

Jafo alisema kuwa kwa wakuu wa mikoa kugawa vitambulisho hiyo 1,022,178, wajasiriamali wameweza kuchangia Sh bilioni 20.44 ambapo Sh bilioni 20.3 ndizo zilizoingizwa kwenye mfumo wa TRA na takribani Sh milioni 135.6 bado ziko mikononi wa wakusanyaji.

“ Mpaka kufikia Aprili 30 mwaka huu kiasi cha Sh milioni 942.47 zilikuwa bado haijaingia kwenye mfumo wa mapato wa TRA, lakini nashukuru ndani ya siku mbili hizi tatu wakuu wa mikoa wameweza kuzifikisha kwenye mfumo fedha nyingi zaidi, niwapongeze kwa hilo.’
Jafo alisema endapo fedha zinazokusanywa kutokana na vitambulisho vya wajasiriamali hazitaingia kwenye mfumo wa mapato wa TRA basi fedha hizo zinakuwa mbichi na kuna hatari ya kuwapo upotevu au kutumika katika matumizi yasiyopangwa.

“ Nitumie fursa hii kuwahimiza wakuu wa mikoa na watendaji ambayo wamekusanya fedha za vitambulisho vya wajasiriamali na kutoziingiza kwenye mfumo wa malipo wa TRA kufanya hivyo mara moja,” alisema
 Aidha, Jafo aliwataka wakuu wa mikoa katika kuhakikisha azima ya Rais John Magufuli ya kutaka wafanyabiashara wadogo watambuliwe na kuwaondolewa usumbufu wanapofanya biashara zao na kushiriki katika uchumi wa nchi kwa kuwaelimisha faida ya kuwa na vitambulisho hiyo.

“ Rais John Magufuli kiu yake ni kuwalinda wafanyabiashara wadogo na kuwaona kuwa na sehemu ya kukuza uchumi wa nchi, alitaka wafanyabiashara wadogo waondokane na adhana zilizokuwa zikiwapata kupitia askari wa majiji ambao walikuwa wakitaifisha bidhaa zao na wakati mwingine kugawana jambo ambalo haikuwa ni haki,”

Kwa awamu ya kwanza na ya pili, vitambulishi vipatavyo 1,850,000 ambavyo vilikuwa na thamani ya Sh bilioni 37 vilitolewa na mpaka Aprili 30 mwaka huu, vitambulisho 1,022,178 vyenye thamani ya Sh bilioni 20.44 vimetolewa kwa wafanyabiashara wadogo.
Aidha, Jafo aliipongeza mikoa ambayo imefanya vizuri katika ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali na ambayo ni Dar es Salaam iliyogawa vitambulisho kwa asilimia 95.2. Tabora kwa asilimia 94.58, Kilimanjaro kwa asilimia 79.05, Pwani kwa asilimia 77.66 na Tanga kwa asilimia 72.

Mikoa ambayo imefanya viabaya na asilimia zake kwenye mabano ni Katavi(asilimia 5.96), Njombe (asilimia 11.14), Rukwa (asilimia 25.03), Iringa(asilimia 30.74) na Lindi (asilimia 33.58).
“ Tunajua changamoto ya baadhi ya mikoa na ndio maana tuko hapa tufanye tathimini ya ugawaji wa vitambulisho hivyo, lengo letu ni kuwa lengo la Rais la kuwalinda wale wasio na sauti lifikiwe kwa wajasiriamali wadogo kutambuliwa,” alisema.

Mkuu wa mkoa wa Tabora, Aggrey Mwandri alisema utaratibu wa kutoa vitambulisho hivyo ulikuwa mgumu hasa kutokana na wananchi kuwa na dhana ya kuwa Serikali inatumia vitambulisho hivyo kuwalipisha kodi.
 “ Ukweli ulikuwa ni kuwa kiasi cha Sh 20,000 ni cha kugharamia uchapishaji wa vitambulisho, lakini wengi waliona kuwa ni njia ya kuwalipisha kodi.

Mwandri aliongeza: “ Tuliweza kufanikiwa kwa kiasi hicho kwa kuwashirikisha viongozi wa kimila, dini na watendaji kuanzia ngazi ya kitongoji, na tukaitisha mikutano ya adhara ya kutoa elimu, na baada ya hapo mwitiko wa wananchi ukawa mkubwa.”
 Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe.Selemani Jafo(Mb) akifungua kikao kazi cha Wakuu wa Mikao na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhusu tathmini ya ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali kilichofanyika St. Gasper Jijini Dodoma.
 Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Kichele akizungumza wakati wa kikao kazi cha Wakuu wa Mikao na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhusu tathmini ya ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali kilichofanyika St. Gasper Jijini Dodoma.
 Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara wakifuatilia kikao kazi kilichoitishwa na OR-TAMISEMI ambacho kimehusisha Mamlaka ya mapato Tanzania kufanya tathmini ya ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wakifuatilia majadiliano wakati wa   kikao kazi cha Wakuu wa Mikao na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhusu tathmini ya ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali kilichofanyika St. Gasper Jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad