HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 17, 2019

BALOZI SEIF AWAASA WANANCHI KUWATUNZA WAZEE WAASISI WA ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wazee Waasisi wa Zanzibar wataendelea kuwa ngao ya Taifa ambayo Viongozi wa sasa pamoja na Wananchi na Kizazi Kipya wana wajibu wa kuwatunza katika maisha yao ya kila siku.

Alisema ngao hiyo inatokana na kazi kubwa waliyoifanya wakati wa harakati za kupigania Ukombozi wa Taifa hili ambapo kwa sasa Viongozi waliopo madarakani pamoja na Wananchi wanaendelea kula matunda ya Uhuru uliotokana na Wazee hao.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed kwenye Futari ya pamoja iliyoandaliwa kwa ajili ya Wazee wanaohifadhiwa katika Nyumba za Serikali zilizopo Welezo Wilaya ya Magharibi “A”.

Alisema Kizazi cha sasa wakati kikiendelea kufaidika na matunda hayo lakini kwa upande mengine wana wajibu wa kulinda na kuendeleza Uhuru huo utakaokuwa kielelezo cha Heshima ya muda wote wa Wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.

Mapema Mchana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi msaada wa Tangi la kuhifadhia Maji, Mashine yake pamoja na Luva ya kusafishia Msikiti wa Ijumaa wa Umbuji uliopo Wilaya ya Kati Mkoa Kusini Unguja.

Msaada huo unafuatia ahadi aliyoitoa wakati wa ufunguzi Rasmi wa Msikiti huo alipomuwakilkisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kwenye Ufunguzi wakeMiaka michache iliyopita nyuma.

Akizungumza na Uongozi wa Msikiti huo Balozi Seif alisema ahadi ni deni kitu ambacho alilazimika kukitekeleza ingawa kimechukuwa muda mrefu kutokana na sababu mbali mbali yakiwemo majukumu yaliyotangulia ya ahadi nyengine za awali.

Akipokea msaada huo kwa Niaba ya Uongozi wa Msikiti huo Sheha wa Shehia ya Umbuji Bwana Muhamad Mrisho Juma alisema Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Kijiji cha Umbuji walilazimika kuwa na subra kutokana na ahadi hiyo kutokana na kazi kubwa inayomkabili Balozi Seif ya kulitumikia Taifa kila siku .

Sheha Mrisho alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba msaada huo muhimu kwao utatumika kwa lengo lililokusudiwa la kuombwa kwake ili uendelee kutoa huduma katika kipindi kirefu kijacho.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Viongozi Watatu wa Kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Afya na Uwekezaji kutoka Nchini Uturuki hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo yao Kiongozi wa Ujumbe huo Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya huduma za Afya na Uwekezaji {KAYI} Bwana Batur Engin alimueleza balozi Seif kwamba Taasisi hiyo yenye Wafanyakazi 600 inatoa huduma katika Mataifa 200 Duniani.

Bwana Batur alisema Wahandisi wa Kampuni hiyo huendeleza kazi za Miundombinu ya Ujenzi wa Hospitali kubwa za kisasa zenye vifaa vya Teknolojia mpya unaofanywa katika mfumo wa ubia.

Alisema zipo Hospitali kubwa zilizojengwa katika Miji ya Paris Nchini Ufaransa, Istambul Uturuki yenyewe pamoja na Hospiatli Kubwa zilizopo Nchini Kenya zinazotarajiwa kukamilika Ujenzi wake hivi karibuni.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Afya na Uwekezaji alieleza pia Kampuni yake huendesha Miradi mengine ya Miundombinu katika Sekta ya Mawasiliano kwa ujenzi wa Viwanja vya Ndege, Bara bara Kubwa za Kisasa pamoja na Mahoteli Makubwa.

Alifahamisha kwamba mtazamo wa Kampuni yake kwa sasa umezingatia kuwekeza katika Visiwa vya Zanzibar Miradi zitakayoweza kutoa huduma katika Mwambao wa Afrika Mashariki pamoja na Ukanda Mzima wa Nchi za Sahara.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari inaendeleza Miradi mikubwa ya Ujenzi wa Hospitali ya Kisasa katika eneo la Binguni pamoja na mpango wa Ujenzi wa Bandari ya Mizigo katika eneo la Mpiga Duri.

Balozi Seif aliueleza Ujumbe wa Viongozi hao kutoka Uturuki kwamba Kampuni yao ina fursa ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uimarishaji wa Ujenzi wa Hospitali hiyo inayotarajiwa pia kuwa na Kitengo cha Mafunzo ya Afya.

“ Inapendeza kuona Ujenzi wa Hospitali Kubwa ya Binguni inafanana na mtazamo wa Kampuni hiyo katika uimarishaji wa Miradi yake katika Huduma za Afya na Uwekezaji Vitega Uchumi”. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali hivi sasa ina mtazamo wa uwepo wa Hospitali ya Kimataifa itakayolenga kutoa huduma kwa Watalii pamoja na wageni wanaoingia Nchini kwa safari za kimatembezi.

Balozi Seif alisema mtazamo huo umekuja kutokana na Zanzibar kwa sasa kuimarika katika Sekta ya Utalii inayoweza kuchukuwa nafasi ya kwanza ya Uchumi wake.

Alisema kuimarika kwa huduma za Afya katika Sekta ya Utalii kutaipa hadhi Zanzibar kurejea katika hadhi yake ya kutoa huduma mbali mbali za kibiashara ndani ya Bahari ya Hindi kama ilivyokuwa ikifanya karne nyingi zilizopita kutokana na mazingira yake ya kuwa kituo cha Biashara enzi hizo.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi msaada wa Tangi la kuhifadhia Maji safi, Mashine ya kusukumuia Maji pamoja na Luva ya kusafishia Msikiti wa Ijumaa wa Kijiji cha Umbuji akitekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa Ufunguzi rasmi wa Msikiti huo Miaka michache iliyopia.
 Sheha wa Shehia ya Umbuji Wilaya ya Kati Bwana Muhamad Mrisho Juma akitoa shukrani kwa niaba ya Ungozi wa Msikiti huo kutokana na msaada huo adhimu.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed akitoa shukrani kwa niaba ya Balozi Seif mara baada ya futari ya pamoja na Wazee wanaohifadhiwa Nyumba za Serikali Welezo.
Balozi Seif akiagana na Wazee wanaohifadhiwa katika Nyumba za Serikali zilizopo Welezo mara baada ya kufutari nao pamoja akiendeleza utaratibu wake aliojipangia ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad