Na Siti Said
Wahandisi
wa kike wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi),
kupitia Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za
barabara, wamewataka wanafunzi wa kike mkoani Dodoma, kuchangamkia fursa
za usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati ili kuongeza wataalam
katika fani ya Uhandisi.
Akizungumza
kwa niaba ya wahandisi hao katika shule ya Sekondari ya KwaMtoro,
Wilayani Chemba mkoani Dodoma, Mhandisi Rahma Mwinyi , amesema kuwa
sekta hiyo bado ina uhaba wa wataalamu wa kike hivyo inahitaji wanafunzi
kusoma masomo hayo ili kuongeza idadi ya wataalamu hao na kuweza
kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025.
“
Hakikisheni mnasoma masomo ya Sayansi na Hisabati kwa bidii, ufaulu wa
masomo haya utategemea ufanyaji wa maswali na mazoezi ya kujipima mara
kwa mara ambayo yatawajengea uelewa na kupelekea kufaulu vizuri,
Serikali bado inahitaji wataalam wa fani hii na pia fursa za ajira
kupitia fani hii zipo nyingi, kazi kwenu kujipanga ili mfikie malengo
yenu”, amesema Mhandisi Mwinyi.
Aidha,
Mhandisi Mwinyi amewataka wanafunzi hao kuachana na dhana potofu ya
kuwa masomo hayo ni magumu na badala yake kutafuta njia mbadala ikiwemo
ya kupanga ratiba ya masomo yao vizuri na kuzingatia yale
wanayofundishwa na walimu darasani.
Kwa
upande wake, Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya KwaMtoro, Bi. Neema Muna,
kwa niaba ya walimu wenzake ameishauri Serikali kuhakikisha wanapeleka
vifaa vya maabara kwa shule ambazo hazina vifaa hususan vijijini kwani
ufaulu wa masomo hayo hutegemea sana kufanya mazoezi kwa vitendo.
Ameongeza
kuwa ipo haja ya Serikali kuajiri na kupeleka walimu wa kutosha katika
shule zilizopo vijijini kulingana na idadi ya wanafunzi na pia huduma za
maji na umeme ziboreshwe ili kukidhi mahitaji ya ufanyaji wa mazoezi
kwa vitendo kupitia katika maabara zao.
Naye,
Mwanafunzi Siminza Mambo wa shule hiyo, ameiomba Serikali kuongeza
walimu wa kike wa sayansi shuleni hapo kwani kwa sasa shule hiyo ina
mwalimu mmoja tu wa jinsia hiyo hali inayowakatisha tamaa wanafunzi wa
kike kujiunga na masomo hayo.
Pia,
Mwanafunzi Lucy Isack, kutoka shule hiyo ameiomba Serikali kuongeza
walimu wa sayansi na hisabati, vitabu na kuboreshea miundombinu ya
maabara ikiwemo vifaa vya kupimia kemikali.
Ziara
ya wahandisi hao katika shule mbalimbali za Sekondari za mkoa wa Dodoma
inalenga kuhamasisha usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa
wasichana ambapo leo wametembelea shule ya KwaMtoro, Dalai na Mondo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari KwaMtoro wilayani Chemba mkoani Dodoma, Bi. Neema Muna (mwenye miwani), akieleza changamoto zinazoikabili shule hiyo kwa Wahandisi wanawake kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara, walipofika shuleni hapo kuhamasisha umuhimu wa usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa wasichana.
Mhandisi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara, Bi. Upendo Sanze, akielekeza jambo kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya KwaMtoro wilayani Chemba mkoani Dodoma, kuhusu umuhimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati.
Mwanafunzi Siminza Mambo, kutoka Shule ya Sekondari ya KwaMtoro wilayani Chemba mkoani Dodoma, akitoa maoni kwa Wahandisi wanawake kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) walipofika shuleni hapo kuhamasisha usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa wasichana.
Wahandisi wanawake kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara, wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi pamoja na walimu wa Shule ya Sekondari ya Dalai, wilayani Kondoa mkoani Dodoma mara baada ya kutoa elimu ya umuhimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa wanafunzi hao.
Maabara ya Shule ya Sekondari ya KwaMtoro wilayani Chemba mkoani Dodoma licha ya kukamilika lakini bado inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vifaa.
Picha na WUUM
No comments:
Post a Comment