HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 18, 2019

BODI YA URATIBU WA NGOs YAFUTA USAJILI WA MASHIRIKA SITA

* Mashirika matatu yaenda kinyume na maadili na utamaduni wa Nchi.

* Mengine matatu yaomba kufutwa kwa kukiri kukiuka Katiba zake.

Kikao cha 40 wa Bodi ya Nne ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kimeyafutia usajili Mashirika 6 Yasiyo ya Kiserikali kufanya kazi na kutoa huduma zake hapa nchini kufuatia kukiuka Kanuni za Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali lakini pia kufanya kazi kinyume na Katiba zao kama zilivyowasilishwa kwa Msajili wa Mashirika hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa Bodi ya Uratibu wa NGOs jijini Dodoma Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Neema Mwanga alisema kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya ripoti ya uchunguzi wa Mashirika hayo kuwasilishwa katika kikao hicho kilichofanyika   tarehe 17 Aprili, 2019.

Ameyataja Mashirika yaliyofutwa kwa kutozingatia Sheria, Kanuni, taratibu na maadili ya nchini kuwa ni Shirika la Community Health Education Services & Advocacy (CHESA), Kazi Busara na Hekima (KBH Sisters), AHA Development Organization Tanzania, Pathfinder Green City, Hope and Others na HAMASA Poverty Reduction(HAPORE).

Aidha Mwanga alifafanua kuwa Mashirika ya Community Health Education Services & Advocacy (CHESA), Kazi Busara na Hekima (KBH Sisters), pamoja na AHA Development Organisation Tanzania  yamefutiwa usajili kutokana na kosa la kukikuka Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali pamoja na Katiba iliyowasilishwa katika Ofisi ya Msajili kwa kuhamasisha matendo yasiyofaa katika jamii mambo ambayo ni ukiukaji wa Sheria, maadili na utamaduni wa Tanzania.

Aidha Mwanga aliongeza kuwa Mashirika ya Pathfinder Green City, Hamasa Poverty Reduction (HAPORE) na Shirika la Hope and Others yenyewe yaliomba kujitoa kwenye Orodha ya Msajili baada ya kutuhumiwa kuendesha kazi  zao kinyume na Katiba zake na hivyo Bodi ilielekeza Mashirika hayo kufutwa kwenye daftari la usajili.  

Aidha, Msajili amefafanua kuwa ufutwaji wa Mashirika hayo umefanywa  kwa mujibu wa kifungu cha 20 (1) (c)  cha Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2005 inayosema kuwa pale Msajili wa Mashirika hayo atakapopokea tuhuma kuhusu Shirika au Mashirika yanayofanya kazi zake pasipo kufuata Sheria, Kanuni na taratibu za nchini Msajili hupeleka notisi au onyo kwa Shirika husika kujiteteta kabla ya kufikia maamuzi ya kufutiwa usajili.

Msajili ameongeza kuwa endapo Ofisi ya Msajili isiporidhika na utetezi wa Shirika au Mashirika yanayotuhumiwa kukiuka Sheria, Kanuni na taratibu itapeleka mashauri hayo katika Kikao cha Bodi ya Uratibu wa Mashirika hayo na hao ndio wenye Mamlaka ya kutoa idhini ya kufutwa au kutofutwa kwa Shirika.

Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Nne ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini Dkt. Faustine Sambaiga amesema kuwa wameielekeza Sekretarieti kuyafutia usajili Mashirika yote Yasiyo ya Kiserikali ambayo yamekuwa hayafuati Sheria, Kanuni na taratibu za nchini ili kukidhi matakwa ya kisheria.

 “ Kama Bodi tunamuagiza Msajili kuyafutia usajili Mashirika hayo kwani Bodi ndio yenye Mamlaka ya kutoa idhini kwa Msajili wa  NGOs kuyafuta Mashirika au kutoyafuta” alisisitiza Dkt Sambaiga.

Mwenyekiti huyo wa Bodi ameyasisitiza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za nchi na kuzingatia uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuchochea Ustawi na Maendeleo ya Jamii.

Hatua hii ya kuyafutia usajili Mashirika sita Yasiyo ya Kiserikali Nchini imekuja mara baada ya kuundwa kwa Bodi ya Nne ya Uratibu wa Mashirika hayo chini ya uwenyekiti wa Dkt. Faustine Sambaiga aliyeteuliwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli hivi karibuni kuongoza Bodi hiyo.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Nne ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini Dkt. Faustine Sambaiga (kushoto) akizungumza na wajumbe wa Bodi wakati wa kikao cha 40 cha Bodi hiyo kilichofanyika jijini Dodoma kulia ni Kaimu Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini Neema Mwanga.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu akizungumza na Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya Nne ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini Dkt. Faustine Sambaiga (kulia) mara baada ya kikao cha 40 cha Bodi hiyo kilichofanyika jijini Dodoma wa pili kushoto ni Kaimu Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini Neema Mwanga na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Usajili Bw. Leornard Baraka.  Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad