HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 20, 2019

ZANZIBAR YAADHIMISHA SIKU YA AFYA YA KINYWA NA MENO DUNIANI

Na Miza Kona Maelezo Zanzibar
Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohammed amewataka Madaktari kufanya utafiti wa kina ili kujua kiwango cha maradhi ya kinywa na meno na namna ya kupunguza maradhi hayo katika jamii.

Waziri Hamad ameyasema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Kinywa na Meno duniani iliyofanyika Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi Kisonge mjini Zanzibar.

Amesema utafiti huo utaweza kusaidia kutoa taaluma zaidi kwa Walimu wanaofundisha watoto wakiwa skuli na hivyo kuwajengea uwezo wa kujikinga na matatizo ya kutoboka kwa meno na kuvimba fizi.

Amefahamisha kuwa kufanyika kwa utafiti huo kutasaidia kupatikana kwa takwimu sahihi na kuweza kujua ukubwa wa maradhi hayo na kupatiwa ufumbuzi wake.

Aidha amewataka wananchi kuvitumia Vituo vya afya na hospitali za serikali kupata huduma zilizobora ili kuondoa matatizo yanayowakabili.

“Nia ya Serikali ni kuwa na taifa la watu wenye afya ni vyema kupima afya zetu angalau mara mbili kwa mwaka katika Vituo vya afya vilivyokaribu nasi,” alieleza Wazri Hamad

Aidha Waziri huyo wa Afya aliwaomba wananchi kufanya usafi wa kinywa pamoja na kuwafundisha watoto namna ya kupiga mswaki ili kuepuka matatizo kutoboka kwa meno na kutoa harufu katika kinywa.

“Asilimia 90 ya matibabu ya maradhi haya tunayo wenyewe, tiba zaidi ni kuwa wasafi, hivyo nawaomba sana kuzingatia usafi maana afya ni usafi” alisisitiza Waziri Hamad.

Waziri Hamad alitumia fursa hiyo kuwasisitiza Wananchi kuchangia damu kwa lengo la kusaidia jamii na kuokoa maisha ya wagonjwa ambao wanakabiliwa na tatizo la kupoteza damu.

Aidha amewasisitiza madaktari na wahudumu wa afya kuwa Wazalendo na kufanya kazi kwa bidii pamoja na lugha nzuri wakati wa kuwahudumia wananchi.

Nae Mkuu wa Kitengo cha Meno na Kinywa Hospitali ya Mnazimmoja Dk Semeni Shaaban Mohamed kuwa amesema asilimia 90 ya wananchi wana matatizo ya meno ni vyema kwa jamii kuwa na utamaduni wa chunguza afya ya meno ili kuepuka madhara ya kutoboka na kung’oka.

Aidha ameeleza kuwa kitengo chake kinakabiliwa na upungufu wa vifaa vya upasuaji pamoja na kuiomba serikali kupeleka huduma za meno katika vituo vidogo vidogo vya afya ili kuondoa usumbufu kwa wananchi kufuata huduma katika hospitali hiyo.
 Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akizungumza na wananchi na Madaktari katika maadhimisho ya siku ya kinywa na meno Duniani yaliyofanyika Mapinduzi Square Michenzani Mjini Zanzibar, (kushoto) Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Sleiman na kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Meno na Kinywa Hospitali ya Mnazimmoja Dkt. Semeni Shaban Mohd.
 Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akiwa na mmoja wa madaktari wa kujitolea kutoka Finland Prof. Ana Pucar akionyesha jinsi ya kupiga msuwaki katika maadhimisho ya siku ya kinywa na meno Duniani.
 Daktari bingwa wa meno Zanzibar Iddi Suleiman akifanyia uchunguzi wa meno mtoto Rashid Msote.
 Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika maadhimisho ya siku ya kinywa na meno Duniani wakiwa kwenye foleni kwa ajili yakwenda kufanyiwa uchunguzi wa kinywa na meno.
Timu ya madaktari wa kujitolea kutoka Finland wakiwa na furaha katika siku ya afya kinywa na meno Duniani iliyoadhimishwa Mapinduzi Square Michenzani Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad