HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 11 March 2019

WASTAAFU ENDELEENI KULIUNGA MKONO JESHI LA POLISI - RPC SHANA

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Askari pamoja na watumishi raia waliolitumikia Jeshi la Polisi mpaka kufikia kustaafu wametakiwa kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo katika kutoa taarifa mbalimbali zitakazosaidia kupambana na uhalifu.

Wito huo umetolewa na Kamanda mpya wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shana jana usiku, katika sherehe ya kuwaaga wastaafu hao ambao ni Mkaguzi mmoja, askari wa vyeo mbalimbali 10 pamoja na watumishi raia wawili iliyofanyika katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi uliopo jijini hapa. 

“Ninyi ndugu zetu tunaomba muendelee kutusaidia katika azma yetu ya kupambana dhidi ya uhalifu na wakati wowote mlango ya ofisi yangu upo wazi kwa ajili ya kuwasikiliza”. Alisema Kamanda Shana ambaye aliwasili mkoani hapa juzi usiku akitokea Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.

Aidha kamanda Shana aliahidi kuwaunga mkono TPF NET mkoani hapa na kuwataka wanawake wasikubali kunyanyaswa na kujiona wanyonge bali wanatakiwa kusonga mbele kwa ajili ya maendeleo ya familia zao huku akitoa mifano ya baadhi ya nafasi za juu za wanawake ambao wapo katika idara na taasisi mbalimbali na wameonekana wakifanya vizuri zaidi kiutendaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF NET) mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi Namsemba Mwakatobe alisema kwamba, wameamua kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kuunganisha sherehe ya kuwaaga wanawake wenzao pamoja na kuwapa zawadi mbalimbali.

Alisema baadhi ya wastaafu hao katika kipindi chao cha utumishi walikuwa walimu wa askari na watumishi raia waliopo hivi sasa hali ambayo imesaidia kuendelea kupata kizazi kingine kinachofanya kazi kwa ufanisi na uweledi wa hali ya juu.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wastaafu Bi. Azama Libundilo ambaye alikuwa na cheo cha Staff Sajenti alisema kwamba kitendo kilichofanywa na wanamtandao huo pamoja na viongozi wa Polisi mkoa,cha kuwathamini wastaafu kinapaswa kuigwa na ofisi zote ambazo hazina utamaduni huo kwani kinawatia moyo nakujiona kwamba bado ni familia ya jeshi hilo.
 Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shana akimkabidhi zawadi Sajenti mstaafu wa Polisi Rukia Msofe wakati wa sherehe ya kuwaaga wastaafu iliyoandaliwa na TPF NET Arusha na kufanyika bwalo la Maofisa wa Polisi lililopo jijini hapa (Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha)
   Mary Simbano  ambaye alikuwa Mhasibu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Arusha, akipewa zawadi binafsi na wanachama wa TPF NET Arusha wakati wa sherehe za kuwaaga wastaafu ambao ni  askari na watumishi raia waliokuwa wanafanya kazi mkoani hapa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha)
 Baadhi ya Polisi wanawake ambao ni wanachama wa TPF NET Arusha wakifungua Champaign wakati wa sherehe ya kuwaaga wastaafu waliotumikia Jeshi hilo iliyofanyika katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi. (Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha)
 Baadhi ya wageni waalikwa wakihudumiwa chakula wakati wa sherehe ya kuwaaga wastaafu ambao ni askari na watumishi raia iliyoandaliwa na TPF NET Arusha (Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha). 

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad