HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 7, 2019

Wamiliki wa vyombo vya usafiri washauriwa kuchangamkia fursa Dodoma

Wamiliki wa vyombo vya usafiri jijini Dodoma, wameshauriwa kuchangamkia fursa ya kutoa huduma ya usafiri kutoka maeneo  mbalimbali ya jiji hilo kuelekea mji wa serikali ambako ofisi za serikali zinajengwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi na wadau wa serikali.
Ushauri huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb), alipofanya ziara kuangalia maendeleo ya ujenzi wa ofisi yake katika mji wa serikali, Ihumwa ambayo iko kwenye hatua za mwisho kukamilika kwa ajili ya kutoa huduma.

Mhe. Mkuchika amesema, ofisi yake itaanza kutoa huduma siku chache zijazo, hivyo uwepo wa huduma ya usafiri ni muhimu sana, kwani itawawezesha wananchi kufika kwa urahisi kupata huduma ikiwa ni pamoja na kuwarahisishia watumishi wa ofisi yake na taasisi nyingine kufika kwa wakati katika maeneo yao ya kazi.

Aidha, Mhe. Mkuchika amezitaka taasisi zote za umma zinazojenga ofisi katika mji wa serikali, kuishirikisha Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) ili kupata ushauri wa kitaalamu wa namna bora ya kujenga miundo mbinu rafiki ya TEHAMA itakoyorahisisha utoaji huduma kwa umma.  “Ni vema, taasisi zinazojenga ofisi katika mji wa serikali kuomba ushauri wa kitaalamu wa usimikaji wa miundombinu ya TEHAMA kabla ya kukamilisha ujenzi ili kuziwezesha taasisi hizo kuwa na mifumo ya TEHAMA ya utoaji huduma ya uhakika,” Mhe. Mkuchika amesisitiza.

Mhe. Mkuchika ameipongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa hatua nzuri ya ujenzi iliyofikiwa na Menejimenti ya ofisi yake kwa usimamizi mzuri.  Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ameridhishwa na ujenzi wa ofisi hiyo kwani umezingatia mahitaji muhimu ya kundi maalum kwa kuweka miundombinu rafiki itakayowawezesha wananchi wenye ulemavu wa miguu kupata huduma bila kikwazo.

Pia, Dkt. Mwanjelwa amesema, ofisi yake imedhamiria kuwa ya kwanza kutoa huduma katika mji wa serikali kama ilivyokuwa ya kwanza kuanza ujenzi katika mji huo, hivyo haoni kikwazo chochote cha kutekeleza azma hiyo kutokana na hatua nzuri ya ujenzi iliyofikiwa.

Ujenzi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika mji wa serikali, Ihumwa ni sehemu ya mwendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ya kuhamishia shughuli za serikali jijini Dodoma aliyoyatoa tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa maadhimisho ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) akiwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) na baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Rais-Utumishi wakiwasili katika Mji wa Serikali kuangalia maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Utumishi katika mji huo Ihumwa, jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) akitoa maelekezo kwa Mhandisi, Lucas Lipambila (kushoto) wakati wa ziara ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Utumishi katika mji wa serikali Ihumwa, jijini Dodoma. Katikati ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb).
Afisa Tawala Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Donald Bombo akisisitiza jambo kwa Mhandisi Lucas Lipambila (wa pili kutoka kulia) baada ya kumalizika kwa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Utumishi katika mji wa serikali Ihumwa, jijini Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) akizungumza mara baada ya kumaliza ziara yake ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa ofisi za Utumishi katika mji wa serikali Ihumwa, jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) na baadhi ya watumishi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akisisitiza jambo baada ya kukamilika kwa ziara ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa ofisi za Utumishi katika mji wa serikali Ihumwa, jijini Dodoma. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb).

Muonekano wa jengo la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora linalojengwa katika mji wa serikali Ihumwa, jijini Dodoma

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad