HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 20, 2019

UHAMIAJI WAFANYA WARSHA YA USHIRIKISHWAJI WA WANANCHI KATIKA ULINZI NA UDHIBITI WA MIPAKA

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Charles Kabeho amefungua warsha ya siku tatu wa ushirikishwaji wa wananchi katika ulinzi na uthibiti wa mipaka kuanzia  tarehe 19 hadi 21 Machi, 2019. Ufunguzi huo umefanyika katika ofisi za kituo cha Uhamiaji Sirari, Wilayani Tarime Mkoa wa Mara.

Kabeho amewataka washiriki kuzingatia yale yote watakayofundishwa na kwenda kuyafanyia kazi katika maeneo wanayoishi. Pia alieleza kwamba maeneo ya mpakani kuna changamoto nyingi ambazo vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi nyingine za serikali zilizopo mpakani haziwezi kuzimaliza peke yake bila ya ushirikishwaji wananchi.

“Ndugu washiriki, kwanza napenda kuwapongeza kwa kuchaguliwa kwenu kushiriki, wengi wenye sifa kama ninyi hawakuipata hii nafasi. basi naomba nafasi hii muitumie vizuri katika kujifunza na mafunzo mtayopata  mkawaelimishe wana jamii wengine ambao hawakupata fursa hii.” Ameeleza Kabeho.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Wilaya kufungua warsha, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara Naibu Kamishna Fredrick Kiondo ameishukuru Idara ya Uhamiaji Makao Makuu na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji(IOM) kwa kuwafikia wananchi moja kwa moja ili kuwapatia elimu juu ya changamoto zinazokabili maeneo ya mipakani.

“Nawashukuru Uhamiaji Makao Makuu na IOM kwa juhudi zao kubwa kuelimisha jamii ya mipakani. Tunazo changamoto nyingi kwenye masuala ya wahamiaji haramu, magendo ya binadamu, usafirishaji haramu wa binadamu, magendo ya bidhaa, madawa ya kulevya (Mirungi) na uhalifu mwingine wa Kimataifa. Ni imani yangu kuwa jamii ikipata uelewa itashirikiana vyema na Idara ya Uhamiaji na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kufichua maovu hayo.”

Warsha hiyo ya siku tatu inashirikisha viongozi kuanzia kitongoji hadi kata, viongozi wa dini, wadau wa mpaka, viongozi wa bodaboda na mabasi ya abiria kwa upande wa Tanzania na Kenya kwa siku ya kwanza, na siku ya pili na siku  ya tatu ni mikutano ya hadhara na wananchi wa Kata zinazozunguka mpaka wa Sirari. Ni imani kubwa kwa idara ya Uhamiaji Tanzania kuwa wananchi wengi watapata elimu katika masuala ya Uhamiaji, Uraia, Taratibu za Kuingia, Ukaazi na Utokaji nchini, Wahamiaji Haramu, Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Uhalifu wa Kimataifa, Magendo ya Binadamu na masuala yote ya Ulinzi na Udhibiti wa Mpaka katika maeneo yao.
Wawezeshaji wa Warsha, Ally Mtanda na David Lukiru wakitoa somo kwa washiriki wa warsha  ya ushirikishwaji wa wananchi katika ulinzi na udhibiti wa mipaka iliyofanyika katika ofisi za kituo cha Uhamiaji Sirari, Wilayani Tarime Mkoa wa Mara.
Washiriki wa kiwa kwenye warsha ya ushirikishwaji wa wananchi katika ulinzi na udhibiti wa mipaka iliyofanyika katika ofisi za kituo cha Uhamiaji Sirari, Wilayani Tarime Mkoa wa Mara.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad