HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 22, 2019

TBS YAKABIDHI LESENI KWA WAZALISHAJI WA BIDHAA AMBAZO ZIMEKIDHI VIGEZO VYA UBORA


*Yawashauri kutumia alama ya ubora kupanua soko la bidhaa zao kwa maslahi ya nchi

Na Said Mwishehe, Globu ya Jamii
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa ushauri kwa wazalishaji ambao bidhaa zao  zimekidhi matakwa ya viwango na kukabidhiwa leseni  za kutumia alama ya ubora kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kupanua masoko yao ikiwa pamoja na kuuza bidhaa zao nje ya nchi.

Ushauri huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TBS Profesa Makenya Maboko wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Viwango Afrika (ARSO)  yaliyofanyika makao makuu ya shirika hilo Ubungo  jijini Dar es Salaam. 
Maadhimisho yameenda sambamba na utoaji leseni  za kutumia alama za ubora kwa wazalishaji ambao bidhaa zao zimekidhi matakwa ya viwango. 
"Alama ya ubora ni muhimu katika biashara , kwani inampa mzalishaji uhakika  kuhusiana na ubora na usalama wa bidhaa yake, hivyo kumjengea imani kwa walaji.Pia alama ya ubora humsaidia mzalishaji  kupanua masoko ya bidhaa zake nje ya nchi,"amesema Prof. Maboko Amesisitiza hatua hiyo ni ya kujivunia kwa wazalishaji ambao wamefikia hatua hiyo ya bidhaa ambazo wanazalisha kukidhi viwango vya ubora na kupewa leseni ya kutumia alama hiyo na kwamba kamaTaifa kupanuka kwa masoko  ya kikanda na kimataifa  kutasaidia kuongeza fedha za kigeni, hivyo kusaidia kukuza uchumi.
Amefafanua kuwa hali hiyo  itasaidia kufikiwa kwa azma ya Taifa ya kujenga uchumi wa kati unaotegemea uzalishaji wa viwandani ifikapo mwaka 2025.
 Hata hivyo amewataka wazalishaji  waliopatiwa leseni hizo  kuzingatia masharti yake na kuwa waadilifu katika uzalishaji wao, ili kuhakikisha wanaendelea kuzalisha bidhaa  zinazokidhi matakwa ya viwango wakati wote. 
 Akizungumzia jitihada zinazofanywa na Rais Dkt. John Magufuli  katika kupambana na rushwa nchini, Prof.Maboko, ameeleza  wao kama wadau wa viwango ni fursa muhimu  ya kuhakikisha wanatoa mchango wao kwa kueneza uelewa na weledi unaotumika katika kuandaa viwango na pia kuwahamasisha wazalishaji na watoa huduma kuhusu umuhimu wa kuzingatia matakwa ya viwango katika shughuli zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Yusuf Ngenya, amesema wao kama taasisi Siku ya Maadhimisho ya  Viwango Afrika ni muhimu, kwani wanapata fursa ya kuwakumbusha wazalishaji, watoa huduma na wananchi wote kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora katika maisha yao ya kila siku.
Kwa mujibu wa Dkt. Ngenya , kauli mbiu ya Maadhimisho hayo ya saba ya Siku ya Viwango Afrika ni ; “Nafasi ya viwango katika kufanikisha mapambano dhidi rushwa kwa mabadiliko endelevu  ya  Afrika.”

Amefafanua kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua katika suala la vita dhidi ya rushwa, hivyo na wao katika tasnia ya viwango, wanayo fursa ya kuonesha njia katika kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa, hivyo kuhakikisha rasilimali za nchi  zinatumika ipasavyo katika kuondoa wananchi katika umaskini na kuwaletea maendeleo.
Ameongeaza kuwa wanayo fursa ya kuweka kielelezo cha uadilifu kwa kuhakikisha  kuwa michakato ya ukaguzi, upimaji, ugezi, utoaji leseni na udhibiti ubora kwa ujumla inafanyika kwa kuzingatia misingi na taratibu.
Pamoja na mambo mengine maadhimisho hayo yamekwenda sambamba na utoaji zawadi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu walioshiriki na kushinda shindano la insha  lililojikita katika kauli mbiu ya maadhimisho hayo.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Profesa Makenya Maboko (watatu kutoka kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dkt. Yusuf Ngenya (kulia kwake) akiwa amesimama na wajumbe wa bodi na menejimenti ya shirika kwa ajili ya kuanza kutoa leseni za kutumia alama za ubora kwa wazalishaji ambao bidhaa zao zimekidhi viwango. Hafla hiyo ilifanyika makao makuu ya shirika hilo Ubungo jijini Dar es salaam  ambapo imekwenda sambasamba na Maadhimisho ya Siku ya Viwango Afrika.
 Mmoja ya wazalishaji wa bidhaa nchini akiwashukuru maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania(TBS) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi waliokuwa mezaa kuu kwa kuwapa mkono baada ya kukabidhiwa leseni yake kutokana na bidhaa anazozalisha kukidhi vigezo vya ubora unaotakiwa na shirika hilo.
 Mmoja wa washiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Viwango Afrika (ARSO)  akizungumza jambo wakati wa hafla hiyo iliyofanyika makao makuu ya shirika hilo Ubungo  jijini Dar es Salaam . 
Baadhi ya washiriki kutoka vyuo vikuu mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja katika ofisi za Makao Makuu ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Ubungo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad