HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, March 23, 2019

TANZANIA YAENDELEA KUSHIKILIA CHETI CHA UBORA KATIKA HUDUMA ZA HALI YA HEWA KATIKA USAFIRI WA ANGA KUPITIA TMA

Na Karama Kenyunko. Globu ya Jamii
WAZIRI wa Ujenzi,Uchukuzi  na Mawasiliano, Mhandisi, Isack Kamwelwe amesema utabiri sahihi wa hali ya hewa nchini Tanzania unaofanywa na mamlaka ya hali ya hewa nchini (TMA), umeiwezesha  Tanzania kuwa miongoni mwa nchi ya tatu barani kutunukiwa  cheti cha ubora wa huduma za hali ya hewa katika usafiri wa anga. (ISO 9001:2015)na hiyo ni kwa mujibu wa Shirika la Viwango Duniani(ISO.)

Akizungumza leo Machi 23 mwaka huu wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Hali ya Hewa Duniani,  Mhandisi Kamwelwe amesema, ili kuhakikisha wananchi wanaelewa umuhimu wa hali ya hewa serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za hali ya hewa kwa matumizi ya sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya anga, Kilimo na miundombinu ya uangazi.
 Amesema, kwa kuhakikisha hilo  serikali imenunua Radar mbili za hali ya hewa ambazo zimewekwa Dar es Salaam na Mwanza huku Radar nyingine tatu ambazo ziko katika hatua ya ununuzi zinatarajiwa kuwekwa katika mikoa ya Mtwara, Mbeya na Kigoma.

"Siku ya hali ya hewa Duniani ni muhimu sana kwani inatupa nafasi ya kutafakari mchango wa Tanzania kama mwanachama wa WMO katika utoaji wa huduma za hali ya hewa hapa Tanzania na ulimwenguni kote" amesema Kamwele.

Kamwelwe amesema katika sekta ya usafiri wa anga mwaka huu Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi tatu barani Afrika zilizopata cheti hicho.

"Kauli mbiu ya mwaka huu ya ‘Jua, Dunia na hali ya hewa imelenga  kutoa elimu kwa jamii na kuongeza uelewa wa sayansi ya hali ya hewa hususani maandalizi, usambazaji na matumizi ya taarifa za hali ya hewa,”amesema Kamwelwe.

Amesema ni dhahiri kwamba huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) zimeendelea kuongeza viwango vya ubora ikiwa ni pamoja na usahihi wa utabiri na zinafaa kutumika katika sekta mbalimbali za maendeleo hapa nchini.

“Katika maadhimisho haya ya 69 ya hali ya hewa duniani ya kauli mbiu ya mwaka huu ‘JUA,Dunia na hali ya hewa’ ambayo imelenga kutoa elimu kwa jamii na kuongeza uelewa wa sayansi ya hali ya hewa hususani maandalizi, usambazaji na matumizi ya taarifa za hali ya hewa,”amesema Kamwelwe.

Ameongeza kuwa, pamoja na mafanikio hayo bado kuna changamoto nyingi zikiwemo  gharama kubwa za vifaa vya hali ya hewa, kuendana na mabadiliko ya kukua kwa teknolojia katika tasnia ya hali ya hewa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi ambapo utatuzi wa changamoto hizo unahitaji jitihada za pamoja za wadau.

 Mkurugenzi Mkuu wa TMA,Dk Agness Kijazi amesema TMA  imepata mafanikio mengi ikiwa ni pamoja na kuendelea kumiliki cheti cha Ubora ISO 900;2015 ambapo Tanzania imekuwa nchi ya tatu barani Afrika kufikia viwango vya ubora hiyo ni mpya iliyotolewa na Shirika la Viwango Duniani.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usafiri wa Anga nchini (TCAA), Hamza Johari amesema,  Huduma za hali ya hewa zimekuwa ni msaada mkubwa sana katika sekta ya anga hasa kwa kuepusha majanga hasa safarini na kufanya ajali katika sekta hii kuwa chache, "kwa rubani kabla hajaanza safari lazima tupate huduma za hali ya hewa katika njia ambayo atapaswa kupita ili wafike salama na iwapo hali ya hewa ikiwa mbaya basi rubani hataruhusiwa kisafiri" ameeleza Johari

Pia  Kaimu Mkurugenzi wa Mkuu wa Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini, (TAA), Elias Mwashiuya amesema, mpaka sasa kuna viwanja 58 na katika viwanja hivyo msingi mkuu ni hali ya hewa. "Tunaangalia kulingana na hali ya hewa pia wanazingatia takwimu za hali ya hewa kulingana na aina ya ndege. Pia tunapata taarifa za kila baada ya saa sita ili kuweza kujua hali ya anga zitakazomuwezesha rubani kutua au kuruka" amesema.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la uwakala wa meli Tanzania, Eng.Japhet L Loisimaye (OLe) amesema utabiri wa Hali ya hewa unaofanywa na TMA umekuwa ukisaidia sana vyombo vya majini kwani haviruhusiwi kuanza safari kabla havijapata utabiri wa hali ya hewa. Kwani wamekuwa wakisimamisha safari za vyombo vya baharini bila kujali hasara watakayoipata bali wanahakikisha na  kuangalia usalama wa wananchi kwanza.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Isack Kamwelwe (kushoto) akihutubia wadau wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani iliyoandaliwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Eng. Japhet Loisimaye akielezea namna taarifa zinazotolewa na TMA zinavyowasaidia wadau wa mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yao, kwenye hafla ya maadhimisho ya siku ya Hali ya Hewa Duniani iliyoandaliwa na TMA jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka za Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Hamza Johari pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Elias Mwashiuya (kulia).
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Hamza Johari (katikati) akielezea jinsi taarifa zinazotolewa na TMA zinavyowasaidia wadau wa usafiri wa anga kutekeleza majukumu yao, kwenye hafla ya maadhimisho ya siku ya Hali ya Hewa Duniani iliyoandaliwa na TMA jijini Dar es Salaam. Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka za Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Eng. Japhet Loisimaye (kulia).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka za Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi (kushoto) akizungumza na wadau wa TMA katika maadhimisho ya siku ya Hali ya Hewa Duniani iliyoandaliwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). Kulia ni wadau wa TMA wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TMA, Dk. Buruhani Nyenzi (kushoto) akimpongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Isack Kamwelwe (katikati) mara baada ya kuwahutubia wadau wa Mamlaka za Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwenye maadhimisho hayo. Kulia ni Dk. Kijazi akifuatilia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad