HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 14, 2019

MIGOGORO YA ARDHI YAMRUDISHA WAZIRI LUGOLA MKOANI MOROGORO

Na Felix Mwagara, MOHA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola anatarajia kuwasili kwa mara nyingine Mkoani Morogoro leo, kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi ambayo imeibua mifarakano baina ya wananchi Mkoani humo.
Waziri Lugola, wiki iliyopita alimaliza ziara yake Mkoani humo iliyokuwa na lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi kuhusiana na utendaji kazi wa Taasisi za Wizara yake.
Lugola katika ziara yake Mkoani humo, alifanya mikutano ya hadhara ambapo alikutana na migogoro mbalimbali lakini kero kubwa kati ya hizo ni kuhusiana na ardhi ambayo inapelekea wananchi kuwekeana chuki, kujeruhiana, kufikishana Polisi pamoja na kuuana.
Kati ya Wilaya tatu alizozitembelea alipokuwa Mkoani humo, ni Morogoro, Mvomero na Kilosa, licha ya wananchi kutoa kero zao mbalimbali, mgogoro wa ardhi uliibuka kwa sehemu kubwa hasa katika Wilaya ya KIlosa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Waziri Lugola alisema alipokuwa Wilaya ya Kilosa, alikutana na mgogoro wa ardhi ambapo umeleta mgawanyiko miongoni mwananchi hivyo akawaahidi kurejea tena Wilayani humo kwa ajili ya kutatua kero zao baada ya kukutana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Lugola alisema mipango yote ipo sawa, hivyo anatarajia kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kilosa Kesho Machi 15 Wilayani humo ili kuwapa majibu ya kero zao pamoja na kumaliza mgogoro wa ardhi unaowakabili. 
“Migogoro mingi inaletwa vituo vya polisi hasa Wilaya ya Kilosa, na wananchi katika mikutano yangu ya hadhara wanalalamika kuhusiana na ardhi, baadhi wanawalaumu polisi wangu kutokuwatendea haki na wengine pia wanawapongeza kwa kazi nzuri, na wengi wao wanalalamikia kuwa matajiri ndio wananyang’anya ardhi zao wakitumia fedha kwa wakiwahonga Polisi,” alisema Lugola.
Aliongeza kuwa, alipokuwa katika mkutano wake wa mwisho katika Tarafa ya Kimamba, Wilaya ya Kilosa Mkoani humo, kuliibuka na hoja nyingi za migogoro ya ardhi, kutokana na usugu wa tatizo hilo, aliwaahidi wananchi wa Wilaya hiyo atarejea tena kwa ajili ya kutatua mgogoro huo.
“Ziara yangu niliikatisha katika Mkoa huo, kwa ajili ya kwenda Dar es Salaam kuhudhuria kikao cha Baraza la Mawaziri, hata hivyo, niliwaahidi wananchi nitakutana na Waziri wa Ardhi, ili tushirikiane kutatua mgogoro huu ambao unaweza ukaleta vurugu kubwa pale Kilosa na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla,” alisema Lugola.
Lugola anatarajia kufanya mkutano mwingine wa hadhara kuleta majibu ya ahadi alizowaahidi wananchi hao pamoja na kusuluhisha mgogoro huo ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao za maendeleo. 
Waziri huyo alisema, hawezi kukaa ofisini huku wananchi wakiwa wanapata matatizo mitaani, hivyo atazunguka nchi nzima kuzungumza na wananchi na kupokea kero mbalimbali zinazowakabili.  
“Wananchi wanapojitokeza kwa wingi inasaidia kusikiliza matatizo yao yanayowakabili, ndio mana nimepanga kufanya ziara kama hizi nchi nzima, hii inasaidia sana kujua matatizo mbalimbali ya wananchi pamoja na kuangalia utendaji kazi wa Taasisi zangu zilizopo ndani ya Wizara hii, na hakika Serikali ya Dokta Magufuli inawajali wananchi wake ndio mana inawafuata mahali walipo, ili wazungumze na Serikali yao uso kwa uso,” Alisema Lugola. 
Lugola alisema Taasisi zilizopo ndani ya Wizara yake ambazo ni Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na Idara ya Probesheni na Huduma kwa Jamii, zifanye kazi za kiweledi bila kuwaonea wananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad