Na Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema wizara
kupitia timu yake maalum ya kushughulikia migogoro, hadi sasa imetatua
migogoro mikubwa 14 kati ya 29 inayohusisha wakulima na wafugaji
pamoja na hifadhi na wawekezaji.
Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na Mkuu wa
Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Mhe. Lengai Ole Sabaya pamoja na
viongozi wengine wa wilaya hiyo, mara baada ya kuarifiwa kuwepo kwa
mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Hai na kubainisha
kuwa ni hatari kwa jamii inayoishi pamoja kuwa na mgogoro wa aina
hiyo.
“Nitamsisitiza katibu mkuu mifugo aliangalie kwa karibu sana hili kwa
sababu ni hatari sana kwa jamii inayoishi pamoja kutokuwa na maelewano
ya kuachiana maeneo kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi.” Alisema
Mhe. Ulega
Ulega ametoa kauli hiyo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Hai Mhe.
Lengai Ole Sabaya kumuarifu kuwa baadhi ya maeneo yenye migogoro ni
Kata ya KIA ambapo wafugaji wamekuwa wakiingiza mifugo yao katika
maeneo ya uwanja wa ndege wa KIA, pamoja na wakulima wilayani humo
kutotaka kuwaachia wafugaji maeneo wasiyoyatumia kwa kilimo hususan
yenye magadi kwa ajili ya malisho kwa wafugaji hivyo kutengeneza chuki
dhidi yao.
Naibu Waziri Ulega amemshauri pia mkuu huyo wa wilaya kutumia Chuo cha
Mifugo Tengeru na Kituo cha Uhimilishaji cha Taifa (NAIC) vilivyopo
Mkoani Arusha ili kuleta mabadiliko kwa wafugaji katika Wilaya ya Hai
Mkoani Kilimanjaro kwa kuwa na ng’ombe wachache na wenye tija
ukizingatia ukanda huo kuna kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh ambacho
kinahitaji maziwa kwa wingi katika uzalishaji wao.
“Ukanda huu kuna kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh ambacho kinahitaji
lita laki moja ya maziwa kwa siku na bado hayatoshelezi hadi
inawalazimu kuchukua maziwa kutoka mikoa ya Iringa na Njombe ni vyema
mkashirikiana na wizara kutoa elimu ili wafugaji wa wilaya hii
wabadilike kwa kufuga kisasa hususan ng’ombe wa maziwa badala ya kuwa
na ng’ombe wengi wasio na tija kiuchumi.” Alisema Mhe. Ulega
Naibu Waziri Ulega amemshauri pia mkuu wa wilaya Mhe. Sabaya kuwa na
kampeni maalum ya kutoa elimu kwa wafugaji pamoja na kushirikiana na
wataalam ili wilaya hiyo iwe ya mfano katika kubadilisha fikra za
wafugaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Hai Lengai Ole Sabaya amesema
changamoto kubwa zilizopo wilayani hapo ni mgogoro kati ya wakulima na
wafugaji ambao tayari upo katika hatua mbalimbali za kutatuliwa pamoja
na wafugaji kutokuwa tayari kubadilika kutoka kwenye ufugaji wa zamani
wa kuwa na makundi makubwa ya mifugo isiyo na tija.
Kufuatia mazungumzo baina yake na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Ulega, mkuu huyo wa wilaya amesema atazidi kushirikiana na wizara hiyo
ili kuhakikisha changamoto hizo zinatatulika na kuifanya wilaya hiyo
kuzidi kunufaika na mifugo iliyopo.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega akifafanua jambo kwa viongozi wa Wilaya ya Hai (hawapo pichani) namna ya kuiboresha sekta ya mifugo wilayani humo
Baadhi ya viongozi wa Wialaya ya Hai, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya wakiwasilisha hoja mbalimbali kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega.
No comments:
Post a Comment