MAFUNZO YA SAIKOLOJIA KWA WADAU WA MAPAMBANO DHIDI YA UDALILISHAJI WANAWAKE NA WATOTO YAFUNGULIWA ZANZIBAR - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 4 March 2019

MAFUNZO YA SAIKOLOJIA KWA WADAU WA MAPAMBANO DHIDI YA UDALILISHAJI WANAWAKE NA WATOTO YAFUNGULIWA ZANZIBAR

Na Ramadhani  Ali - Maelezo                
Vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto bado vinaendelea kuongezeka Zanzibar licha ya juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali, Taasisi za kiraia na Mashirika wahisani ya Umoja wa Mataifa.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa watoa huduma wa waathirika wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinisi, mtoa huduma kutoka Kitengo cha Mkono kwa mkono Hospitali kuu ya Mnazimmoja Bi. Fatma Ali Haji alisema udhalilishaji wa kijinsia ni masuala yote ambayo hayapaswi kufanyiwa binadamu ikiwemo kuingiliwa kwa nguvu, kupigwa na kunyanyaswa.

Hata hivyo alisema hivi sasa jamii imekuwa na mwamko mzuri wa kutoa taarifa katika sehemu husika inapotokea vitendo vya udhalilishaji kinyume na ilivyokuwa zamani ambapo vitendo hivyo vilikuwa vikipatiwa suluhisho kwa njia za siri mitaani ili kuepuka aibu kwa muhusika.

Alisema hivi sasa kumefunguliwa vituo saba vya mkono kwa mkono viliopo katika hospitali za Zanzibar na vimekuwa vikitoa huduma nzuri kwa waathirika wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na wamejenga imani kutokana na msaada mkubwa wanaopata wanapofikwa na matatizo hayo.

Alisema mafunzo ya siku tano yaliyoandaliwa kwa ushirikiano na Shirika linaloshughulikia Idadi ya watu (UNFPA) na Wizara ya Afya yanalengo la kuwajengea uwezo wahudumu wa vituo hivyo waweze kutoa huduma bora zaidi kwa waathirika.

Alisema mtoto anapobakwa pamoja na wazazi huwa wanachanganyikiwa na kupata msongo wa mawazo hivyo huhitaji msaada mkubwa kutoka kwa wahudumu wa vituo vya mkono kwa mkono ili waweze kurejea katika hali ya kawaida.

Aliwashauri wazazi na walezi wanapopata matatizo ya udhalilishaji wa kijinsia watoe taarifa katika vituo vya mkono kwa mkono ambavyo vinawatendaji kutoka taasisi mbali mbali ili kurahisisha utoji wa huduma .

Akifungua mafunzo hayo, Naibu Waziri wa Afya Bi. Harusi Said Suleiman aliwataka washiriki wa mafunzo hayo ambao ni watoa hudumu wa watu walioathirika kutumia lugha nzuri na kuwapa upendo kwani kufanya hivyo ni kuwapunguzia maumivu waliyopata.

Alisema kuanzishwa kwa vituo vya mkono kwa mkono katika Hospitali za Zanzibar kunatoa nafasi ya kuimarisha huduma kwa wahanga wa matendo ya udhalilishaji na kuona huduma zinazotolewa katika vituo hivyo vinafikia vigenzo vya kimataifa vinavyokubaliwa na Shirika la Afya ulimwenguni WHO.
 Baadhi ya Wadau wa Mapambano dhidi ya Udhalilishaji waliohudhuria katika Mafunzo ya siku Tano ya Saikolojia yaliofanyika Ukumbi wa Hospitali ya Wagonjwa wa Akili Kidongo chekundu mjini Unguja.
 Msaidizi Meneja Kitengo Shirikishi Afya ya Mama na Mtoto Dk Mtumwa Ibrahim akitoa hotuba ya kumkaribisha Mgeni Rasmi ili kuyafungua  Mafunzo ya siku Tano ya Saikolojia kwa Wadau wa Mapambano dhidi ya udhalilishaji  yaliofanyika Ukumbi wa Hospitali ya Wagonjwa wa Akili Kidongo chekundu mjini Unguja.
 Naibu Waziri wa Afya Harusu Saidi Suleiman akitoa hotuba ya Ufunguzi wa Mafunzo ya siku Tano ya Saikolojia kwa Wadau wa Mapambano dhidi ya udhalilishaji  yaliofanyika Ukumbi wa Hospitali ya Wagonjwa wa Akili Kidongo chekundu mjini Unguja.
 Mwezeshaji wa Mafunzo Edwick Mapalala akitoa mafunzo ya Saikolojia kwa Wadau wa Mapambano dhidi ya udhalilishaji  yaliofanyika Ukumbi wa Hospitali ya Wagonjwa wa Akili Kidongo chekundu mjini Unguja.
Mtoa huduma wa kitengo cha Mkono kwa Mkono Dk,Fatma Ali Haji akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na Udhalilishaji katika ufunguzi wa Mafunzo ya siku Tano ya Saikolojia kwa Wadau wa Mapambano dhidi ya udhalilishaji  yaliofanyika Ukumbi wa Hospitali ya Wagonjwa wa Akili Kidongo chekundu mjini Unguja. PICHA NA YUSSUF SIMAI/MAELEZO ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad