HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, March 23, 2019

JE, WAJUWA FRANCO MAKIADI ALIZIKWA MARA MBILI MAKABURI TOFAUTI?

Na Moshy Kiyungi
Rekodi ambayo haiwezi kusahaulika barani Afrika pengine duniani kote, ni ya aliyekuwa mwanamuziki nguli hayati Franco Luambo Luanzo Makiadi, mwili wake kuzikwa mara mbili katika makaburi tofauti.

Tukio lingine ni lile ambalo kamwe halijasikika sehemu nyingine ni lile la mke mmoja aliyeolewa na marais wawili kwa nyakati tofauti.

Graca aliyekuwa mke wa rais wa Msumbiji hayati Samora Machael, baada ya kufariki mumewe, akaja kuolewa na aliyekuwa rais wa nchi ya Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela.

Wapenzi na mashabiki wa muziki wa dansi toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na nchi jirani, kila mwaka ifikapo mwezi wa Oktoba hukumbuka kifo cha mwanamuziki huyo.

Franco alipatwa na mauti Oktoba 12, 1989 akiwa katika hospitali mojawapo nchini Ubelgiji alikokuwa amelazwa kwa maradhi ya muda mrefu.

Mwili wake ulisafirishwa ukarejeshwa kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Zaire zamani), kwa mazishi.

Baada ya kufikishwa nchini mwake, jeneza lililokuwa limebeba mwili wake lilipitishwa mitaani kuagwa na wananchi likisindikizwa na ulinzi mkali wa polisi na baadaye serikali ikatangaza siku nne za maombolezo ya kitaifa.

Siku ya mazishi yake, Leon Kengo wa Dondo,  alikwenda kutoa heshima zake za mwisho kwa niaba ya serekali.

Mazishi ya mara ya kwanza

Wakati wa misa  ya mazishi yake, Padre alitamka “Luambo alikuwa Mtume wa muziki, hakuna alichokisahau katika utunzi wake, kavichambua vitu kadhalika na watu wa kila rika, hata rais Mobutu hajaachwa nyuma.

Nyimbo zake kadhaa zilipigwa marufuku, hata hivyo ziliendelea kupendwa sana na umma. huku nyimbo zake  nyingine hadi leo huchukuliwa kama nembo ya taifa….”

Katika siku hizo za maombolezo radio ya taifa hilo ilikuwa ikipiga nyimbo za Franco hadi tarehe 17, Oktoba 1989 alipozikwa kwa heshima zote za kitaifa.Mazishi mara ya pili:

Baadaye serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilieonesha kwa kiasi kikubwa kuwathamini wanamuziki waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Uchumi na Siasa nchini humo.

Mabaki ya mwili wa Franco Luanzo Makiadi yaliyokuwa katika makaburi ya Gombe, yalifukuliwa na kwenda kuzikwa kwa mara ya pili eneo ambako kulijengwa mnara wa sanamu yake karibu lango la kuingilia makaburi hayo yakitazamana na barabara kubwa ya  Bulbati.

Kwa kuthamini mchango wake mkubwa kwa taifa, Waziri Mkuu wa nchi hiyo wakati huo Augustin Matata kwa niaba ya serikali yake, alizindua mnara  huo Oktoba 17, 2015, wakati wa sherehe kubwa ya maadhimisho ya miaka 26 ya kifo chake zilizofanyika katika jiji la Kinshasa.

Katika sherehe hizo ilitamkwa kwamba serikali itaendelea kuwaenzi wasanii wote na kuahidi kujenga minara ya nguli wengine waliotangulia mbele za haki.Wasifu wa Franco:

Wasifu wa gwiji hilo unaeleza kuwa alizaliwa Julai 06, 1938, katika kijiji cha Sona Bata Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.


Baba yake Joseph Emogo alikuwa mfanyakazi wa shirika la reli wakati mama yake alikuwa mama wa nyumbani akioka mikate na kuuza sokoni.

Wakati akiwa bado mdogo wazazi wake walihamia katika jiji la Kinshasa.

Franco akiwa na umri mdogo alitengeneza gitaa la kienyeji ambalo alilitumia kupiga na kuwavutia wateja pembeni mwa mama yake wakati akiuza mikate.

Kipaji chake kiligunduliwa na mpiga gitaa Paul Ebengo Dewayon, ambaye alijitolea kumfunza Franco jinsi ya kupiga vyema ala hiyo.

Mwaka 1950, wakati huo akiwa na umri wa miaka 12, alitengeneza jina akiwa katika bendi ya Watam ya Dewayon ambaye alikuwa kiongozi wa bendi hiyo.

Miaka mitatu baadae Franco alirekodi  wimbo wake wa kwanza uliokuwa na jina la Bolingo na ngai na Beatrice. (mpenzi wangu Beatrice).

Baada ya kukubalika kuwa mmoja wa wana bendi ya Loningisa Studio, kiongozi wa bendi hiyo Henri Bowane alitoa nadhiri kwamba ataishi na Franco katika maisha yake yote yaliyosalia.

Chini ya Bowne, Franco akawa mpiga gitaa la solo, alikuwa akipigamtindo wa sebene.

Akaanza kutunga na kuimba yeye mwenyewe kwa mtindo wa rumba na za Kiafrika na hata za Kilatini.

Mwaka 1955 pamoja na kwamba alikuwa akipewa kazi nyingi katika studio, Franco aliunda bendi akiwa na Jean Serge Essous iliyokuwa ikipigia katika ukumbi wa baa ya OK.

Mwaka uliofuatia bendi hiyo ilibadilishwa jina na kuwa OK Jazz, baadae ikaitwa T.P.OK. Jazz kuenzi sehemu ilipoanzia bendi hiyo yaani katika baa yenye jila la OK (OK. Bar)

Katika kipindi cha mwaka mmoja bendi ya T.P.OK Jazz ikagundulika kwamba inataka kumpiku Vicky Longomba ambaye alikuwa katika bendi ya African Jazz, illiyokuwa ikiongozwa na Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ ambayo ndiyo ilikuwa bendi kubwa nchini humo.

Franco alishadai kwamba bendi yake ya T.P. OK Jazz ilitoa zaidi ya album 150 katika kipindi cha miaka 30. 


Kwa kuwa sheria haina umaarufu, mwaka 1958 Makiadi alifungwa kwa kosa la ajali ya barabarani.

Jamhuri  ya Kidemokrasia ya Kongo ina historia ndefu katika siasa na muziki. Katika makala haya imekudokezea kwa kifupi maswala mazima ya siasa na muziki yanavyouwiana kwa kiasia kikubwa.

Purukushani za Kisiasa katika nchi yake ya Kongo. Franco alilazimika kuhamia Ubelgiji kwa ajili ya kurekodi nyimbo zake.

Baada ya nchi kutulia ikiwa chini ya uongozi wa rais Mobutu Seseseko Kuku Ng’endu Wazabanga, ambaye alibadilisha jina la Kongo kuwa Zaire, Franco alirudi nchini mwake na kafanya tamasha kambambe la Festival OK. Jazz African Arts lililofanyika Kinshasa mwaka 1966.

Mobutu alitawala nchi hiyo tangu Novemba 25, 1966 hadi Mei 16, 1997.  Alitanguliwa na rais wa kwanza Joseph Kasavumbu, aliyekuwa rais tangu Julai 01, 1960 hadi Novemba 24, 1965.

Mobutu Seseseko alipinduliwa na Laurent Kabila ambae aliitawala nchi hiyo tangu mei 17, 1997 hadi Januari 16, 2001 alipouawa. Baada ya kuawa Laurent Kabila, nchi ikaongozwa na mwanae Joseph Desire Kabila, hadi alipomuachia kijiti rais aliyepo Tshisekedi.
    
Bendi ya OK. Jazz iliisaidia sana serikali ya Mobutu katika mambo ya kisiasa kupitia nyimbo zake zilizokuwa na mafunzo pamoja na ushawishi mwingi.

Franco katika tungo zake hakuona soni kusifia mazuri wala kuonya mabaya pamoja na kwamba aliwekwa lupango mara nyingi alipokiuka taratibu za nchi.

Mwaka 1970 Luambo alipata pigo kubwa kwa kufiwa na mdogo wake Bavon Marie Marie, ambae kifo chake kilitokana na ajali ya gari alipokuwa akiendesha kwa hasira baada ya kukorofishana na kaka yake Franco juu ya mwanamke wa mdogo wake.

Mwaka 1980 serikali ya Kongo (Zaire) ilimtunukia hadhi ya kuwa babu wa muziki wa DRC, kama heshima kwa juhudi zake za kufufua uchumi uliokuwa ukiyumba nchini humo.

Wakati wa maisha yake aliwahi kuongeza uzito ghafla na kufikia paundi 300 ambazo ni sawa na kilo 136.

Franco Luambo Makiadi alitokea kuwa tajiri sana katika kipindi cha utawala wa rais Mobutu Seseseko.

Mbali na urafiki ambao aliokuwanao na rais huyo, ilifikia wakati fulani serekali ikazipiga marufuku baadhi ya nyimbo zake zilizo kuwa na ujumbe uliokiuka maadili ya umma.

Kutokana na sababu mbali mbali, serikali ya Mobutu ilikuwa makini sana na wanamuziki wake. Kulikuwa watu maalumu wakifanya kazi za kuwazichunguza kila wimbo kubaini ujumbe uliomo.


Sifa kubwa ya Franco ni kwamba takriban nyimbo zake zote zilikuwa ni zenye mafunzo kwa jamii, aidha hakusita kukemea hata serikali yake ilipofanya sivyo ndivyo.

Franco Makiadi kuna kipindi alishutumiwa kuimba nyimbo ambazo zilikuwa zikiigusa serikali ya Mobutu, ambapo ilimfungulia mashitaka akawekwa jela.

Baadae Luambo akiwa na kundi lake wakavuka mto Kongo unaotenganzisha nchi hizo mbili za Kongo Brazzaville na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC), kwenda kujihifadhi kwa muda katika jiji la Brazzaville.

Akiwa jijini humo, rais Mobutu alimtumia wajumbe kwa ajili ya kumshawishi arudi Kinshasa, akiahidiwa kuwa maisha yake yasingelikuwa hatarini.

Bila kinyongo Franco aliupokea wito huo japo alikuwa ni mwenye kusita, mwishowe akaamua kurudi kama alivyoombwa na kiongozi wake wa nchi.

Pasipo katarajia Franco alipokanyaga ardhi ya  Kinshasa, kajikuta yuko matatani tena, akikaribishwa na kikosi cha wanajeshi.

Wakamuamuru yeye na kundi lake kupanda kwenya gari lao, akapelekwa hadi jela ya Ndolo.

Huko walikaa kwa muda wa siku mbili, yasemekana walicharazwa bakora za kutosha.

Baada ya kutolewa kwenye jela ya  hiyo,  Franco na kundi lake, wakahamishwa kwenye kambi ya jeshi  ya Tshatshi ambako walishikiliwa kwa siku kadhaa.

Ndipo ikatokea siku ambayo rais Mobutu alikwenda mwenyewe kujadiliana na Luambo Makiadi.

Alimtamkia maneno haya: “ kuanzia leo hii hadi itakapo fikia wakati wa mimi kuondoka madarakani, utakuwa ukiniimbia ukunisifia mimi, unatakiwa kunifanyia kazi zangu zote, tena kwa wakati wowote nitakapo kuhitaji…”

Kuanzia siku hiyo Franco akawa kiungo kikuu hususani katika Kampeni zote za rais.

Kwa ushirikiano huo, Franco alinufaika sana kuwazidi wanamuziki wengine wote wa nchi hiyo katika kipindi hicho cha utawala wa serekali ya Mobutu Seseseko Kuku Ng’wendu Wazabanga.

Mwaka 1978, Luambo akawekwa tena jela kutokana na utunzi wa nyimbo za Helein na Jackie.

Nyimbo hizo zilikuwa na maneno machafu yasiyo na maadili kwa umma. Sheria ikachukuliwa kuzipiga marufuku zisipitishwe kwenye radio na TV ya taifa.

Franco mwenyewe alijitetea akisema kuwa nyimbo hizo zilikuwa bado hazijaingia sokoni, bali zilikuwa zikiiandaliwa kwenye CD. Japo watu walikuwa wakizisikiliza wakati wa maonesho yao kwenye ukumbi wake wa 1.2.3 Kinshasa.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali kipindi hicho  Bwana Leon Kengo wa Dondo, alisimamia swala hilo akaamuru Franco awekwe jela.

Alipelekwa kwenye jela ya Luzubu, iliyopo mkoa wa Bas Kongo, ambao ndiko alikozaliwa Franco.

Akiwa jela, Makiadi akawa ni mwenye masikitiko, akijiuliza kisa cha rais Mobutu kushindwa kumsaidia. Msongo huo wa mawazo ulipelekea kuathirika na ugonjwa wa Hemorrhoid, uliomsumbua sana.

Miaka michache baadae, palitokea na mabadiliko kwenye baraza la mawaziri, ambapo mwanasheria mkuu wa serikali Leon Kengo wa Dondo, alienguliwa wadhifa huo, na akapelekwa kuwa balozi nchini Ubelgiji.

Franco baada ya kuskia hivyo, furaha ilimjaa na bila kukawia akamtungia wimbo  “Tailleur”, wenye tafsiri ya “Utabiri wangu umetokea kuwa kweli, mdomo wangu kama mganga wa jadi”

Luambo baadae mwaka 1985, alifyatua wimbo mkali uliotikisa nchi, uliopewa jina la ‘Mario’.

Lakini mwaka 1987 fununu zikaanza kuzagaa kwamba Franco yu mgonjwa.

Wimbo aliotengeneza mwaka huo kabla ya kifo chake ulikuwa wa ‘Attention na SIDA ’(jihadhari kwa ukimwi/ aids)

Mwaka huu Oktoba 12, itatimia miongo mitatu tangu aiage dunia.

Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi, Amina,

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad