HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 29, 2019

DKT. MPANGO AAGIZA KUTOTUMIA FUNGU LA LISHE KWA MATUMIZI MENGINE

Serikali imeziagiza Wizara, Mikoa na Halmashauri zote nchini kutumia fungu lililotengwa kwa ajili ya lishe  kwa matumizi yaliyopangwa  ili kuhakikisha watanzania wanaimarika kiafya na kushiriki kikamilifu katika Shughuli za Maendeleo.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango wakati wa Mkutano kati yake na Mwana wa Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya Lishe Dunia, Sarah Zeid na Mwakilishi wa Shirika  la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) nchini Tanzania, Michael Dunford, Jijini Dodoma.
Dkt. Mpango alisema kuwa iwapo eneo la lishe halitasimamiwa kikamilifu Taifa litazalisha watoto wenye udumavu wa ubongo na kusababisha kupungua kwa uwezo wa kufikiri na utendaji hafifu wakiwa katika shughuli mbalimbali.
Alisema ipo mikoa ambayo inazalisha mazao mengi  kama Mbeya na Njombe lakini inaidadi kubwa ya watoto wenye utapimulo, hivyo ni jukumu la kila mtanzania kuhakikisha anaangalia ni chakula gani kinahitajika kwa ajili ya watoto na wakinamama wajawazito ili kupunguza suala la ukosefu wa lishe.
Aidha amempongeza Mwana wa Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid, kwa kupambana na vifo vya wakina mama wajawazito na watoto kote Duniani, kwa kuwa mchango wa wanawake ni mkubwa sana katika Sekta za maendeleo kama Kilimo ikizingatiwa kuwa, kwa upande wa Tanzania wanawake ni takribani asilimia 51 ya watanzania wote hivyo kuwa na umuhimu wa kutunza raslimali hiyo kwa manufaa ya kizazi hiki na kijacho.
Kwa upande wake Mwana wa Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake katika kupambana na utapiamlo unaosababishwa na ukosefu wa lishe na amewataka watanzania kuhakikisha suala la Lishe linapewa kipaumbele  na kila mmoja kwa manufaa ya Taifa na Dunia kwa ujumla.
Naye Mwakilishi wa WFP nchini Tanzania Michael Dunford, amesema dhumuni la Mwana wa Mfalme kuitembelea Tanzania ni kujifunza na kuhakikisha WFP inafanya kazi kwa Karibu na Serikali kwa lengo la kuwasaidia wananchi kupata Lishe bora kwa kuwa Shirika hilo lina uwezo na lipo tayari  kutoa misaada hiyo kwa Tanzania. 
 Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akieleza jitihada za Serikali katika kupambana na utapiamlo ikiwa ni pamoja na  kila Mkoa kuandaa bajeti ya Lishe  wakati wa Mkutano kati yake na Mwana wa Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya Lishe Dunia, Sarah Zeid (hayupo pichani), Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Khatib Kazungu na kulia ni Kamishana msaidizi wa Bajeti wa Wizara hiyo Charles Mwamwaja. 
 Mwana wa Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya Lishe Dunia, Sarah Zeid, akieleza anavyofurahishwa na Serikali ya Tanzania inavyosimamia suala la Lishe, wakati wa Mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), kushoto ni Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani- WFP nchini Tanzania, Michael Dunford.
 Mwakilishi wa Shirika  la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) Michael Dunford, akieleza utayari wa Shirika hilo kuisaidia Tanzania katika masuala ya Lishe, wakati wa Mkutano kati ya Mwana wa Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid (kushoto) na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
 Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kulia), na Ujumbe wa Shirika  la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), ukiongozwa na Mwana wa Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya Lishe Dunia, Sarah Zeid (wa pili kulia) katika mkutano kuhusu Lishe uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango  Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akipeana mkono na Mwana wa Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya Lishe Dunia, Sarah Zeid (kushoto), baada ya kumalizika mkutano kuhusu Lishe uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Mwana wa Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya Lishe Dunia, Sarah Zeid (kushoto), wakifurahia jambo katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Tanzania na Shirika la Chakula Duniani- WFP, baada ya kumalizika mkutano kuhusu Lishe uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
(Picha na Peter Haule, Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad