HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 1, 2019

Bodi ya Wadhamini ya Taasisi JKCI yaridhishwa na huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi hiyo

Kuongezeka wa idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa vipimo na uzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo ambayo imeziba kupitia  mtambo wa Cathlab ni ishara kuwa watu wengi wanahitaji kupata huduma hiyo.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akisoma ripoti ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba hadi Desemba kwa bodi ya Wadhamini.

Prof. Janabi alisema tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo mwaka 2016 hadi 2018 katika mtambo wa Cathlab wameona zaidi  ya wagonjwa 2389 ambao waliwafanyiwa vipimo na kuwazibua  mishipa ya damu ya moyo iliyokuwa  imeziba.

“Kupitia mtambo huu tunafanya upasuaji wa moyo wa  bila kufungua kifua kupitia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja.  Kwa mwaka jana pekee tulifanya upasuaji kwa wagonjwa 1056 na kuvunja rekodi katika nchi za Afrika Mashariki na Kati”, alisema Prof. Janabi.

Alisema hivi sasa madaktari wa magonjwa ya moyo kwa watoto kupitia mtambo huo wa Cathlab  wameanza  kuziba matundu na kuzibua mishipa ya damu iliyoziba.

“Kipindi cha nyuma watoto walikuwa wanafanyiwa upasuaji huu na madaktari wageni hii ilitokana na kutokuwa na daktari wa kutoa huduma hiyo katika Taasisi yetu. Mwaka jana daktari wetu mmoja aliyekuwa anasoma Afrika ya Kusini amerudi baada ya kumaliza masomo yake na anafanya upasuaji siku ya Jumatano”,.

“Tumetenga siku moja kwa wiki ambayo ni jumatano watoto wanafanyiwa upasuaji wa kuziba matundu na kuzibua mishipa ya damu iliyoziba, uhitaji ni mkubwa na mtambo uliopo ni mmoja. Kuna haja ya kuwa na mtambo mwingine wa Cathlab ili wagonjwa wengi wenye uhitaji wa huduma hii waweze kuipata”, alisema Prof. Janabi.

Katika hatua nyingine Prof. Janabi alisema mwezi wa sita mwaka huu Madaktari Afrika kutoka nchini Marekani watakuja nchini kupanda  mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuchangia fedha za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Prof. William Mahalu aliipongeza menejimenti na wafanyakazi wote wa Taasisi hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutoa huduma ya matibabu ya magonjwa ya moyo.

Prof. Mahalu ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa  moyo na mishipa ya damu alisema kufanya vizuri kwa mtambo wa Cathlab kunaonesha kuwa watu wengi  wanahitaji huduma hiyo na wao  kama bodi wameona  kunahaja ya kuongeza mtambo wa pili wa Cathlab ili wagonjwa wengi wapate huduma hiyo.

“Mmetuambia hivi karibuni mmesaini mkataba wa makubaliano ya  kuletwa kwa wagonjwa kutoka nchi ya Malawi na Visiwa vya Zanzibar kwa ajili ya matibabu, hongereni sana. Endeleeni kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili watu wengi zaidi wafaidike na huduma mnayoitoa”, alisema Prof. Mahalu.

Alisema miaka minne au mitano ijayo wataalamu kutoka nje ya nchi  wanaokuja  kufanya kambi maalum za matibabu ya moyo watakuja nchini kujifunza  kutoka kwa watanzania  baada ya wao kuja kutoa msaada.

Prof. Mahalu alimalizia kwa kuwataka wataalamu wa magonjwa ya moyo kufuatilia maendeleo ya  wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo pindi wanaporuhusiwa kurudi nyumbani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu akizungumza jambo na wafanyakazi wa maabara alipotembelea maabara hiyo kwa ajili ya kuangalia mashine mpya za uchunguzi wa vipimo vya magonjwa ya moyo zilizofungwa. Watatu kulia kutoka kwa Prof. Mahalu ni mjumbe wa bodi Dkt. Donan Mbando.
Watoto wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa wanacheza gemu kama walivyokutwa  na mpiga picha wetu. Watoto wawili kati yao wamefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua  na wawili wanasubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu na mjumbe wa bodi hiyo Dkt. Donan Mbando wakitoka kuangalia wodi mpya ya watoto wenye magonjwa ya moyo ambayo imejengwa na kufanyiwa ukarabati.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu na mjumbe wa bodi hiyo Dkt. Donan Mbando wakiangalia chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU) kilichopo katika wodi  mpya ya watoto wenye magonjwa ya moyo ambayo imejengwa na kufanyiwa ukarabati. Chumba hicho kikianza kufanya kazi kitakuwa na vitanda nane na kuweza kurahisisha kutoa huduma kwa watoto wanaohitaji matibabu  ya dharula.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu akiangalia (medical gas bed head panel) mahali pa kuchomeka mashine ya kutolewa hewa ya matibabu  kwenda kwa mgonjwa  katika wodi mpya ya kulipia ya watoto wenye magonjwa ya moyo ambayo imejengwa na kufanyiwa ukarabati. 
Picha na JKCI

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad