HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 12, 2019

BALOZI MAHIGA AWASILI WIZARANI NA KUKABIDHIWA RASMI OFISI


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amewasili makao makuu ya Wizara jijini Dodoma na kukabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi. Kitendo hicho kinafuatia kubadilishana wizara baina ya mawaziri hao kufuatia mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Mhe. Rais DKt. John Pombe Magufuli Machi tatu mwaka huu.
Akikabidhi ofisi Prof. Kabudi amewashukuru watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi alichofanya nao kazi na kuwasihi kuendelea kumpa ushirikiano kama huo Balozi Dkt. Mahiga kwani anaamini yale aliyoyaanzisha yataendelezwa na Waziri huyo kwa nguvu zote.
Prof. Kabudi amesema katika kipindi chake cha uongozi Wizarani  amebadilisha  muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali nakutoa ofisi mpya tatu za Mwanasheria Mkuu wa Serikal, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na ana imani kuwa mabadiliko hayo yatatekelezwa kikamilifu chini ya uongozi wa mjenzi mahiri Dkt. Augustine Mahiga.
“Mlinipa ushirikiano mkubwa katika kipindi change, niwasihi muendelee hivyo kwani kwa kushirikiana nanyi tulifanikiwa kubadilisha  muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hivyo kutoa ofisi mpya tatu za Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, natumai kuwa utekelezaji wa majukumu yaliyo mbele yao utakuwa kamilifu chini ya Mhe. Balozi Dkt. Mahiga ambaye ni mjenzi Mahiri kama mtashirikiana vyema,” alisema Prof. Kabudi.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa Ofisi Mhe. Balozi Dkt. Mahiga amesema amepokea jukumu hilo kwa mikono miwili na amewashukuru watumishi wa Wizara hiyo kwa mapokezi waliompatia na kuahidi kushirikiana na watumishi wote katika kazi zao na hivyo kuendeleza yale yote ambayo Prof. Kabudi ameyaacha kwa ajili ya kuiletea nchi maendeleo kupitia sekta ya Sheria nchini.
“Niwashukuru kwa mapokezi yenu leo hii, nimefarijika kuwa nanyi hapa siku hii kama ambavyo Mhe. Rais alisema siku naapishwa kuwa nisiwe na shaka nimezungukwa na wanasheria mahiri,  niwaahidi kuwa tutashirikiana katika kazi zote ili tuendeleze yale yote ambayo mwanafunzi wangu Prof. Kabudi ameishia,” alisema Balozi Dkt. Mahiga
Awali mawaziri hao walikabidhiana majengo ya ofisi zao yaliyoko katika Mji wa Serikali Mtumba na baadaye kuja zilizoko Ofisi za Wizara zilizoko Chuo Kikuu cha Dodoma- UDOM ambako walikabidhiana taarifa mbalimbali za Wizara na kuzungumza na watumishi.
Makabidhiano hayo yamehudhuriwa na katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria prof. Sifuni Mchome, Naibu Katibu Mkuu Bw. Amon Mpanju, Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga na watendaji wengine wa Wizara na taasisi zake waliopo Jijini Dodoma.
 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (watatu kulia) katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (wanne kulia)  baada ya kutembelea jengo la Wizara ya Katiba na Sheria lililoko katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ambako pia alitumia nafasi hiyo kumkabaidhi jengo hilo kama asehemu ya makabidhiano ya Wizara baina ya Mawaziri hao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akitia saini kitabu wa cha wageni baada ya kukagua jengo la Wizara ya Katiba na Sheria na kulikabidhi jengo hilo kwa Waziri wa sasa wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (mwenye tai ya Bluu) anayeongea na Katibu Mkuu Prof. Sifuni Mchome. Jengo hilo liko katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea shada la maua kutoka kwa mtumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi Agnela Chang’a baada ya kuwasili katika ofisi za Wizara jijini Dodoma tangu apishwe kushika nafasi hiyo , huku aliyekuwa Waziri Mhe, Prof. Kabudi  na Katibu Mkuu Prof. Mchome wakiangalia.

 Waziri wa Katiba na Sheria mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiambatana na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  mhe. Prof.Palamagamba Kabudi (nyuma yake) wakisalimiana na watumishi wa Wizara baada ya kuwasili makao makuu ya Wizara UDOM kwa ajili ya kukabidhiana Ofisi baina ya Mawaziri hao kufuatia mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Mhe. Rais hivi karibuni.
 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akishikana mkono na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga baada ya kumkabidhi ofisi rasmi baada ya kubadilishana wizara hizo kufuatia mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa hivi karibuni na Mhe. Rais. Makabidhiano hayo yamefanyika makao maku ya Wizara yaliyo katika Chuo Kikuu cha Dodoma- UDOM
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea nyaraka kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi   wakati alipomkabidhi rasmi ofisi baada ya kubadilishana wizara hizo kufuatia mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa hivi karibuni na Mhe. Rais. Makabidhiano hayo yamefanyika makao maku ya Wizara yaliyo katika Chuo Kikuu cha Dodoma- UDOM- jijini Dodoma, wakiangalia kushoto kwa prof Kabudi ni Naibu Katibu Mkuu Bw. Amon Mpanju na kulia ni Katibu Mkuu Prof. Sifuni Mchome na Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga na watumishi wengine wa Wizara 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad