HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 19 March 2019

BAGAMOYO YANUFAIKA NA MRADI WA MAJI KATIKA KUHIMILI MABADILIKO YA TABIANCHI


Serikali imesema itahakikisha kuwa inaandaa miradi mbalimbali ili kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi hapa Nchini. Rai hiyo imetolewa  na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kutembelea moja ya Mradi wa Visima na Miundombinu ya kuvuna maji ya mvua katika Wilaya ya Bagamoyo inayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Naibu Waziri Sima amesema kuwa Mradi huo umelenga hasa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi zitokanazo na maji ya bahari kuchangamana na maji ya visima. “Katika maeneo haya mradi umechimba visima kumi (10) na kuvijengea matanki ya lita 15,000 kwa lengo la kuwapatia maji safi  wakazi wa maeneo haya ambao visima vyao vya zamani vimeathiriwa na maji ya chumvi”.  Sima alisisitiza.

Aidha mradi huu umejenga miundombinu ya kuvuna maji ya mvua katika shule za Sekondari za Kingani na Matipwili zote za Wilayani Bagamoyo ambapo kwa kila shule takriban lita 147,000 hukusanywa katika matanki na huhudumia takriban wanafunzi 800. 

Mradi huu tofauti na miradi mingine ya maji umelenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi zinazosababisha watu kulazimika kutumia maji ya chumvi kutokana na visima vingi vya awali kuingia maji ya chumvi hali inayosababishwa na kuongezeka kwa ujazo wa bahari. “Lengo hasa ni kuwapatia vyanzo mbadala vya maji ikiwa ni hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo haya” Sima alisisitiza.

Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Suleiman Murad Sadick ameipongeza Serikali kwa kutekeleza mradi huo na kuishauri Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kupitia kamati ya Maji kuhakikisha kuwa wanalinda miundombinu ya mradi huo ili uweze kunufaisha wakazi wengi zaidi na kuangalia namna bora ya uendashaji wa mradi huo ili kuwapunguzia gharama wananchi.

“Hakikisheni kuwa miradi hii inakuwa endelevu, kamati ya maji angalieni namna bora ya uendeshaji wa mradi huu, kiwango cha Shilingi 50 kwa ndoo bado ni kikubwa, kaeni mje na namna bora zaidi ili kuwaondolea wananchi hawa kero na tozo ya maji” Alisisitiza Mhe. Sadick

Mradi huu wa Kujenga Uwezo wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi ambao umeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kupata fedha takriban dola milioni 3.3 kutoka Mfuko wa Nchi Maskini Duniani chini ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi ulitanguliwa na tathmini ya hali ya maji ya ardhini kwa lengo la kuainisha maeneo ambayo hayajaathirika na  maji ya chumvi kutoka baharini. 
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge wa Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Suleiman Murad Sadick (wa tatu kutoka kulia) akipata maelezo kutoka kwa Bw. Luise Lugata Mtaalamu Mwelekezi kutoka Kampuni ya WEMA Contractors juu ya hali ya uchimbaji wa visima katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. Wengine pichani, ni sehemu wa waheshimiwa wabunge, wajumbe wa Kamati hiyo na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mussa Sima.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge wa Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Suleiman Murad Sadick (aliyesimama) akiongea na walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kingani katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. Kingani ni miongoni mwa shule zilizonufaika na mradi wa kuchimba visima na kujenga miundombinu ya kuvunaji maji ya mvua chini ya Mradi wa kuhimili mabadiliko ya Tabianchi katika Ukanda wa Pwani unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima akimtwisha ndoo ya maji Bi Kulwa Mohamed mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kufanya ziara ya kikazi ya kukagua mradi wa uchimbaji wa visima na uvunaji wa maji ya mvua katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo katika eneo la Magomeni ikiwa ni  njia mojawapo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi katika maeneo ya Pwani.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad