HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 13 February 2019

ZAIDI YA MILIONI 200 ZILIZOTOLEWA NA SERIKALI ZAWARUDISHA SHULENI WANAFUZI 1701 WA KIDATO CHA KWANZA MKURANGA

 Na Leandra Gabriel, Blogu ya Jamii
 NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega amefanikiwa kumaliza changamoto katika sekta ya elimu iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa Wilaya ya mkuranga kwa kipindi kirefu hasa kwa watoto walifaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kushindwa kuripoti kutokana na ukosefu wa madarasa.
Akizungumza na wananchi  wa Mkuranga wakati alipokuwa akikagua  shule 3 za sekondari zilizojengwa kwa nguvu ya wananchi kwa kushirikiana na serikali katika kata za Njia nne, Mwandege na kata ya Tambani, Ulega amesema kuwa serikali ya awamu ya Tano imetoa zaidi ya milioni 200 ili kumalizia shule hizo ili wanafunzi waweze kuanza masomo mara moja.
Amesema kuwa awali palikuwa na changamoto kubwa na hivyo kupelekea wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka jana kukosa shule ya sekondari huku wakiwa na ufaulu wa hali ya juu, amezitaja shule zilizopata msaada huo kutoka kwa serikali ni pamoja na Mwandege, Njia nne na  shule iliyopewa jina lake la Abdala Ulega sekondari.
“Wazazi wenzangu mnatakiwa kuwasimamia watoto wetu waweze kuwa katika maadili mema ili kuwa mfano wa kuigwa nchini kwani itafikia hatua mimi nitastaafu hivyo lazima tuwe na wasomi wengi katika wilaya yetu ya mkuranga na hiyo yote elimu ndio msingi mkubwa.” amesema Ulega.
Aidha Ulega ametoa mifuko 40 ya saruji,  zaidi ya milioni tatu kwa kila  shule ili kuhakikisha mwezi wa tatu wanafunzi hao wanaanza shule mara moja ili kutowaweka wanafunzi hao katika hatari nya kupata vishawishi vitakavyokatisha ndoto zao hasa mimba.
 Kwa upande wake Afisa elimu wa sekondari wa Wilaya hiyo  Benjamini Majoya amempongeza Naibu waziri  kwa jinsi anavyopambania elimu katika wilaya hiyo ili iweze kukua na hiyo ni kwa namna  anavyojitolea katika kuhakikisha miundombinu inakuwa rafiki kwa wanafunzi.
Akitoa taarifa za elimu wilaya humo Afisa elimu huyo amesema  kuwa mara baada ya Serikali kutoa kiasi cha pesa hicho kupitia kwa Naibu waziri Ulega shule hizo zitakamilika haraka na wanafunzi 1071 ambao bado hawajaanza shule wataanza  mara moja na  kumaliza changamoto kwa wanafunzi hao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Firbeto Sanga amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli imekuwa ni serikali ya utekelezaji kwa vitendo kuliko maneno hasa katika kuhakikisha sekta muhimu zinaangaliwa kwa makini Zaidi.
Aidha amempongeza Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega kwa jinsi anavyopambania kuipaisha wilaya hiyo katika masuala ya maendeleo mbalimbali hasa miundombinu ya barabara, shule, hospitali mengine mengi.
 Naibu Waziri Mifugo na Vuvi (MB) wa Mkurangara , Abdallah Ulega akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua ujenzi wa madarasa katika kata Njianne, Mwandege na Tambani, leo Wilayani Mkuranga.(Picha zote na Emmanuel Massaka,MMG)
 Naibu Waziri Mifugo na Vuvi (MB) wa Mkurangara, Abdallah Ulega akikagua madarasa yaliyojengwa na wananchi pamoja na Serikali huku ikitegemewa Machi mwaka huu yataanza kutumika kwa wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza, leo Wilayani Mkuranga.
Afisa Elimu wa Sekondari wilaya ya Mkuranga,Benjamini Majoya akiwahakikishia wazazi na walezi wa wilezi shule hizo zitafunguliawa mwezi wa tatu mwaka huu,(Picha na Emmanuel Massaka,MMG)
Muonekano wa Madarasa ya shule hizo ambazo ni; Shule ya Sekondari iliyopewa jina la mbunge huyo Abdallah Ulega, Tambani na Njia nne.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad