HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 14, 2019

WAZIRI KAIRUKI: SERIKALI KUENDELEA KUJENGA MAZINGIRA WEZESHI NA ENDELEVU KATIKA SEKTA YA KILIMO

Serikali imedhamiria kuendelea kujenga mazingira wezeshi na endelevu katika Sekta ya Kilimo kupitia sera imara na zenye kutekelezeka.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mhe.Angellah Kairuki wakati akifungua Kongamano la Tano la Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuhusu Sera Jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa tarehe 13Februari, 2019.

Waziri alieleza kuwa, dhamira ya Serikali inaenda sambamba na mchango wa sekta ya Kilimo katika uzalishaji pamoja na ukuaji wa uchumi nchini kwa kuzingatia namna sekta hiyo inavyochangia katika maeneo mengi ikiwemo,utoaji wa ajira kwa wananchi waliowengi.

“Ni mambo ambayo yanajieleza yenyewe na kila mmoja wetu anayajua vizuri.  Asilimia 65.5 ya Watanzania wanategemea ajira na maisha yao kwenye kilimo, pia kinachangia asilimia 95 ya mahitaji ya chakula nchini na asilimia 65 ya mali ghafi ya viwanda vyetu,”alisema Kairuki

Aidha aliongezea kuwa, asilimia 30 ya fedha za kigeni hutokana na mauzo ya nje ya mazao na bidhaa za kilimo na huchangia asilimia 25 kwenye pato la Taifa.

Sambamba na hilo waziri alieleza kuwa jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano tangu imeingia madarakani imeendelea kutambua umuhimu wa kilimo katika kuongeza tija maeneo ya uzalishaji na mna haja ya kuleta msukumo zaidi katika kukiendeleza.

Pamoja na jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta hiyo, Waziri alibainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo na sehemu kubwa ya kilimo kutegemea jembe la mkono, matumizi madogo ya mbegu bora zinazotoa mazao mengi na kuhimili maradhi na athari za kimazingira, matumizi ya maji ni kidogo mno pamoja na kilimo kutegemea mvua  bila kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji chenye uhakika.

“Tunategemea mno mvua ya Mwenyezi Mungu hatujatumia vya kutosha maji aliyotuwekea juu ya ardhi na chini ya ardhi kwa kilimo katika hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo nchini hekta milioni 29 zinafaa kwa kilimo cha kumwagilia lakini ni asilimia 1 tu ya ardhi hiyo inamwagiliwa. Tumejipa lengo la kuongeza kilimo kinachomwagiliwa nchini,”alisisitiza Kairuki

Kairuki alihamasha wakulima kuendelea kutumia mbolea kutokana na Tanzania kutumia wastani wa kilo19 kwa hekta kiwango ambacho ni kidogo kulinganisha kiwango cha takribani kilo 50 kwa hekta kinachotumiwa na Jumuiya na Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kwa upande wake Naibu Waziri Kilimo, Mhe.Omari Mgumba alieleza jitihada za serikali kuendelea kuhakiki madai ya madeni yenye ukakasi ya Wakala wa pembejeo wanaosambaza mbegu na mbolea wanaoidai serikali kiasi cha shilingi bilioni 35.

“kama mnavyofahamu mwaka ukipita wa fedha madeni yanahamia Wizara ya Fedha kwa hatua zingine ikiwemo kuyachunguza na kujiridhisha ambapo hadi sasa yamebainika kuwa na ukakasi katika takwimu na tofauti ya taarifa na Serikali inaendelea kufuatilia hujuma zilizofanyika ili kujiridhisha,”alisisitiza Mgumba.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Chuo cha Kilimo cha Sokoine ,Jackline Mkindi alipongeza uwepo wa kongamano hilo ambalo litatoa fursa za kujadili na kueleza changamoto wanazokumbana nazo hususani upande wa usambazaji wa Pembejeo  nchini na madeni yaliyopo ambayo hadi sasa ni sh.bilioni 39.9 ambazo zinapaswa kulipwa na serikali.

“Tunaimba Serikali ishushe bei na kuendelea kulipa madai sahihi kwa wanao stahili pamoja na kutataua changamoto za wakulima kutofikia gharama za pembejeo na kuwasaidia kujikamua katika uzalishaji kwa kuwa na pembejeo bora na kwa wakati,”alisema Mkindi.

Kongamano limeandaliwa na Jukwaa la Uchambuzi wa Sera za kilimo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Sekta binafsi na za umma ili kuleta mageuzi katika sekta ya Kilimo na kuchangia katika ukuaji wa Viwanda na kuhudhuriwa na takribani zaidi ya washiriki 300 nchini.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki akihutubia washiriki wa Kongamano la Tano al Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi lililofanyika katika Ukumbi wa Hazina Dodoma Februari 13, 2019 kwa lengo la Kuchambua na Kujadili sera ili kuboresha maeneo ya kisera ya kilimo lililoratibiwa na Jukwaa la Watafiti na Wachambuzi wa Sera za kilimo kwa kushirikisha wadau mbalimbali nchini.
 Naibu Waziri Kilimo Mhe.Omari Mgumba akiwasilisha hotuba yake wakati wa kongamano hilo.
 Sehemu ya wajumbe walioshiriki kongamano hilo wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki linaloendelea Jijini Dodoma kwa siku tatu kuanzia tarehe 13 hadi 15 Februari, 2019.
 Sehemu ya wajumbe walioshiriki kongamano hilo wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki (hayupo pichani) linaloendelea Jijini Dodoma.
 Mratibu wa Jukwaa la Uchambuzi wa Sera za Kilimo Prof.David Nyange akiwasilisha mada wakati wa Kongamano hilo.
 Mwenyekiri TPSF Bw.Salum Shamte akieleza masuala yanayohusu sekta Binafsi wakati wa Kongamano hilo.
 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Joseph Kiraiya akizungumza jambo kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi hiyo anayeshughulikia Sera, Uratibu na Uwekezaji Bi.Dorothy Mwaluko wakati wa Kongamano hilo.
Mwenyekiti Mwenza wa Timu ya Wadau Bi.Michellle Cornize akichangia jambo wakati wa Kongamano hilo.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad