HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 12 February 2019

WANAFUNZI MANYARA NA SINGIDA WANUFAIKA NA SWASH

WANAFUNZI wa vilabu 1,700 vya afya na usafi mashuleni kwenye wilaya za Mbulu, Hanang Mkoani Manyara na Mkalama Mkoani Singida, wamenufaika na elimu ya afya waliyopatiwa kupitia kituo cha pembe nne za utamaduni Haydom (4CCP). 

Ofisa miradi wa kituo cha pembe nne za utamaduni Haydom (4CCP) Nelson Faustine aliyasema hayo wakati wa kongamano la wanachama wa klabu za afya na usafi mashuleni lililohusisha walimu na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. 

Faustine alisema wametoa mafunzo ya matumizi sahihi ya vyoo, vibuyu chirizi, kichanja, shimo la taka, usafi binafsi na namna ya kutibu maji. "Tumepanga kuongeza vifaa vya usafi, kuandaa majarida yanayohusiana na afya na kuhamasisha matumizi ya muongozo wa kitaifa wa maji, elimu ya afya na usafi wa mazingira mashuleni," alisema. 

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Horace Kolimba alisema aliagiza shule zote za halmashauri hiyo kuanzisha klabu za afya na usafi mashuleni. Kolimba alisema wametoa maagizo kwa watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha hadi Februari 28 shule zote ziwe na vyoo ili wanafunzi wavitumie wakiwa wanasoma. 

Ofisa miradi wa shirika la Norwegian Church Aid, Zachayo Makobero alisema mpango huo umekuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi wa klabu za afya na usafi mashuleni. Mwalimu wa shule ya msingi Mwengeza wilayani Mkalama mkoani Singida, Julieth Gara alisema elimu hiyo imewasaidia mno wanafunzi kutokana na kufanya usafi wa mazingira. 

Mwalimu Gara alisema awali kabla ya elimu hiyo wanafunzi walikuwa wanaugua magonjwa ya tumbo na kuharisha ila sasa hivi hawana tatizo hilo tena. Mwanafunzi wa kidato cha tano wa shule ya sekondari Dokta Olsen ya Haydom, Aisha Monyo alisema kupitia klabu za afya na usafi mashuleni, wamepata elimu ya usafi na mazingira mashuleni. 

Monyo alisema wanafunzi wamepokea elimu hiyo kwa kusafisha mazingira ya shule na vyoo pamoja na kunawa mikono pindi wanapotoka vyooni tofauti kabla ya kupata elimu hiyo. Ofisa habari wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama, Omary Mtamike alisema awali walikuwa na shule moja ya klabu ya afya na usafi mashuleni ila hivi sasa zipo shule 28.

Mtamike alisema kutokana na manufaa ya mradi huo wa Swash, wao kama halmashauri wamejipanga kuhakikisha wanaboresha zaidi kwa kuongeza shule nyingine za msingi na sekondari. 
 Ofisa miradi wa kituo cha pembe nne za utamaduni Haydom (4CCP) Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, Nelson Faustine akizungumza kwenye kongamano la klabu za afya na usafi mashuleni. 
 Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za Wilaya za Mbulu na Hanang' Mkoani Manyara na Mkalama Mkoani Singida wakiwa kwenye kongamano la klabu za afya na usafi mashuleni kwenye Mji mdogo wa Haydom Wilayani Mbulu. 
 Baadhi ya wadau wa elimu  wa Wilaya za Mbulu na Hanang' Mkoani Manyara wakiwa kwenye kongamano la klabu za afya na usafi mashuleni lililoandaliwa na kituo cha pembe nne za utamaduni Haydom, (4CCP). 
Mshauri mkuu wa miradi ya maji na afya kwa Norwegian Church Aid (NCA) Manfred Arlt akizungumza na wadau wa elimu kwenye kongamano la klabu za afya na usafi mashuleni lililoandaliwa na kituo cha pembe nne za utamaduni Haydom (4CCP).  

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad