HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 14 February 2019

RC Gambo aifagilia Benki ya CRDB kwa kuchangamkia Biashara ya fedha za kigeni Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo ameimwagia sifa Benki ya CRDB kwa kuwa wa kwanza kuchangamkia biashara ya ununuaji na uuzaji wa fedha za kigeni baada ya serikali kufungia baadhi ya maduka ya biashara hiyo jijini Arusha.  


Akizungumza katika hafla maalum iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa wateja wake wa mkoa wa Arusha, Bwana Gambo alisema kuwa kwa ubunifu na uharaka waliouonyesha katika kuchangamkia fursa hii, Benki ya CRDB inasapoti kwa vitendo juhudi za serikali katika kujenga uchumi endelevu na wenye kugusa sekta zote za uzalishaji.


“Kama mtakumbuka, serikali iliamua kuingilia kati suala la maduka ya kubadilishia fedha nchini, hususani hapa Arusha ili kubaini maduka yanayofanya biashara hizo kinyume na sheria na taratibu. Zoezi hilo lilipelekea kufungwa kwa baadhi ya maduka na hivyo kuleta upungufu kiasi kwa huduma za fedha za kigeni. Kitendo chenu cha kuamua kuweka dirisha maalum kwenye matawi yenu yote, ili yaweze kutoa huduma za uuzaji na ununuzi wa fedha za kigeni, umeonyesha kwa kiasi gani nyinyi ni wazelendo wenye nia njema ya kuona juhudi za serikali yetu ya awamu ya tano chini ya Rais wetu mpendwa John Pombe Magufuli inaleta maendeleo ya kweli kwa watanzania. Hongereni sana” alisema Mheshimiwa Gumbo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Ally Laay (kushoto) wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, wakati wa Semina ya siku moja kwa Wafanyabiashara na Wateja wa Benki ya CRDB, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru, Jijini Arusha leo. 

Kwa upande mwingine, mheshimiwa Gambo pia aliipa changamoto Benki ya CRDB kuangalia jinsi ya kuboresha huduma hiyo  kwa kuongeza muda wa kutoa huduma katika matawi yake kwani watalii wengi huhitaji huduma ya kubadilisha fedha kwa mida ambayo matawi ya benki huwa yameshafungwa. Mkuu wa Mkoa pia aliishauri Benki ya CRDB iangalie jinsi ya kuwafikia wateja wenye mahitaji hayo kwa maeneo maalum ya utalii kama vile Mto wa Mbu na Karatu.

Kwa upande wa wafanyabishara wadogo maarufu kama wamachinga, Mheshimiwa Gambo aliitaka Benki ya CRDB kuendelea kuwa wabunifu na kuleta bidhaa kwa ajili ya kundi la wateja wadogo yaani wamachinga ambao wana mchango mkubwa katika uchumi wa taifa. Mheshimiwa Gambo alisema kuwa Serikali imeanza kwa kutoa vitambulisho kwa wajasiliamari ili kuwa rasimisha, hivyo Benki zinakujukumu la kwenda mbele zaidi kwa kuwapatia mikopo nafuu ili waweze kukuza baishara zao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela pamoja na Mkurugenzi wa Masoko Utafiti na Huduma kwa Wateja wa Benki hiyo, Tully Esther Mwambapa wakiangalia kipeperushi cha mmoja wa Wafanyabiashara wa Jiji la Arusha.

Akizungumza  katika semina hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Bwana Abdulmajid Nsekela alisema kuwa benki hiyo imejipanga vizuri kuweza kutoa huduma stahiki kwa wakazi wa mkoa wa Arusha na nchi nzima kwa ujumla. “Nichukue fursa hii kuwahakikishia wakazi wa mkoa wa Arusha kuwa matawi yetu saba yalipo mkoani humu yako tayari kwa ajili yenu. Huduma zetu zina kidhi mahitaji ya makundi yote ya jamii kuanzia watoto, wakubwa, kinamama, wafanyabishara wadogo, wakati na wakubwa. Pia tunafanya biashara za Bima na kukusanya malipo yote ya serikali kuanzia malipo ya ankara, kodi na mengineyo. Pia Benki inawahudumia wateja wadogowadogo kupitia  kitengo chake cha wajasiliamari yaani CRDB Bank Microfinace” alisema  Nsekela.

Semina ya Benki ya CRDB kwa wafanyabishara wa mkoa wa Arusha iliyofanyika katika hoteli ya Mount Meru jijini hapa, imeandaliwa na Benki ya CRDB ikiwa ni sehemu ya mipango mkakati wake wa kuwafikia wateja wake ilik kuwaainishia huduma mbalimbali zinazopatikana ndani ya benki ya CRDB zitakazoweza kuwanufaisha kibiashara na huku ikikusanya maoni yao juu ya njia bora zaidi za kuwahudumia. Mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo mada za mikopo, biashara ya fedha za kigeni, mikopo ya wajasiliamari na jinsi ya kuwa wakala wa benki ya CRDB.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya siku moja kwa Wafanyabiashara na Wateja wa Benki ya CRDB, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru, Jijini Arusha leo.

Benki ya CRDB ilianzishwa mwaka 1996 na imeendelea kukua zaidi hadi kufikia kuwa benki inayoaminika, chaguo la kwanza la mteja na kuongoza kwa ubanifu katika soko. Benki ya CRDB imekuwa ikirekodi ongezeko la faida kila mwaka tokea ilipoanzishwa na imekuwa ikilipa gawio kila mwaka kwa wanahisa wake. Benki ilipiga hatua muhimu hivi karibuni baada ya kuvuka mipaka ya Tanzania na kuanzisha kampuni tanzu ya CDRB Burundi.

Benki ya CRDB inatoa huduma mbalimbali kwa wateja wakubwa, wakati na wadogo kupitia matawi zaidi ya 250, Matawi yanayo tembea 13, Mashine za kutolea fedha zaidi ya 515, vifaa vya manunuzi (PoS) zaidi ya 1,000 na Mawakala wa FahariHuduma 2,558. Pia Benki ya CDRB inatoa huduma ya kibenki kupitia mtandao yaani “Internet banking” na huduma ya kibenki kupitia simu ya mkononi ijulikanayo kama “SimBanking”.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Ally Laay akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya siku moja kwa Wafanyabiashara na Wateja wa Benki ya CRDB, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru, Jijini Arusha leo. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya siku moja kwa Wafanyabiashara na Wateja wa Benki ya CRDB, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru, Jijini Arusha leo. 
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo akiongozana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Ally Laay (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, wakati wakiingia ukumbini tayari kwa ufunguzi wa Semina ya siku moja kwa Wafanyabiashara na Wateja wa Benki ya CRDB, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru, Jijini Arusha leo.No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad