HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 15, 2019

MBUNGE WA USHETU AKERWA NA VITENDO VYA UHALIFU JIMBONI KWAKE

Mbunge wa Jimbo la Ushetu, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amekemea vitendo vya kiuhalifu vinavyoendelea katika Halmashauri ya Ushetu ambavyo vimepelekea kusababisha majeruhi na vifo Halmashaurini hapo.

Amezungumza hayo katika kata ya Mpunze iliyopo katika Halmashauri hiyo ambapo kabla ya kuzungumza nao Mbunge huyo alipita katika kituo cha afya cha Ukune kwa ajili ya kuitizama na kuipa pole familia moja iliyoivamiwa usiku na kikundi cha watu kisichojulikana ambacho kiliwashambulia familia hiyo kwa kukatwa mapanga na kuwaibia fedha.

Mbunge Kwandikikwa, ameonesha kusikitishwa na matukio yanayoendelea katika kata hizo na kuwaahidi  wananchi wake kulisimamia suala hilo kikamilifu.

"Hatuwezi kukubali hali hii kwasababu wananchi wanaogopa kufanya biashara na wengine wanaogopa kuzalisha hivyo suala la ulinzi lipo mikononi mwetu wenyewe ni lazima jambo hili tuliondoe", amesisitiza Mbunge Kwandikwa.

Ameongeza kuwa atafanya juhudi za kuweka Kituo cha Polisi maeneo jirani ili kuweza kuongeza hali ya usalama kwa wananchi na iwe rahisi kwao kuripoti kituoni hapo matukio yote ya kiuhalifu pindi yanapotokea.

Aidha, Mheshimiwa Kwandikwa, amewataka wananchi kutoa taarifa kwake na kwa vyombo vya usalama kwa yeyote wanayemdhani anajihusisha na vitendo vya kijambazi katika maeneo yao ya wanamoishi.

"Hatutovumilia hali hii naomba viongozi wanaouhusika na ulinzi mjipange kisawasawa kwani hata mimi saa hii niko tayari kazini", amefafanua Mbunge huyo.

Katika hatua nyingine, Mbunge huyo amewaeleza wananchi wake baadhi ya miradi inayoendelea kufanyika katika kata hiyo na kata zingine za Halmashauri ya Ushetu na kusisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu na kujitoa katika shughuli za kimaendeleo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Sabasabini, Bw. Emmanuel Makashi, amemshukuru Mbunge huyo kwa kulisimiamia suala la usalama katika kata za jimbo lake kwani limekuwa kero ambapo naye ni miongoni mwa waathirika wa kuvamiwa.

Mbunge huyo yupo mkoani Shinyanga kukagua hatua zilizofikiwa katika miradi inayoendelea kutekelezwa kama vile ujenzi wa hospitali ya wilaya, jengo la halmshauri, na barabara zinazoendelea kujengwa kwa kiwango cha changarawe ya Nyamilangano-Butibu yenye urefu wa kilomita 12.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa, akizungumza na wananchi wa Kata ya Mpunze kuhusu kutoa ushirikiano wa namna ya kutokomeza matukio ya kiuhalifu yanayoendelea katika kata za jimbo hilo, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga. 
Mbunge wa Jimbo la Ushetu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa, akisalimia baadhi ya wagonjwa  waliofika katika Kituo cha Afya cha Ukune, wilayani Kahama, ambapo alienda kuwajulia hali wananchi waliovamiwa na majambazi na kukatwa mapanga na kuibiwa fedha, mkoani Shinyanga. 
Mbunge wa Jimbo la Ushetu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa, akimtwisha maji Bi. Monica Joseph, yaliyotokana na ujenzi wa kisima kikubwa katika kijiji cha Kayenze, kata ya Ukune, wilayani Kahama.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu, Dkt. Atanasi Lucas, akitoa maelezo ya mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya kwa Mbunge wa Jimbo la Ushetu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa, wakati alipokagua hatua za maendeleo ya mradi huo, mkoani Shinyanga. Ujenzi wa Hosptali hiyo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu na utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 1.5.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa, akisalimiana na mafundi wanaojenga jengo la ofisi za Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama.
Kazi za ujenzi zikiendelea katika jengo la ofisi la Halmashauri ya Ushetu, linalojengwa na mkandarasi wa Shirika la Mzinga kwa gharama ya shilingi zaidi ya  bilioni nne.
Muonekano wa majengo ya chumba cha kinamama wa wajawazito (Matenity), chumba cha upasuaji na mochwari lililokamilika kujengwa katika kijiji cha Ukune, wilayani Kahama. Ujenzi wa majengo hayo pia umehusisha maabara na nyumba ya mganga mkuu kwa gharama ya shilingi milioni 400.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad