HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 14 February 2019

MABULA AAGIZA WANANCHI KWIMBA KUPATIWA VIWANJA NDANI YA MIEZI MITATU

Na Munir Shemweta, KWIMBA
Naibu Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza kuwapatia viwanja ama fedha wananchi 44 waliotakiwa kupatiwa viwanja katika eneo la Ngungumalwa wilayani humo ndani ya miezi mitatu na wasipotekeleza waliohusika katika suala hilo watawajibishwa.

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo jana tarehe 13 Januari 2019 katika wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ulipaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi katika kanda ya Ziwa.

Aidha, ameitaka halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kufanya uchunguzi wa kiasi cha fedha takriban milioni 74 zilizotolewa na wananchi kwa ajili ya kupimiwa na kupatiwa viwanja eneo la Ngungumalwa ambazo hazikutumika kwa kazi hiyo ili kubaini zilitumika katika mazingira gani tofauti na malengo yaliyokusudiwa.

Dkt Mabula alisema iwapo wananchi hao hawatapatiwa viwanja ama kurudishiwa fedha zao ndani ya muda wa miezi mitatu aliotoa basi wote waliohusika kwa namna moja ama nyingine watawajibishwa ili kurudisha imani kwa wananchi.

‘’Kuchukua fedha za wananchi bila kupatiwa maeneo kunawafanya kukosa imani na serikali yao na mimi sitakubali kuona wananchi wakidhulumiwa haki yao na halmashauri ya Kwimba ina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapatiwa maeneo haraka iwezekanavyo’’ alisema Mabula.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kwimba Pendo Malabeja alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Mkazi kuwa halmashauri yake ilishaanza kuwalipa baadhi ya wananchi ingawa hakuainisha kiasi na idadi ya wananchi waliolipwa na kubainisha kuwa suala hilo bado linaendelea kufanyiwa kazi.

Vile vile, Dkt Mabula ameitaka halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kupanga na kupima maeneo yote ambayo yanakuwa kwa kasi na kuacha kujikita katika zoezi la uarasimishaji ambapo alifafanua kitendo cha kuacha kupanga na kupima maeneo yanayokuwa kwa kasi kutasabaisha ujenzi holela.

Aliongeza kuwa, Wilaya ya Kwimba iko nyuma sana katika kupima na kupanga maeneo jambo linaloifanya halmashauri hiyo kushindwa kujikusanyia mapato mengi kupitia sekta ya ardhi ambapo alitolea mfano wa jiji la Dodoma kuwa limekuwa likoongoza katika ukusanyaji mapato ya serikali ambapo mengi yanatokana na kupima na kuuza viwanja.

Ameitaka halmashauri hiyo kijipanga vizuri na kuitumia Ofisi ya Ardhi Kanda ya Ziwa pamoja na halmashauri jirani kama Misungwi kusaidia katika zoezi la kupima viwanja ili kuhakikisha linapanga na kupima maeneo mengi sambamba na kuwa na mji uliopangika huku ikijiongezea mapato.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Senyi Ngaga alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa wilaya yake ilikuwa nyuma katika masuala ya ardhi lakini sasa wamejiwekea mkakati maalum kuhakikisha inakuwa na maeneo mengi yalipangwa na kupimwa na suala la kwanza ni kuhakikisha idara ya ardhi inapatiwa fedha ya kutosha kwa nia ya kufanya kazi zake kwa ufanisi.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsikiliza Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Makwasa Biswalo (wa pili kulia) wakati alipofanya ziara katika halamashauri ya wilaya ya Kwimba kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Senyi Ngaga.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wakati alipofanya ziara katika halamashauri hiyo kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Wa tatu kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Senyi Ngaga na wa kwanza kulia ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Makwasa Biswalo na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kwimba Pendo Malabeja.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua majalada katika masijala ya ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wakati wakati alipofanya ziara katika halmashauri hiyo kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua moja ya majalada katika masijala ya ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wakati wakati alipofanya ziara katika halamashauri hiyo kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wakati wakati alipofanya ziara katika halamashauri ya wilaya ya Kwimba kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Senyi Ngaga.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad