HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 14 February 2019

Balozi Seif ashiriki mkutano wa Mbunge Shinyanga

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema Viongozi pamoja na Vijana wa CCM wakati Taifa wakati huu linakaribia kuingia katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hawana muda wa kujiingiza katika Siasa za Makundi ambazo zikiendekezwa zinaweza kupunguza nguvu za Chama hicho.

Alisema Katiba ya Chama imeweka wazi kwamba CCM lazima ishinde  wakati wa Uchaguzi na pale inapobainika kuwepo kwa Mwanachama au kiongozi wa CCM kakataa kumpigia kura Mwanachama mwenzake kwa sababu tu sio chaguo lake kwenye mchakato wa kura za Maoni, huo utaeleweka kuwa ni usaliti.

Balozi Seif  Ali Iddi alitoa kauli hiyo alipokaribishwa katika Mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mh. Steven Julius Masele alipokuwa akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha Miaka Mitatu zilizofanyika katika Uwanja wa Zimamoto Mjini Shinyanga.

Mkutano huo ulikwenda sambamba na maadhimisho ya Sherehe za Kutimia Miaka 42 tokea kuzaliwa kwa chama cha Mapinduzi uliojumuisha pia uwepo wa Viongozi na Wanachama wa CCM wa Majimbo pamoja na Wilaya nyengine zilizomo ndani ya Mkoa wa Shinyanga.

Balozi Seif ambae ni Mlezi wa Mkoa huo wa Shinyanga na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wana CCM  hao kwamba Chama kinahaki ya kumfukuza Uanachama Mwanachama ye yote mwenye hulka kama  hiyo inayofanana na yule mwenye tabia ya kuvaa sare ya kijani na manjano wakati wa mchana na kubadilika nyakati za usiku.

Ameupongeza ushirikiano wa pamoja wa Wabunge wote wa Majimbo ya Wilaya zilizomo ndani ya Mkoa wa Shinyanga kwa kazi kubwa wanazozifanya za kusimamia Utekelezaji wa Ilani ya CCM  ambazo zimekuwa zikishuhudiwa na Viongozi pamoja na Wananchi wa Majimbo yao.

Balozi Seif  akiwa Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga aliahidi kwa nafasi ya kipekee kumsaidia Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mh. Steven Julius Masele popote atakapokwama ili kumuongezea nguvu alizozielekeza kwenye Jimbo lake katika dhana nzima ya kuwatumikia Wananchi Wapiga kura wake.

Akizunguzungumzia suala la wahisani Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga alisema Taifa  lazima lifikie wakati kuwa na uwezo wake kamili wa kujitegemea ili kuwepuka misaada na Mikopo ya Wafadhili yenye muelekeo wa Masharti yasiyotekelezeka.

Balozi Seif alisema yapo masharti ya Mikopo na Misaada inayotolewa na baadhi ya Wafadhili ambayo mengine imekuwa ikishuhudiwa kulenga kwenda kinyume na Mila, Silka na Utamaduni wa Taifa.

Mapema akitoa Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Kipindi cha Miaka Mitatu iliyopita ndani ya Jimbo la Shinyanga Mjini, Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Steven Julius Masele alisema yale aliyoahidi katika kipindi cha Kampeni za Uchaguzi tayari ameshayatekeleza kwa asilimia kubwa.

Mh. Masele alisema miradi ya Jamii kama huduma za Afya pamoja na  Elimu katika Kata na vijiji mbali mbali vya Jimbo hilo imepata msukumo mkubwa kutokana na Wananchi wenye kujitolea katika kuianzisha kasi iliyomtia ari ka kuchangia nguvu za uwezeshaji.

Alisema ipo miradi ya Maendeleo ya kiuchumi kama bara bara imetekelezwa ndani ya kipindi cha Miaka Mitatu na kuwezesha kuwaondoshea usumbufu wa huduma za mawasiliano ya Usafiri Wananchi wake mbali na ile mikubwa inayotengewa Bajeti ya Serikali Kuu.

Mh.Masele alifafanua kwamba zaidi ya shilingi Milioni 36.3 zimetumika kuchangaia nguvu za  kuendeleza miradi ya Wananchi na kuahidi kusimamia kazi ya kuifanya Shinyanga mpya inayolengwa kuelekea katika  hadhi ya Mji wa Paris.

Mapema asubuhi mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga Balozi Seif Ali Iddi alipata fursa ya kulizindua Shina la Wakereketwa wa Umoja wa Vijana wa CCM la Japanes Coner  kwa kupandisha Bendera.

Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Bibi Haula Kachomba alisema Mashina kama hayo yalikuwa yamepotea na Chama cha Mapinduzi ngazi ya Mkoa kimeamua kuyafufua tena Mashina yake kwa kukumbuka kuwa ndio nguvu ya Chama.

Uzinduzi huo ulikwenda sambamba pia na Balozi Seif  kuwatembelea Wanashina la Wakereketwa wa CCM  Nambari Tatu la Mtaa wa Mkongo lililokamilisha safu ya Uongozi na kuwapongeza kwa uamuzi wao wa kujikusanya pamoja mbali ya kuimarisha chama lakini pia husaidia kuchangia ubunifu wa miradi ya kujikidhi Kiuchumi.

Baadae Balozi Seif  alishiriki kazi za ujenzi wa Taifa na kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa  Jeile la zamani lililovunjwa kutokana na kukosa ubora wa Majengo yanayopendekezwa na Chama.

Katika kuendeleza jengo hilo mbali ya Balozi Seif kuchangia Shilingi Milioni Moja lakini Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi alitoa wazo la kufanywa mchango wa papo kwa papo kwa waliohudhuria sherehe hizo za uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ofisi hiyo ya CCM.

Wazo la Mama Asha liliweza kuibua Mchango wa Shilingi Milioni 1,208,000/- Taslimu, ahadi ya fedha taslim shilingi Laki Tano, ahadi ya Saruji inayokadiriwa kufikia Paketi 180 kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge, Viongozi tofauti pamoja na Wananchi binafsi.
 Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kichama Balozi Seif Ali Iddi akipandisha Bendera kuashiria kulizindua Shina la Wakereketwa wa Umoja wa Vijana wa CCM la Japanese Kata ya Kambarage Mjini Shinyanga.
 Balozi Seif na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi wakijenga kuashirika kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Chama cha Mapinduzi ya Kata ya Kitangili Mjini Shinyanga.
 Mke wa Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kichama Mama Asha Suleiman Iddi akihamasisha Wana CCM Kuchangia ujenzi wa Ofisi ya Kata ya Kitangili Mjini Shinyanga uliopelekea kupatikana kwa Shilingi Milioni 1.2  na ahadi ya saruji Mifuko 180.
 Kikundi cha Wasanii cha Mabawa ndani ya Manispaa ya Shinyanga mjini kikitoa Burdani kwenye Mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mh. Steven Julius Masele wa uwasilishaji wa Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kipindi cha Miaka Mitatu.
 Balozi Seif akimpokea Mkereketwa wa Chama cha Demokrasia ya Maendeleo {CHADEMA} Nd. Singu aliyeamua kukihama chama hicho na kuomba kujiunga na CCM.
 Wanachama Wapya 347 wa CCM wa Jimbo la Shinyanga Mjini wakila kiapo cha uaminifu baada ya kukabidhiwa Kadi za Wanachama Wapya wa Chama hicho katikwa Uwanja wa Zimamoto Mjini Shinyanga.
Balozi Seif  akimlisha Keki Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Nd. Mabala Mlolwa kusherehekea Chama cha Mapinduzi kutimia Miaka 42 katika Uwanja wa Zimamoto Mjini Shinyanga. Wa Kwanza kutoka Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mheshimiwa Steven Julius Masele. Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad