HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 7, 2019

SIMANJIRO WAZINDUA UGAWAJI VITAMBULISHO

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Tumaini Magessa amezindua utoaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogowadogo kwa kuwataka wafanyabiashara wakubwa na wakati kutojihusisha na zoezi hilo.  Magessa aliyasema hayo mji mdogo wa Mirerani, wakati wa kugawa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo.

Magessa alisema wafanyabiashara waliosajiliwa kwenye mfumo wa mamlaka ya mapato nchini (TRA) hawapaswi kupatiwa vitambulisho hivyo. "Serikali ipo pamoja nanyi wafanyabiashara wadogo, ndiyo sababu Rais John Magufuli akawatambua na kuagiza vitambulisho vyenu vitengenezwe," alisema Magessa. 

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Yefred Myenzi alisema wafanyabiashara wanapaswa kuwa wazalendo kwa kulipa kodi ili kufanikisha maendeleo. "Kupitia kodi ndiyo serikali inafanikisha maendeleo mbalimbali ikiwemo kujenga vyumba vya madarasa yahoo shule za sekondari na msingi ambavyo watoto wetu watasoma," alisema  Myenzi. 

Ofisa wa mamlaka ya mapato nchini (TRA) Mji mdogo wa Mirerani, Castory Henry alisema wafanyabiashara wadogo wanaopaswa kupewa vitambulisho hivyo ni wale ambao mauzo yao hayazidi sh4 milioni kwa mwaka. Henry alisema kwa wale ambao wamesajiliwa na wapo kwenye mfumo wa TRA na mapato yao hajazidi sh4 milioni waandike barua kwao ili nao watambulike.

Mmoja kati ya wanufaika waliopata vitambulisho hivyo, Rudia Nalogwa alimshukuru Rais John Magufuli kwa kutambua jitihada za wafanyabiashara wadogo.  Nalogwa alisema yeye ni fundi cherehani hivyo anastahili kupata kitambukisho hicho kwa ajili ya kulipa kodi na kujipatia kipato. 

Katibu tawala wa wilaya ya Simanjiro, Zuwena Omary alisema zoezi hilo litafanyika kwa muda wa wiki mmoja.  "Wafanyabiashara wanaoona wana sifa za kupata vitambulisho hivyo wajiandikishe kwa maofisa watendaji wa kata ili wapatiwe," alisema Omary. 
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Yefred Myenzi akizungumzia umuhimu wa ulipaji kodi kwa wafanyabiashara wakati wa uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogowadogo wilayani humo.
 Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Zuwena Omary akielezea namna ya upatikanaji wa vitambulisho hivyo wakati wa uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogowadogo wilayani humo.
 Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Tumaini Magessa akielezea sifa za wafanyabiashara wadogo wanaopaswa kupata vitambulisho hivyo vilivyotolewa na Rais John Magufuli. 
Wafanyabiashara wadogo wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wakifuatilia kikao cha Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo mhandisi Tumaini Magessa wakati wa uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogowadogo wilayani humo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad