HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, January 31, 2019

NMB yakabidihi msaada wa madawati Sekondari ya Magawa na vifaa vya ujenzi Zahanati ya Nganje, Mkuranga

Na Ripota wetu, Mkuranga

BENKI ya NMB imekabidhi msaada wa viti na madawati 50 kwa Shule ya Sekondari Magawa pamoja na baadhi ya vifaa vya ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Nganje Wilaya ya Mkuranga vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 10.

Vifaa hivyo vilikabidhiwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Kitengo cha Biashara ya Serikali wa NMB, Bi. Vicky Bishubo kwa Naibu Waziri wa Nishati, Mh. Subira Hamisi Mgalu (MB) katika hafla iliyofanyika kwenye Shule ya Sekondari Magawa wilayani Mkuranga.

Akifafanua zaidi juu ya msaada huo, Bi. Vicky Bishubo alisema viti na madawati 50 yaliyotolewa kwa Shule ya Sekondari Magawa vina thamani ya shilingi milioni 5, huku mbao 520 na misumari iliyotolewa kwenye ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Nganje inathamani ya shilingi milioni 5.

Aidha aliongeza kuwa Benki ya NMB inazipa kipaumbele changamoto za sekta ya elimu na afya nchini Tanzania kutokana na umuhimu wa sekta hizo, kwa kile kuwa kama nguzo kuu ya maendeleo kwa taifa na hata nchi yoyote duniani.

"..Tunatambua juhudi za Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ya kusimamia elimu na afya kwa nguvu zote kwa kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, na pia kuboresha utoaji wa huduma za afya mijini na vijijini; tunaipongeza Serikali kwa hilo."

Alisema Serikali inafanya mambo makubwa katika sekta hizo, lakini NMB kama wadau wanawajibu wa kuunga mkono juhudi hizi za maendeleo kwa kusaidia jamii kwani kupitia jamii ndio imeifanya benki kuendelea kufanya vizuri.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Mh. Subira Hamisi Mgalu (MB) akipokea msaada huo aliishukuru Benki ya NMB kwa ukarimu wao wa kuijali jamii na kuziomba taasisi zingine zifuate nyayo za NMB katika kuisaidia jamii kwa mambo mbalimbali.

"...Nawashukuru, nawashukuru sana kwa kujitoa kwenu kwa jamii nimekuwa nikishuhudia mkisaidia jamii kupitia sekta mbalimbali, huu ni mfano wa kuigwa kwa kweli endeleeni kuisaidia jamii nasi tunaahidi kuunga mkono shughuli zenu," alisema Bi. Mgalu.
Mkuu wa Kitengo cha Biashara ya Serikali wa NMB, Bi. Vicky Bishubo akikabidhi sehemu ya madawati na viti 50 kwa Naibu Waziri wa Nishati, Mh. Subira Hamisi Mgalu (MB) kusaidia Shule ya Sekondari Magawa. Vifaa hivyo vina thamani ya shilingi milioni 5. Wanaoshuhudia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga, Juma Abeid (kushoto) na Meneja wa Tawi la NMB Mkuranga, Joseph Iramba (kulia).

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Magawa wakibeba meza na viti mara baada ya kukabidhiwa na NMB.



Mkuu wa Kitengo cha Biashara ya Serikali wa NMB, Bi. Vicky Bishubo akikabidhi sehemu ya mbao 520 na misumari kwa Naibu Waziri wa Nishati, Mh. Subira Hamisi Mgalu (MB) ikiwa ni mchango wao katika ujenzi wa Zahanati ya Nganje iliyopo wilayani Mkuranga. Vifaa hivyo vina thamani ya shilingi milioni 5. Wanaoshuhudia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga, Juma Abeid (kushoto) na Meneja wa Tawi la NMB Mkuranga, Joseph Iramba (kulia).

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Magawa wakiwa wamekalia madawati hayo mara baada ya kukabidhiwa na Benki ya NMB.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara ya Serikali wa NMB, Bi. Vicky Bishubo akizungumza katika hafla hiyo.

Naibu Waziri wa Nishati, Mh. Subira Hamisi Mgalu (MB) akiishukuru NMB kwa msaada wake.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad