HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 16 January 2019

NAIBU WAZIRI NYONGO AAMURU KUKAMATWA WAMILIKI MGODI WA NYAKAVANGALA

Na Asteria Muhozya, Iringa
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo ameamuru kukamatwa kwa Wamiliki wa mgodi wa Nyakavangala unaomilikiwa na  Thomas Masuka and Partners  kufuatia wamiliki hao kutofautiana juu ya taarifa  waliyoiwasilisha kwa Naibu Waziri kuhusu namna mgodi huo unavyoendeshwa ikiwemo ulipaji wa kodi na mrabaha wa serikali.
Aidha, Naibu waziri amewataka wamiliki hao kutoa maelezo ya kina kuhusu ni lini watalipa kodi zote wanazodaiwa na serikali baada ya kuonekana kuwa mgodi huo unadaiwa zaidi ya shilingi milioni 128 za mrabaha ambazo imedaiwa kuwa, wapo baadhi ya wamiliki ambao wamekuwa wakikusanya fedha hizo lakini zimekuwa hazilipwi.
Katika ziara yake mkoani humo, Naibu Waziri alisema kuwa pamoja na kujionea shughuli za uchimbaji katika migodi ya dhahabu ya Ulata na Nyakavangala, amebaini ukwepaji mkubwa wa kodi pamoja na mrabaha wa serikali.
Pia, amemtaka Afisa Madini kutoa maelekezo ya kina kuhusu suala zima la ulipwaji wa kodi na mrabaha wa serikali, huku akiagiza zoezi hilo pia limuhusishe Afisa Msimamizi wa madini aliyekuwepo katika kipindi ambacho fedha hizo hazikulipwa.
“Hatutaki ugomvi hapa kwenye migodi. Tunataka mgodi ufanye kazi. Dhahabu ziuzwe mahali panapoonekana. Hapa naona hesabu za viroba tu. Mnunuzi wa dhahabu hapa ni nani”, alihoji Naibu  Waziri.
Wakati akizungumza na wachimbaji katika mkutano wa hadhara, amewataka wachimbaji hao kuchimba kwa kuzingatia usalama  huku akisisitiza suala la kufuata sheria na taratibu  huku akiwataka kutoa taarifa za  uhakika kwa wale wote wanaokikuka sheria ikiwemo watoroshaji wa madini huku akisisitiza  utoaji  taarifa hizo usiwe wa majungu.
Akitolea ufafanuzi suala la fedha za mrabaha, amesema fedha hizo hazipaswi kuelekezwa katika masuala mengine na wamiliki wa migodi ikiwemo kutumiwa katika huduma za jamii badala yake  zinapaswa kulipwa serikalini. 
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela aliwataka wamiliki hao kukaa chini na kukubaliana namna ya kulipa kiasi cha fedha ambacho wanadaiwa na serikali huku akimtaka Afisa kutoka Halmashauri anayehusika na masuala ya usimamizi wa fedha kuhakikisha kwamba fedha ambazo mgodi huo ulipaswa kuzilipa kama mrabaha zinapatikana.
Mgodi huo wa Nyakavangala unamilikiwa na Thomas Masuka kwa ushirikiano na wawekezaji wengine wazawa wapatao 20. Wakati akiagiza kukamatwa kwao, wamiliki 8 kati ya 20 ndiyo walikuwa wamehudhuria kikao kati yake na wamiliki hao.
Naibu Waziri Nyongo alitoa agizo hilo Januari 15 wakat akihitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani humo.
 Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (katikati) akioneshwa jambo na wachimbaji katika mgodi wa Nyakavangala unaomilikiwa na Thomas Masuka and Partners.  Naibu Waziri alifika mgodini hapo kukagua hali ya uchimbaji madini inavyoendelea.
 Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, akikagua moja ya mgodi  katika mgodi wa Nyakavangala wakati wa ziara yake mgodini hapo. Wa tatu kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela.
 Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akimweleza jambo mmoja wa wachimbaji wakati akikagua mazingira ya uchimbaji madini katika mgodi wa Nyakavangala. Wanaomfuata ni baadhi ya wachimbaji wadogo wanaochimba katika mgodi huo.
 Naibu Waziri wa Madini Stansaus Nyongo akisisitiza jambo wakati wa ziara yake ya kukagua mgodi wa Nyakavangala. Nyuma yake ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela.
 Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akijaribu kupandisha Kamba zinazotumika kungia na kutoka ndani ya migodi katika moja ya mgodi wa dhahabu, Kavangala.
 Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela akimwonesha jambo Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati wa ziara yake ya kukagua migodi ya Nyakavangala.
 Sehemu ya wachimbaji wadogo wakifuatilia mkutano baina yao na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo. (Hayupo pichani)
 Afisa Madini anayesimamia Mikoa ya Iringa na Njombe Wilfred Machumu akieleza jambo wakati wa kikao baina ya Naibu Waziri  wa Madini Stanslaus Nyongo na wamiliki wa mgodi wa Thomas Masuka and Partners. Kulia ni Naibu Waziri Nyongo. Nayefuatia ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akimsikiliza mmoja wa wawekezaji katika eneo la Nyakavangala Kazi Kuboma alipofika  katika eneo lake ili kuona namna anavyoendesha shughuli zake  uchenjuaji madini. Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela na Maafisa Madini na Maafisa wa Wilaya.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad