HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 29, 2019

NAIBU WAZIRI MABULA ASHANGAZWA NA H/JIJI LA DODOMA KUSHINDWA KUDAI BILIONI SITA ZA WADAIWA KODI YA ARDHI

Na Munir Shemweta,  DODOMA 
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula ameshangazwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kujikita zaidi katika kuuza viwanja huku ikiacha kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa wadaiwa wa kodi ya ardhi kinachofikia bilioni sita. 

Awali Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi  alisema jiji lake limeongoza katika kukusanya mapato ambapo lilifanikiwa kukusanya bilioni saba na kati ya hizo bilioni nne nukta nane zinatokana na kodi ya ardhi. 

Akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya jiji la Dodoma katika mfulukizo wa ziara zake za kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi  leo tarehe 28 januari 2018 Dkt Mabula alisema pamoja na jiji kukusanya fedha nyingi katika idara ya ardhi kupitia uuzaji viwanja lakini  linapaswa kuhakikisha madeni ya wadaiwa sugu yanakusanywa ili kuepuka ulimbikizaji madeni. 

Naibu Waziri wa Ardhi alisema pamoja na jiji hilo kufanya vizuri lakini yeye anachelewa kulipa pongezi kutokana na kushindwa kukusanya kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa wadaiwa wa kodi ya ardhi sambamba na kushindwa kutoa ilani za madai kwa wadaiwa hao jambo linaloikosesha serikali mapato mengi. 

Kufuatia hali hiyo Dkt Mabula ameipa halmashauri hiyo ya jiji la Dodoma wiki mbili kuhakikisha inampatiwa orodha ya wadaiwa wa kodi ya ardhi waliopatiwa ilani za madai na kitu gani kimefanyika kwa wale watakaokaidi kulipa. 

Amelitaka jiji hilo pamoja na kuuza viwanja lakini linapaswa kuhakiisha linakusanya madeni na taarifa za wadaiwa wote wa kodi ya ardhi zinaingia katika vikao vya uchumi na mipango vya madiwani lengo ni kutoa nafasi ya ufuatiliaji kutoka kwa madiwani. 

"Dodoma ni uso na jicho la nchi kutokana na uamuzi uliotolewa wa kuwa makao makuu ya nchi  na watumishi mnatakiwa  kufanya kazi kwa bidii kama vile mko katika makao makuu ya nchi" alisema Dkt Mabula 

Aidha,  Naibu Waziri wa Ardhi amewataka watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri hiyo wenye madeni ya kodi ya ardhi kuwa wa kwanza kulipa madeni kabla ya kuanza kudhughulika na wadaiwa sugu kwa kuwa  wanatakiwa kuwa mfano.

Vile vile,  Dkt Mabula ameitaka halmashauri ya jiji la Dodoma kusimamia mji usichafuke ili kuepuka kuwa na jiji la ajabu na kulitaka kusimamia vyema utoaji vibali vya ujenzi sambamba na  kuhakikisha ukaguzi na unafanyika na kuwa na watu wa kuwapa taarifa maeneo yanayojengwa kiholela ili kudhibiti wanakiuka sheria za ujenzi na kusisitiza  huu siyo wakati wa kuleana na cha msingi ni kupanga mji vizuri. 

Pia Naibu Waziri wa Ardhi alikumbana na tatizo la utunzaji majalada ya ardhi usiozingatia taratibu kama alivyokuta katika halmashauri mbalimbali alizozitembelea na kuagiza upungufu uliojitokeza kurekebishwa haraka iwezekanavyo. 

Mkuu wa Idara ya Ardhi, Mipango Miji na Maliasili katika halmashauri ya jiji la Dodoma Joseph Mafuru alisema jiji hilo katika mwaka uliopita limefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 7. 196 ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni  4. 8 zimetoka katika kodi ya pango la ardhi na katika kipindi cha kuanzia januari mwaka huu tayari  imekusanya shilingi bilioni 1. 194 

Mkuu huyo wa idara ya ardhi alisema halmadhauri hiyo ina jumla ya migogoro 2136 na kati ya hiyo 1541 ishapatiwa ufumbuzi huku migogoro 595 ikiendelea kutatuliwa. 

Kwa upande wake Katibu Tawala wa wilaya ya Dodoma Edward Mpogolo alisema halmashauri ya jiji la Dodoma imekuwa ikifanya kazi nzuri lakini imekuwa ikukambana na baadhi ya changamoto Kama ucheleweshaji ulipaji fidia  katika baadhi ya maeneo yaliyo twaliwa na serikali kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Ametolea mfano wa sehrmu ya eneo la Iyumbu mkoani Dodoma ambalo  limetwaliwa kwa ajili ya shughuli mbalimbaki kama vile  barabara na eneo la  kuzikia (makaburi). 

Alisema,  hali hiyo inawafanya wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa kutojua hatma ya malipo yao na hivyo kuwafanya kuishi kwa mashaka. 
  Naibu Waziri wa Ardhi Nyumaba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimpa maelekezo Mtunza kumbukumbu wa halmashauri ya jiji la Dodoma Rashid Chikawe katika ofisi za idara ya ardhi wakati alipofanya ukaguzi katika majalada ya ardhi kwenye jiji hilo leo tarehe 28 Januari 2019 kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. wa pili kulia ni Katibu Tawala wa wilaya ya Dodoma Edward Mpogolo

 Watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya jiji la Dodoma wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipofanya ziara katika halamashauri hiyo kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi.
 - Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwasili katika halamashauri ya jiji la Dodoma kuzungumza na watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri hiyo kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad