HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 29, 2019

MAKONDA AWAAGIZA WAKUU WA WILAYA KUHAKIKISHA UGAWAJI WA VITAMBULISHO VILIVYOTOLEWA NA RAIS MAGUFULI UNAMALIZIKA KABLA YA MWEZI MACHI

* Atoa tahadhari katika kipindi hiki cha mvua
MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amewaagiza wakuu wa Wilaya zote 5 kuhakikisha hadi kufikia Mosi, Machi mwaka huu kila mfanyabiashara ndogondogo anakuwa na Kitambulisho cha utambuzi kilichotolewa na Rais Dkt. John Magufuli na kuwataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo ambayo haina malipo.

 Makonda amesema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokutana na viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya kata na kueleza kuwa baada ya Tarehe 01/03/2019 mfanyabiashara yeyote atakayekutwa bila kitambulisho, leseni ya manispaa au vielelezo vya kulipa kodi toka TRA atajikuta mikononi mwa vyombo vya dola kama muhujumu Uchumi.

Sambamba na hayo Makonda  amegawa vitambulisho vya wafanyabiashara ndogondogo kwa Wakuu wa Wilaya na kufanya mkoa huo kuwa kinara kwa kupokea takribani vitambulisho 175,0000 kutoka kwa Rais Magufuli.

Aidha  Makonda amesema baada ya 01/03/2019 serikali ya Mkoa itawaingiza wafanyabiashara hao katika mfumo wa kisasa (Database) utakaowezesha serikali kuwafikia na kuwapa mafunzo ya namna kukuza biashara zao ili waweze kufikia uchumi wa Kati.

Pamoja na hayo amewatahadharisha watendaji wanaowatoza kiasi kikubwa cha fedha za vitambulisho tofauti na bei elekezi ya sh. 20,000 huku akiwahimiza wafanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo waliyopewa na Rais.

Mbali na Vitambulisho  Makonda ametoa miezi miwili kwa Wakurugenzi wa Manispaa kuhakikisha Leseni za wafanyabiashara zinaingizwa katika mfumo mmoja ikiwa ni pamoja na kuharakisha utoaji wa leseni ili kupunguza usumbufu kwa wananchi.

Vilevile ametoa tahadhari kwa wakazi wa Dar es Salaam kuchukua hatua katika kipindi hiki cha mvua kwa kuhakikisha wanafuatilia matangazo yanayotolewa na mamlaka ya hali ya hewa pamoja na kutojenga mabondeni pamoja na kuhama maeneo hatarishi ili kubaki salama.
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akizungumza na watendaji wa Mkoa katika kikao kilichowakutanisha na kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo jijini hapo.
 Watendaji wa Mkoa wa Dar es Salaam wakifuatilia mkutano uliowakutanisha na Mkuu wa Mkoa na kujadili changamoto na namna ya kuzitatua, leo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda (kulia) akimkabidhi kasha la vitambulisho  Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema (kushoto) leo jijini Dar es Salaam, katikati ni Katibu Tawala Mkoa wa Dar es salaam Abubakar Kunenge.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad