HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 2, 2019

MAJALIWA AWASILI SONGEA KUANZA ZIARA YA KIKAZI MKOANI RUVUMA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Ruvuma uhakikishe kuwa vijana wote wanaomaliza darasa la saba kwenye kila Halmashuri za mkoa huo wanakwenda kuanza kidato cha kwanza. Aametoa agizo hilo leo (Jumatano, Januari 2, 2018) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Ruvuma baada ya kuwasili kwenye uwanja ndege wa Songea kuanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Ruvuma.

Waziri Mkuu amesema Halmashuri zote za mkoa huo zijikite katika kujenga madarasa ili wanafunzi wote waliofaulu ambao wanatakiwa kwenda sekondari waende. Amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa dhati kuahakikisha kwamba watoto wote wenye sifa za kupata elimu ya seondari wanapata elimu hiyo kote nchini hivyo juhudi za makusudi lazima zifanywe na kila Halmashauri ili kutimiza azma.

Akizungumzia suala la utoro shuleni, Waziri Mkuu amesema hilo ni moja kati ya maeneo yanayozorotesha juhudi kubwa za Serikali za kuwapatia watoto wa Tanzania elimu katika maeneo mengi nchini na lazima viongozi wa wilaya na mikoa wasimame imara ili kukomesha hali hiyo. Amesema viongozi wa ngazi zote katika mikoa na wilaya ndiyo hasa wanaoweza kumaliza tatizo la utoro wakishirikiana kwa karibu na wanavijiji ambao wanaishi na watoto hao na wanajua ni watoto wangapi hawaendi shule.

Hivyo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kutoa maelekezo na miongozo itakayowabana watoto watoro pamoja na wazazi au walezi wao kwani wanayo mamlaka na uwezo wa kuchukuwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi. Akizungumzia zao la korosho , Waziri Mkuu amewataka viongozi wa mkoa wa Ruvuma kuwaondolea hofu wananchi wanaolima zao hilo katika mkoa huo kwa kuwahakikishia kwamba Serikali inazo fedha za kutosha kununua korosho zote ziliyovunwa na wakulima.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato ya Serikali, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa mikoa na wilaya kubeba dhamana waliyopewa na Taifa ambayo ni pamoja na kusimamia ukusanyaji mapato ya Serikali kwa kishirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). "Halmashauri zote na wakuu wa wilaya wasimamie kwa dhati ukusanyuaji wa kodi."

Akiwa mkoani Ruvuma, Waziri Mkuu kesho anatarajiwa kufungua soko la mazao la Lilambo katika wilaya ya Songea, kufungua ghala la mazao la Mgazini na kuweka jiwe la msini la ujenzi wa zahanati ya Luganga na kisha kuhutubia mkutano wa hadhara.

Keshokutwa Waziri Mkuu ataongoza kikao cha wadau wa zao la kahawa kitakachowashirikisha pia Waziri wa Kilimo na Mrajisi wa Ushirika. Wengine watakaoshiriki katika kikao hicho ni viongozi wa AMCOS, UNION na viongozi wa Bodi ya kahawa.
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme wakati alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Songea kuanza ziara ya kikazi mkoani  humo, Januari 2, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary (wapili kulia) wakisalimiana  na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho  wakati walipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Songea kuanza ziara ya kikazi mkoani humo, Januari 2, 2018. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, ambaye pia ni Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama na watatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina, Mndeme. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Viongozi wa Mkoa wa Ruvuma wakati alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Songea kuanza ziara ya kikazi mkoani humo, Januari 2, 2018. Kulia ni mkewe Mary na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad