HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 21 January 2019

MADIWANI SIMANJIRO WAMFAGILIA RAIS MAGUFULI

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, limesoma maazimio ya kumpongeza Rais John Magufuli kwa kutatua migogoro ya maeneo ya hifadhi na vijiji 366 na kurejesha kikokotoo cha awali cha wastaafu. Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi akisoma maazimio hayo, alisema baraza hilo linampongeza kwa dhati Rais Magufuli kutokana na matukio hayo mawili. 

Myenzi alisema baraza limeona maamuzi hayo ya Rais Magufuli ni kielelezo tosha cha uongozi mahiri, uliotukuka na sikivu kwa wananchi wanyonge ambao ni nguzo muhimu ya ujenzi wa Taifa. Alisema uamuzi wa kurejesha kikokotoo katika utaratibu wa awali, ni kielelezo tosha cha uongozi mahiri na kutatua migogoro ya watumiaji wa ardhi na mipaka ya maeneo ya hifadhi ni ya kupongezwa. 

"Kwa upendo huu aliouonyesha mheshimiwa Rais Magufuli, baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro linampongeza kwa dhati na kuomba aendelee na moyo huu wa upendo kwa Taifa lake," alisema Myenzi. Diwani wa kata ya Terrat, Jackson Ole Materi alisema mgogoro wa hifadhi na vijiji 366 ulikuwa unaathiri ustawi wa wananchi hasa jamii za wafugaji, wakulima, wavuvi na watumiaji wa ardhi katika mipaka ya vijiji na maeneo ya hifadhi. 

Ole Materi alisema kwa uamuzi huo imedhihirika azma ya Rais Magufuli ya kuwajali wanyonge na kuhakikisha jamii yenye utulivu inayotumia muda mwingi kwa uzalishaji badala ya kutatua migogoro. Diwani wa kata ya Loiborsiret, Ezekiel Lesenga (Mardad) alisema wananchi wa eneo hilo nao wanampomgeza Rais Magufuli kwa uamuzi wake kwani nao ni waathirika wa ardhi. 

Mardad alisema kwenye kijiji cha Kimotorok kuna taasisi mbalimbali ikiwemo shule, zahanati, kanisa na makazi ya watu waliotakiwa kufukuzwa sababu ya kupakana na hifadhi ya jamii ya Mkungunero. Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Albert Msole alisema baraza hilo linaundwa na jamii ya wafugaji na wakulima linampongeza Rais Magufuli na kumtakia maisha marefu na ufanisi kwenye majukumu yake. 

Msole alisema wilaya ya Simanjiro nayo ni miongoni mwa wanufaika wa matamko hayo mawili kwani watumishi wa serikali wamenufaika na wafugaji pia wamefaidika. 

Diwani wa kata ya Emboreet, Christopher Kuya alisema Rais Magufuli amejali maslali na matakwa ya wafanyakazi ambao walikuwa waathirika wakubwa pindi wakistaafu. 

"Uamuzi huu wa Rais Magufuli ni kielelezo tosha cha uongozi wake thabiti na sisi madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro tunampongeza mno," alisema Kuya. 
 Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhe Albert Msole akifunga kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo ambao walimpongeza Rais John Magufuli kwa kuwatetea wafugaji na watumishi wa serikali, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Yefred Myenzi. 
 Diwani wa kata ya Loiborsiret Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Ezekiel Lesenga Mardad akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kwa kumpongeza Rais John Magufuli kwa kuwatetea wafugaji hasa kijiji cha Kimotorok kjnachopakana na hifadhi ya jamii ya Mkungunero. 
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Yefred Myenzi akisoma maazimio ya Baraza la Madiwani la kumpongeza Rais John Magufuli kwa kuwatetea wafugaji na watumishi, kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Albert Msole. 
 Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara na watumishi wa Halmashauri hiyo wakifuatilia kikao cha Baraza la Madiwani. 
Diwani wa kata ya Terrat wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Jackson Ole Materi akisoma taarifa ya hoja ya kumpongeza Rais John Magufuli kwa kuwatetea wafugaji na watumishi wa serikali.  

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad