HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, January 18, 2019

MADINI KUWEKA MSUKUMO MIRADI YA LIGANGA, MCHUCHUMA

Na Asteria Muhozya, Ludewa
Wizara ya Madini imesema itashirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) kuweka msukumo ili kuhakikisha  kwamba miradi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma na ule wa Chuma Linganga inaanza kutekelezwa.
Kauli hiyo ilitolewa Januari 16 na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za madini mkoani Njombe  na kuona namna ya kutatua changamoto  zinazohusu Wizara ya Madini   katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema miradi hiyo ni moja ya miradi ya kimkakati ambayo Taifa linatarajiwa kunufaika kwa kiasi kikubwa, hivyo kutokana na umuhimu wake, wizara ya madini itashirikiana na wizara hiyo kuhakikisha hatua zaidi zinapigwa ili hatimaye miradi hiyo ianze kutekelezwa kwa kuwa imechukua muda mrefu.
Aliongeza kuwa, ni miradi mikubwa ambayo taifa linatarajiwa kunufaika nayo  kupitia ajira  na kuongeza pato la nchi huku akiyataja madini ya chuma kuwa  moja ya malighafi muhimu kwa uchumi  wa Tanzania ya viwanda  na kusema kuwa, kama taifa, linautolea macho mradi huo na kwamba serikali imedhamiria kuutekeleza.
Aliongeza kwamba, katika Serikali ya Awamu ya Tano, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli anayo imani kubwa  kuwa  miradi hiyo itaanza huku  serikali ikitegemea  kupeleka  maendeleo  kwa wananchi kupitia miradi husika.

 “Wizara yetu ndiyo inatoa leseni za madini na tayari tulishatoa leseni ya Makaa ya mawe mchuchuma kwa hiyo nimefika kuangalia changamoto ambazo ziko upande wa wizara yetu kuweza kuzitatua ili tutoke hapa. Miradi hii tumeisikia miaka mingi ni wakati sasa tunataka ianze.” alisisitiza Nyongo. 
Aliongeza kuwa, ikiwa wizara ndiyo inatoa leseni za madini,  inaowajibu wa kujua yule aliyepewa leseni kama anaifanyia kazi na kuongeza, “Sisi tuliotoa leseni lazima tuangalie tuliyempa leseni amekwama wapi  lakini pia tujue  miradi hii inaanza lini? Makaa ya mawe na chuma vyote vinahitajika kwa taifa. Tunatambua makaa ya mawe ni madini ambayo yana tija kwa uchumi kwa nchi,” alisema Nyongo.

Akifafanua zaidi kuhusu miradi hiyo alisema kuwa, mradi wa Makaa ya Mawe unatarajiwa kuzalisha umeme ambao mbali ya kuuza kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), umeme huo unatarajia kutumika katika kuzalisha madini ya Chuma Liganga.
 “ Mpango ni Liganga kutumia megawati 250 kwa shughuli zake za kuzalisha chuma na megawati 350 zitauzwa Tanesco kuzalisha umeme,” aliongeza. 
Akifafanua sababu za kuchelewa kwa miradi hiyo, alisema ni kutokana na changamoto za kimkataba ambazo bado ziko katika majadiliano katika ngazi za juu na kuitaja baadhi ya mikataba hiyo kuwa ni  kuwa ni pamoja na mikataba ya upunguzaji wa kodi.
Aliongeza kuwa, wizara ya madini ikiwa ni wizara ambayo inasimamia Sheria ya Madini, imelenga kuhakikisha kwamba miradi hiyo mikubwa inaanza ili hatimaye iweze kuwanufaisha watanzania na taifa.
Akielezea suala la fidia kwa wananchi waliopisha miradi hiyo, alianza kwa kumpongeza Mkuu wa Wilaya ya Ludewa kwa kutenganisha suala la miradi hiyo na fidia  ambapo alisema kwamba taratibu za juu zikikamilika, wananchi watalipwa fidia  na hivyo kuwataka kuwa na subira na kuwa tayari kupisha utekelezaji wa miradi hiyo.
Awali,  Mkuu wa Mkoa wa Njombe , Christopher Ole Sendeka alimweleza waziri umuhimu wa wizara ya madini kujielekeza  kwenye kupata taarifa halisi kuhusu tafiti zilizofanyika awali kuhusu  akiba iliyopo ya madini ya chuma  Liganga na Makaa ya Mawe mchuchuma. 
Aidha, aliongeza kuwa, mbali na chuma na makaa ya mawe mkoa huo unayo madini mbalimbali ikiwemo dhahabu ambayo bado haijachimbwa kwa kiasi kikubwa.
Miradi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma na Chuma Liganga, inatekelezwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na kampuni ya Sichuan Hongda Group Ltd, ya China.
Pia, akiwa mkoani humo, Naibu Waziri alitembelea mgodi wa Kokoko Kokoto wa Nyakamtwe Quary, ambapo alitoa changamoto kwa mmiliki wa mgodi huo kuongeza kasi ya uzalishaji na kuwa wabunifu kutumia fursa  za miradi mikubwa ya ujenzi  inayotekelezwa na serikali ikiwemo ya ujenzi wa reli ili kokoto hizo ziweze kutumika.
 Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akimsikiliza Meneja wa mgodi wa Kokoto wa Nyakamtwe Quary, uliopo mkoani Njombe   alipoutembelea wakati wa ziara yake hivi karibuni. Mhagama ni mmoja wa wanufaika wa ruzuku iliyotolewa awali na Serikali  kwa wachimbaji wadogo . Wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Songea, Ruth Msafiri.
 Mtaalam kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Mhandisi Paschal Malesa, akimweleza jambo Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati alipotembelea mradi wa Liganga uliopo Wilayani Ludewa mkoani Njombe. Naibu Waziri Nyongo alitembelea kujua maendeleo ya utekelezaji mradi huo ikiwemo kujua changamoto ambazo  ziko upande wa Wizara inaweza  ili izifanyie kazi kuhakikisha kwamba mgodi huo unatekelezwa kama ilivyopangwa.
 Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akiangalia makaa ya katika mgodi wa Liganga alipoutembelea hivi karibuni. Naibu Waziri alifanya ziara hiyo kwa lengo la kujua changamoto za utekelezaji wa mradi huo. Anayemweleza jambo ni Mtalaam kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Mhandisi Paschal Malesa.
 Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka akimsikiliza akimweleza jambo Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati wa ziara yake mkoani humo.
 Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akitoka katika Ofisi za Wilaya ya Ludewa  tayari kwa ziara ya kutembelea katika mgodi wa Liganga kwa ajili ya kujionea changamoto za utekelezaji wa mradi huo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Andrea Tsere.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini wakifuatilia kikao baina yake na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka. (hayupo pichani) Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad